SERIKALI imeyapokea maombi ya kikao
cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) cha Mkoa wa Mbeya yanayopendekeza
mkoa huo ugawanywe na kupata mikoa miwili ya Mbeya na Songwe.
Akizungumza na maelfu ya wananchi
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Jumamosi, Februari 28,
2015) kwenye uwanja wa Saba Saba wilayani Chunya, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda alisema Serikali imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa
mkoa huo ambao una kilometa za mraba 63,000.
“Tumekwishapokea maombi ya
kuugawanya mkoa wa Mbeya kwa sababu mkoa huu una eneo la kilometa za
mraba 63,617 zilizogawanyika katika Wilaya 8 na Halmashauri 10. Hili
ni eneo kubwa sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma
maendeleo,” alisema.
Alisema kamati hiyo imeshauri mkoa
huo ugawanywe katika wilaya nne nne ambapo mkoa mpya wa Songwe
utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya. Wamekubaliana
kuwa makao makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa chunya mmeenda mbali
zaidi kwa kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya
ambapo chunya itaenda Mbeya,” alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
Alisema katika kikao hicho
ilikubaliwa kwamba makao makuu ya wilaya mpya ya Songwe yatakuwa
Mkwajuni. “Nimekubali maombi haya kwa sababu yatapunguza gharama za
uendeshaji, na kama itashindikana kupata wilaya mpya basi itabidi
tuwape Halmashauri ya Songwe,” alisema.
Mkoa wa Mbeya una wilaya nane ambazo
zimegawanyika katika tarafa 27, kata 262, vijiji 842 na mitaa 252.
Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012
ni 2,707,410.
Akizungumzia kuhusu mpango wa maji
katika wilaya hiyo, Waziri Mkuu alisema bado kuna changamoto kubwa ya
kufikisha maji vijijini ambako upatikanaji wake uko kwenye asilimia
46. “Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa vitatu na mwakani tuna
mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11, tunachohitaji ni fedha
na usimamizi,” alisema.
Alivitaja vijiji viyakavyopata
visima hivyo ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala, Isangawana, Galula,
Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile, Bitimanyanga na
Mapogoro.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezindua
maabara tatu katika shule ya sekondari ya Saza ambazo zimejengwa kwa
ufadhili wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya, Bi. Sophia Kumbuli alisema
ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu sh. Milioni 268.5 vikijumuisha
pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi.
“Kati ya hizo sh. Milioni 23.5 ni
za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali na sh. Milioni 245 ni
ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji na gesi,”
alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara
yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya
kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua
ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na
usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, MACHI MOSI, 2015
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni