WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la ugonjwa wa malaria kwa kuamua kujenga kiwanda cha kisasa cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha malaria.
Kiwanda hicho cha viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kimejengwa eneo la TAMCO, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua kiwanda hicho jana jioni (Ijumaa, Mei 8, 2015), Waziri Mkuu alisema ana imani kujengwa kwa kiwanda hicho kutamaliza tatizo la malaria hapa nchini na katika nchi za jirani.
“Malaria ni ugonjwa hatari na unaongoza kwa kusababisha vifo hapa nchini. Watu karibu milioni mbili wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa huu. Tukianza kutengeneza hizi dawa zitasaidia sana kupunguza tatizo hili na kuokoa maisha ya watoto na wanawake wajawazito ambao ndiyo waathirika wakubwa,” alisema.
Akielezea utendaji kazi wa dawa hizo, Waziri Mkuu alisema: “Dawa hizi zinapotumiwa kwenye madimbwi, viluwiluwi ni lazima watakufa katika muda wa saa 24… na mle kwenye dimbwi dawa ile inabakia ikifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja. Hii ina maana wakizaliwa viluwiluwi wengine pia wanakufa bila hata kuweka dawa nyingine,” alisema.
Kiwanda hicho ambacho kitatoa ajira za moja kwa moja 186, kinatarajiwa kuzinduliwa Juni 25, mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete. Kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa majaribio mapema mwezi ujao.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na viongozi wa Mkoa wa Pwani waliofika kushiriki ukaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bw. Evarist Ndikilo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania kujenga viwanda vingi zaidi katika Mkoa huo.
Akitoa maelezo kuhusu utengenezaji wa dawa hizo wakati Waziri Mkuu akikagua kiwanda hicho, Msimamizi Mkuu wa ujenzi, Dk. Ricardo Campos Menendez alisema ujenzi wa kiwanda hicho hapa nchini utatoa fursa kwa Tanzania kuuza dawa hizo kwa nchi jirani za Kenya, Congo – DRC ambazo pia zinasumbuliwa na tatizo la malaria.
“Tukishazaliza dawa za kutosha na kuzisambaza kwenye mikao yote, itabidi tuangalie uzalishaji wa kibishara kwa ajili ya nchi jirani zenye tatizo kama hili… hiki ni kiwanda pekee barani Afrika,” alisema.
Alisema pia kwamba kiwanda kitafanya kazi kwa karibu na vyuo vikuu kufanya tafiti na kutoa fursa za kutengeneza dawa za aina mbalimbali kulingana na mahitaji yaliyopo.
Kiwanda hicho kinachojengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya LABIOFAM SA ya Cuba, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za dawa ya Biolarvicides kwa mwaka.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni