.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 29 Aprili 2015

DK. SHEIN:MATIBABU YA UBONGO NA UTI WA MGONGO NI HATUA MUHIMU YA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Ujumbe wa Watalaamu Mabingwa wa Magonjwa ya Kichwa, Uti wa Mgongo na Matibabu ya Maumivu kutoka nchi za Afrika Mashariki ukiongozwa na Dk.Mahmoud Qureshi pia Makamu wa Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Mafunzo Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu ulipofika Ikulu Mjini Zanzibar jana,

                                                                                           [Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuanza kwa huduma ya matibabu ya ubongo na uti wa mgongo katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ni hatua muhimu katika kufikia lengo la Mpango wa Serikali wa kuifanya hospitali hiyo kuwa hospitali kamili ya rufaa.
 

Akizungumza na ujumbe wa wataalamu wa magonjwa ya kichwa na uti wa mgongo kutoka nchi za Afrika Mashariki Ikulu jana, Dk. Shein alisema amefurahishwa na namna Kituo cha Matibabu ya Ubongo na Uti wa Mgongo katika hospitali ya Mnazi Mmoja kilivyopata mafanikio ya haraka katika kipindi kifupi tangu kilipoanzishwa.
 

Aliupongeza uongozi wa Wizara ya Afya kwa kuitumia vyema fursa iliyopata Zanzibar ya msaada wa kuanzisha kituo hicho ambacho ni cha pekee nchini Tanzania.
 

Aidha Dk. Shein aliipongeza taasisi inayoshughulikia matibabu ya uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hispania (Neurosurgical Education Foundation-NED) kwa msaada wake hadi kufanikisha ujenzi na kituo kicho.
 

Dk. Shein aliueleza ujumbe huo ambao ulifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali na Mnazi Mmoja Dk. Jamala Adam Taibu kuwa anapata faraja kuona hatua kwa hatua malengo ya Serikali ya kuimarisha huduma za rufaa katika hospitali hiyo yanatekelezwa.
 

Alifafanua kuwa wakati akifungua kikao cha kwanza cha Baraza la Wawakilishi mara baada ya kuunda Serikali mwaka 2010 aliahidi kuanzisha huduma tatu kuu nchini ambazo ni upasuaji wa moyo, matibabu ya njia ya chakula, na maradhi ya njia ya mkojo na figo.
 

Alibainisha kuwa kati ya huduma hizo ni huduma ya upasuaji moyo ndio maandalizi yake hayajakamilika lakini mengine maandalizi yamekamilika na utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali na za kutia moyo sana.
 

Ni jambo la kujivunia aliueleza ujumbe huo kuona sasa kituo cha Matibabu ya Ubongo na Uti wa Mgongo katika hospitali hiyo kinaweza kuvutia wataalamu kutoka nchi za nje hivyo kutoa fursa kwa madaktari nchini kujifunza kutoka wataalamu hao.
 

Kwa hivyo alitoa wito kwa madaktari vijana kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo ipasavyo kujifunza na kupata utaalamu hadi kuwa mabingwa katika fani hiyo.
 

Aliukumbusha tena uongozi wa hospitatli hiyo kuzingatia mambo makuu ya hospitali ya rufaa ambayo ni kutoa huduma, kutoa mafunzo na kufanya tafiti na kusisitiza kuwa kwa kuzingatia hayo hospitali itakuwa imetimiza majukumu yake ipasavyo.
 

Katika maelezo yake kwa Mheshimiwa Rais, Dk. Jamala alieleza Kituo cha Matibabu ya Ubongo na Uti wa Mgongo cha hospitali ya Mnazi Mmoja kilikuwa mwenyeji wa semina ya siku mbili ya Watalaamu Mabingwa wa Magonjwa ya Kichwa, Uti wa Mgongo na Matibabu ya Maumivu kutoka nchi za Afrika Mashariki iliyofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 25 Aprili, 2015.

 

Alifafanua kuwa pamoja na kutoa huduma za upasuaji lakini pia kituo kinatoa mafunzo kwa watalaamu wa humu nchini ikiwemo kupitia semina kama hiyo.
 

Akitoa takwimu za huduma za upasuaji zilizotolewa hadi sasa, Dk. Jamala alieleza jumla wagonjwa 713 wamefanyiwa huduma za upasuaji wakiwemo watoto 212 waliofanyiwa upasuaji wa vichwa na wengine 78 upasuaji wa utii wa mgongo.
 

Wagonjwa wengine walifanyiwa upasuaji wa kuondosha uvimbe katika ubongo(62),upasuaji uti wa mgongo (183), upasuaji wa kichwa kuondoa damu viza(53), kuondoa uvimbe wa mafuta na saratani ya damu (51) na upasuaji wa magonjwa mengine (74)

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji mishipa ya fahamu kutoka hospitali ya Aga Khan mjini Nairobi Dk. Mahmoud Qureshi alisema amefurahishwa na namna Mheshimiwa Rais wa Zanzibar anavyounga mkono jitihada za kituo hicho ambacho sasa kimekuwa cha kikanda.
 

Dk. Qureshi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Mafunzo Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu, alibainisha kuwa taasisi yao ilitiwa moyo sana na rai alizozitoa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar wakati alipokifungua kituo hicho mwanzoni mwa mwaka huu.
 

Kwa hivyo alisema semina iliyomalizika hivi karibuni ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa rai hizo za Mheshimiwa Rais kwa taasisi yao na ndio maana wameona fahari kufadhili usafiri na malazi kwa washiriki toka nje ya Zanzibar. 

Nchi washiriki wa semina hiyo walitoka Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania bara, Zimbabwe, Zambia na wenyeji Zanzibar.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni