Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na Balozi mdogo wa Oman Sheikh Ali Al-Rashdi, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisi kwake Migombani.
(Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu mchango unaotolewa na serikali ya Oman katika kuiendeleza Zanzibar kwenye sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu.
Akizungumza na balozi mdogo wa Oman sheikh Ali Al-Rashdi ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango huo ambao unalenga kuwaongezea ujuzi wananchi wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa Serikali ya Oman imekuwa kigezo kizuri cha utoaji wa elimu kwa Zanzibar, kwani imekuwa ikitoa nafasi za masomo “scholarships’ kwa njia ya mtandao, jambo ambalo linatoa fursa sawa kwa kila mwenye sifa za kuomba nafasi hizo, na kuondokana na dhana ya kuwepo upendeleo katika upatikanaji wa fursa za elimu nchini.
Amesema nafasi za masomo zinazotolewa kupitia mfuko wa elimu wa Sultan Qaboos wa Oman, zimekuwa zikiwasaidia vijana wa Zanzibar kuongeza ujuzi katika fani mbali mbali, hatua ambayo itarahisisha maendeleo ya nchi.
Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameelezea kuridhishwa na jinsi Oman inavyofanya juhudi za kukijengea uwezo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), na kwamba itakifanya chuo kicho kiweze kutoa elimu bora zaidi.
Aidha Maalim Seif ameishukuru Oman kwa kuiendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili, na kuongeza kuwa Oman imekuwa miongoni mwa nchi za kigeni zinazozungumza zaidi lugha hiyo ya Taifa ya Tanzania.
Kwa upande wake balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Ali Al-Rashdi amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa Serikali ya Oman imekuwa ikitoa misaada hiyo kwa Zanzibar, ikielewa kwamba inatekeleza wajibu wake kwa ndugu zao wa Zanzibar wenye historia ndefu.
Amesema Oman na Zanzibar zina uhusiano wa kindugu wa muda mrefu, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo kuendelea kuwa karibu na Zanzibar, na kutaka uhusiano huo uimarishwe zaidi.
Ameeleza kuwa Oman inakusudia kujenga taasisi kubwa ya elimu itakayotoa taaluma mbali mbali zikiwemo za dini na sayansi katika eneo la Tunguu, baada ya kukamilika ujenzi wa msikiti mkubwa unaoendelea katika chuo cha Kiislamu Mazizini.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni