Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akifungua pazia kuashiria ufunguza
rasmi wa MASJID AQSAA katika kijiji cha Kiboja Mkwajuni, Wilaya ya
Kati Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia waumini wa dini ya
Kiislamu waliohudhuria ufunguza wa MASJID AQSAA katika kijiji cha
Kiboja Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi wa dini ya kiislamu nchini
pamoja na waislamu mbali mbali wakisikiliza hotuba ya Ijumaa
iliyotolewa na Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraha
(hayupo pichani) katika msikiti mpya wa MASJID AQSAA ulioko Kiboja
Mkwajuni. Kushoto ni Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji akifuatiwa na
Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kabi.
Na. Mwandishi wa OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewasisitiza waislamu nchini kuachana
na tabia ya kugombania misikiti, kwani haisaidii kuendeleza dini
hiyo.
Amesema misikiti ni nyumba za
Mwenyezi Mungu, hivyo hakuna sababu kwa waislamu kulumbana kwa sababu
za kugombea uongozi au kutokana na tofauti ya kimadhehebu.
Maalim Seif ametoa nasaha hizo
wakati akifungua msikiti wa Ijumaa MASJIDIL AQSAA katika kijiji cha
Kiboje Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema Uislamu ni dini yenye
nidhamu kamili, na kuwataka waumini wa dini hiyo kufuata nidhamu hizo
katika kuendesha mambo yao bila ya kukaribisha malumbano na
mifarakano baina yao.
Amewahimiza waislamu wa eneo hilo
kuuimarisha na kuuendeleza msikiti huo kwa kuendeleza harakati za
darsa, sambamba na kuwaandalia watoto muda wa kutosha kuweza
kuhudhuria katika darsa hizo ili kuwajenga kimaadili.
Amesema madrasa zina mchango wa
kipekee katika kuwaandaa watoto na kuwakuza kuwa raia wema
walioleleka katika maadili ya Kiislamu, na kwamba waislamu bado wana
jukumu la kuzianzisha madrasa kwa wingi na kuhakikisha kuwa watoto
wanapita katika darsa hizo kupata malezi sahihi.
Amefahamisha kuwa hivi sasa Zanzibar
inahitaji malezi mazuri kwa watoto na vijana kuliko wakati mwengine
wowote, kutokana na matishio makubwa yanayojitokeza na kuvurugika
kwa maadili mema.
Amewakumbusha waislamu kuchangia
harakati za dini hiyo kwa kujenga na kuimarisha misikiti na madrasa,
kwani kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wake katika kuziendeleza
nyumba hizo za Mwenyezi Mungu.
Aidha Maalim Seif amewakumbusha
waislamu kuendeleza umoja, maelewano, na mshikamano miongoni mwao, na
kujiepusha na chuki miongoni mwa waumini wa dini hiyo na dini
nyengine.
Amesema serikali imefanya juhudi
kubwa kuiwezesha jamii kuondokana na hasama, chuki na kudharauliana
na badala yake kujenga mazingira ya umoja, mshikamano na maelewano,
mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono kwa vitendo.
Katika hatua nyengine Maalim Seif
ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa waangalifu katika kuwachagulia
vyuo vijana wao, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa ni
pamoja na kuporomoka kwa maadili .
Amesema baadhi ya vyuo hasa
vilivyoko nje ya nchi havina misingi mizuri ya malezi, na kwamba bila
ya kuwa waangalifu jamii inaweza kupoteza wengi ambao hatimaye
wanaweza kujitumbukiza katika vitendo viovu.
“Chagueni vyuo vitakavyo
wanufaisha vijana, sio kijana kwa sababu anakwenda kusoma nje ya nchi
umkubalie tu, wazazi na walezi ni lazima mufuatilie kujua uhakika wa
vyuo hivyo” alisisitiza.
Akizungumza kabla ya hotuba ya
Ijumaa, Sheikh Thabit Noman Jombo kutoka ofisi ya Mufti wa Zanzibar
amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuutumia msikiti huo kama sehemu ya
kutolea taaluma.
Amesema Zanzibar ilikuwa kitovu cha
elimu katika nchi za Afrika Mashariki, na hakuna budi kuienzi
historia hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mapema akisoma risala ya wazee wa
msikiti huo Sheikh Abdalla Rajab, amewashukuru waliojenga msikiti huo
mkubwa katika kijiji chao, na kuahidi kuutunza na kuweka darsa ambazo
zitakuwa endelevu.
Amesema uwepo wa msikiti huo ni
faraja kwa wanakijiji na maeneo jirani, kwani pia wameweza kuondokana
na shida ya maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa kipindi
kirefu.



Hakuna maoni :
Chapisha Maoni