.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 7 Mei 2015

MAALIM SEIF AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI BIBI HAWA NDILOWE NA BALOZI MTEULE WA TANZANIA NCHINI JAPAN BIBI BATILDA BURIANI

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan bibi Batilda Buriani ofisini kwake Migombani.


                                                                                      Na: Hassan Hamad (OMKR).
 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea haja ya kuimarishwa kwa biashara na uwekezaji wa kikanda, ili kutoa fursa kwa wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kukuza biashara na maendeleo yao.
 

Amesema wafanyabiashara wengi wa ukanda huu wa Afrika Mashariki wamekuwa wakifanya biashara kati ya nchi moja na nyengine, na kutaka utaratibu huo uendelezwe kwa kuwekewa mikakati imara, ili kurahisisha biashara hizo.
 

Maalim Seif ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na balozi wa Malawi nchini Tanzania bibi Hawa Ndilowe na balozi mteule wa Tanzania nchini Japan bibi Batilda Buriani ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa balozi nchini Kenya.
 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema iwapo shughuli za kibiashara na uwekezaji zitawekewa mipango na mikakati endelevu, nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo kutokana rasilimali nyingi zilizopo.
 

Akizungumza na balozi wa Malawi nchini Tanzania, Maalim Seif amesema nchi hizo zinaweza kushirikiana katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo kilimo, elimu na utalii, ambazo zinaonekana kuleta mafanikio makubwa.
 

Amesema Zanzibar tayari inazo hoteli za nyota tano, hivyo watalii kutoka maeneo mbali mbali duniani pamoja na wawekezaji wakiwemo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, wanaweza kuzitumia kuendeleza biashara zao.
 

Akizungumzia kuhusu Japan, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema nchi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar, na kutaka uhusiano uliopo kati yake ya Tanzania uendelezwe.
 

Amemueleza balozi huyo mteule wa Tanzania nchi Japan kuwa nchi hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hasa katika miradi mikubwa ya maji na kilimo, sekta ambazo zimekuwa zikisaidia kupunguza kero za wananchi.
 

Amemshauri balozi Batilda kuitangaza vyema Tanzania kwa wawekezaji na watalii wa Japan, ili waweze kuzijua fursa zilizopo nchini na kuweza kuja kwa wingi kuwekeza vitega uchumi vyao.
 

Aidha Maalim Seif amesema Zanzibar bado inahitaji vyanzo mbadala vya nishati ya umeme, ambapo mchango mkubwa wa kitaalamu unahitaji kuweza kupata umeme utokanao na upepo kwa kisiwa cha Unguja na ule utokanao na maji ya bahari kwa upande wa Pemba.
 

Kwa upande wake, balozi wa Malawi nchini Tanzania bibi Hawa Ndilowe, amesifu mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya nchi yake na Tanzania, na kwamba yamekuwa yakileta mafanikio makubwa kwa wananchi wa pande hizo mbili.
 

Amesema vijana kadhaa wa Malawi wamekuwa wakijiunga na vyuo vikuu pamoja na kufanya biashara zao nchini Tanzania, na kuomba ushirikiano huo uimarishwe.
 

Naye balozi Batilda Buriani ambaye mbali ya Japan pia ataiwakilisha Tanzania katika nchi za New Zealand, Australia na Korea ya Kusini, amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa ataiendeleza vyema kazi iliyoachwa na mtangulizi wake katika nchi hizo, ikiwa ni pamoja na kuzitangaza fursa za utalii na uwekezaji nchini Tanzania. 

Balozi Batilda ambaye alikuja kwa ajili ya kujitambulisha, amesema kazi aliyoifanya nchi Kenya ya kukuza ushirikiano na kuhamasisha fursa za ajira kwa vijana wa Tanzania, ataiendeleza nchini Japan ili kusaidia kukabiliana na tatizo la ajira nchini.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni