.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 24 Mei 2015

TAASISI ZA DINI ZANZIBAR ZAASWA KUTOEGEMEWA UPANDE WA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA

Mratibu wa GNRC Zanzibar Dk.Mohammed Hafidh akifunga semina hiyo na kutoa nasaha zake kwa wajumbe wa semina hiyo
Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwakilishwa kwenye Ofisi ya Jengo la Bima Mperani Mjini Unguja.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mwenyekiti wa Semina ya kuhamasisha viongozi wa Dini ya Kiislamu katika kusimamia Amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 Sheikh Khamis Abdulhamid akiongoza washiriki wa semina hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Zanzibar Dr. Muhyiddin Ahmad Khamis akiwasilisha mada juu ya Nafasi ya Uislamu katika kujenga na kudumisha amani katika Jamii kwenye semina ya kuhamasisha amani wakati wa uchaguzi mkuu.
Imamu wa msikiti Mkuu wa Msumbiji Sheikh Othman Khamis Ali akichangia katika mkutano huo.
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdulla Talib Abdulla akiwasilisha mada juu ya Nafasi ya Taasisi za kidini katika kufanikisha uchaguzi wa Amani na uadilifu 2015.

Na Ramadhani Ali
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdulla Talib Abdulla amesema Taasisi za dini hazipaswi kuegemea upande wa chama chochote cha siasa ama kushiriki katika kampeni za uchaguzi lakini zinawajibu wa kujenga jamii ishiriki kikamilifu kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kujenga matumaini makubwa ya kuwa na amani.

Sheikh Abdulla Talib ameeleza hayo alipokuwa akiwasilisha mada ya nafasi ya Taasisi za kidini katika kufanikisha uchaguzi wa amani na uadilifu katika Semina ya kuhamaisha Viongozi wa dini ya Kiislamu kusimamia amani wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Amesema dini inamisingi muhimu inayoweza kutumika katika kujenga amani kwani kuna uhusiano mkubwa wa kinadharia baina ya dini na uchaguzi wa amani na uadilifu.

Ameongeza kuwa kufanya kazi ya kujenga amani ni kutekeleza dhamana ya dini kwani uislamu wakati wote unasisitiza umoja, upendo na amani ya kila mtu.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana amewaeleza washiriki wa semina hiyo ambao ni masheikh na wanazuoni kutoka mikoa mitatu ya Unguja kwamba wanadhima ya kusisitiza kufuatwa sheria na uadilifu kuanzia sasa mpaka kutangazwa matokeo ya uchaguzi.

“Uchaguzi wa amani unahitaji kuwepo uadilifu, kufuatwa taratibu na miongozo katika mchakato wote, ushirikishwaji wa pande zinazohusika kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, kutolewa elimu ya kutosha ya uraia, uwazi na uwajibikaji pamoja na kuyakubali matokeo,”alieleza Sheikh Abdulla Talib.

Katika kufanikisha uchaguzi huru na haki Sheikh Talib ameshauri kuwa na matumizi mazuri ya nyumba za Ibada na maeneo ya kidini pamoja na matumizi mazuri ya aya, hadithi, nukuu za kihistoria na hekma nyengine.

“Kwa kuzingatia uhalisia wa uchaguzi, taasisi za kidini zinapaswa kutumia mbinu na taratibu za kidini na nyenginezo katika kulingania uchaguzi wa amani, ”aliongeza sheikh Abdulla Talib.

Aliwakumbusha wanazuoni hao kuwa Zanzibar ni nchi ndogo yenye watu wachache wenye uhusiano wa karibu na tatizo linapotokea huzigusa familia nyingi hivyo amewashauri mahubiri yao yalenge kufanyika uchaguzi katika misingi ya uhuru, uwazi, haki, amani na utulivu.

Washiriki wa semina hiyo wameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa waadilifu na kufuata taratibu na sheria zote za uchaguzi kuanzia hatua za kuliboresha daftari la wapiga kura hadi kukamilika zoezi la uchaguzi bila ya kuingiza ushabiki wa kisiasa.

Katika maazimio yao masheikh hao wametaka kuhakikishiwa usalama wao wakati wa kutekeleza jukumu la kuwahubiria wafuasi wao kwani wameingiwa na wasi wasi wa kukamatwa kutokana na visingizio mbali mbali.

Semina hiyo iliyofanyika katika jengo la Ofisi ya Bima Mperani, iliandaliwa na Jumuiya ya JUMAZA na UKUEM kwa kushirikiana na mtandao wa kimataifa wa dini kwa ajili ya kulinda watoto (GNRC)

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni