.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 18 Machi 2015

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NCHI ZA NJE WA MAREKANI ANAYESHUGHULIKIA USALAMA WA RAIA, DEMOKRASIA NA HAKI ZA BINAADAMU ATAEMBELEA KITUO CHA VIJANA MUEMBE MADEMA - ZANZIBAR

Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Marekani anaeshuhulikia masuala ya Usalama wa Raia, Demokrasia na haki za Binadam Bi. Sarah Sawell akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) alipofika katika kituo cha Vijana muembe madema Mjini Zanzibar.


Serikali ya Marekani imeamua kuwatembelea Vijana wa Bara la Afrika kwa lengo la kukaa nao pamoja na kuzungumza nao juu ya Changamoto na Matatizo yanayowakabili vijana hao.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Kituo cha Vijana iliyopo nyuma ya Kituo cha Polisi Madema, Wilaya ya Mjini Unguja.

Amesema vijana wanakabiliwa na matatizo mengi kwa sasa yanayowafanya kukata kabisa tamaa ya maisha na badala yake kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi, ujambazi na wengine kuweza kutumiwa na makundi maovu yasiyo na tija kwao.

Aidha amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ndio tatizo kubwa zaidi duniani jambo ambalo lilimfanya Rais wa Marekani Barack Obama wiki 3 zilizopita kuitisha mkutano wa pamoja wa Dunia ili kujadili masuala ya vijana ambapo Taasisi Mbalimbali za Kiserikali na Binafsi Duniani zilishiriki katika mkutano huo.

Amefahamisha kuwa lengo la ziara yake barani afrika ni kuyaendeleza kwa kuyafikisha kwa vijana yale yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo ili kuwaonesha njia ya mafanikio vijana hao pamoja na kuwapa msaada pindi utakapohitajika.


Akizungumzia kuhusiana na mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) nchini Tanzania amesema Serikali yake imeshachukua hatua mbalimbali katika kulinda haki za binadamu duniani kote kwa kuwapatia ulinzi na usalama wakiwemo hao albino ila juhudi zaidi za kuwalinda zinatakiwa kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa albino wanakuwa katika usalama zaidi.

Akigusia kuhusu mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Tanzania amesema Serikali ya Marekani imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uchaguzi hivyo itaendeleza na jitihada hizo ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa katika hali ya usalama na amani na kuepukana na vurugu zisizo za lazima.

Nae Mwenyekiti Mtendaji wa Vituo vya Vijana Tanzania Nd. Abdalla Miraji Othman amesema vituo vyao kwa sasa vinakabiliwa na Changamoto nyingi ikiwemo usafiri pamoja na posho na mishahara kwa wafanyakazi wa vituo hivyo kwani huwa havitolewi kwa wakati jambo ambalo linarejesha nyuma kwa kiasi kikubwa jitihada zao za kuwaokoa vijana kutokana na vitendo viovu.

Akitoa wito wake Nd. Othman amesema ipo haja kwa Benki za Kitanzania kupunguza masharti ya kutoa mikopo pamoja na Riba ili vijana wamudu kuchukua mikopo katika Benki hizo kwa lengo la kujiajiri na hatimae kujikomboa kimaisha.

Amesema Ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall ilikua ni ya Siku 1 Visiwani Zanzibar ambapo ziara hiyo inatrajiwa kufanyika takriban bara lote la Afrika kwa lengo la kukutana na vijana na kuzungumza nao juu ya masuala mbalimbali.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO- ZANZIBAR

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni