MMOJA wa watu wenye ulemavu wa ngozi, albino na
mwanahabari shupavu kutoka kampuni ya Mwananchi Communication, Henry
Mdimu amejitolea kuwa balozi wa hiyari kupinga mauaji ya kikatili ya
watu wenye albino yanaoendelea nchini.
Bw.
Mdimu ambaye ameungwa mkono na baadhi ya marafiki na watu wanaokerwa na
vitendo hivyo, ikiwemo Chama cha Bloggers nchini, Tanzania Bloggers
Network (TBN) amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kushuhudia ndugu
zake wakiteseka kwa muda mrefu dhidi ya mauaji hayo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Balozi Mdimu amesema
lengo lake kuu ni kuhakikisha anazunguka pamoja na marafiki watakao
muunga mkono na kutoa elimu kwa kuanzia Kanda ya Ziwa ili tatizo hilo
lisiendelee kuenea nchi nzima.
Akifafanua zaidi
alisema mauaji ya watu wenye albino yanaichafua Tanzania hivyo
atahakikisha anaisaidia Serikali kupambana na watu wenye imani hizo za
kipuuzi ili kuondoa doa linaloichafua nchi yetu ambayo imekuwa na sifa
ya amani dunia nzima.
"...Nimeamua kufanya hivi
baada ya kushuhudia ndugu zangu wakiteseka kwa muda mrefu. Awali
nilishindwa kuanzisha harakati hizi nikiamini kuna vyombo vinavyohusika
na utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi."
"...Hivyo
nimeamua niweke jitihada zangu binafsi niisaidie Serikali yangu katika
kuondoa doa hili linaloichafua Nchi yetu yenye sifa ya Amani duninia
nzima. Hivyo nawaomba Watanzania wenzangu mniunge mkono tukishirikiana na Serikali ili mauaji haya yakome," alisema Mdimu.
"Kutokana
na ushawishi nilionao kama Mwandishi, Mtangazaji wa redio na Blogger
naamini nitaleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha haki ya kusihi
kwa ndugu zangu inaheshimiwa na kubaki historia. Salamu zangu ziwafikie
wanyanyasaji, wauaji na wenye kufanya dhihaka kwa watu wenye ulemavu wa
ngozi kuwa IMETOSHA."
Akifafanua zaidi alisema
kwa uchunguzi wake wa awali umebaini ukosefu wa elimu juu ya watu wenye
ulemavu wa ngozi ndio chanzo cha tatizo hilo kukua na hatimaye kuuana
kwa imani za kishirikina. "...Hivyo basi, silaha ya Elimu ni sehemu
kubwa ya haraki hizi," alisisitiza Balozi huyo wa kujitolea.
Aidha
alisema kuendesha harakati hizo alizozipa jina la 'IMETOSHA' elimu
itatolewa kwa njia ya sanaa, na washauri nasaha pamoja na kundi la
wanamuziki ambao pia wataandaa nyimbo mbalimbali za kutoa mafunzo ya
kutokomeza ukatili huu.
Alisema wasanii ambao
hadi sasa wamejitokeza kuunga mkono kampeni hizo ni paoma na Jhikoman,
Kassim Mganga, Profesa J, Ray C, Fid Q, Roma Mkatoliki na Dami Msimamo.
Hata
hivyo alisema bado pia anaamini nguvu ya vyombo vya habari ikiungana na
kampeni hizo wanaweza kufanikiwa zaidi hivyo kuomba ushirikiano katika
kuhakikisha vinapaza sauti kutokomeza mauaji hayo ya kikatili.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni