Mnara wa kumbu kumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 unaoendelea kujengwa katika bustani ya Majengo la Maendeleo Michenzani unatarajiwa kukamilika ujenzi wake rasmi kati ya mwishoni mwa mwezi huu wa sita au mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu.
Ujenzi wa mrana huo ulioanza katika shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi mwezi Januari mwaka 2014 una urefu wa Mita 35.5 zitakazowawezesha watu watakaobahatika kupanda juu ya mnara huo kuona mandhari ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa Mnara ambayo yako katika hatua za mwisho kukamilika kwake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Abdulwakil Haji Hafidh alimueleza Balozi Seif kwamba Mnara huo umejigawa katika sehemu tatu zitakazojitegemea.
Nd. Hafidh alisema sehemu ya chini itakuwa Maktaba maalum ya vielelezo vya kumbu kumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar itakayotowa fursa kwa wananchi kujifunza mambo mbali mbali ya Historia ya Mapinduzi hayo.
Alisema sehemu ya kati itatengwa maalum kwa huduma za vyakula na vinywaji wakati ile sehemu ya tatu itakuwa maalum kwa watakaopanda juu kuangalia mji wa Zanzibar kwa kutumia camera maalum sambamba na Mkahawa wa Michezo { Sports Restaurent } utakaotoa nafasi kwa vijana kujifunza mambo ya historia za wanamichezo maarufu Duniani.
Mkurugenzi Mtendaji Hafidh alimueleza Balozi Seif kwamba eneo la bustani linakalouzunguuka mnara huo wa Michenzani litakuwa na maeneo yaliyotengwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo watakaoandaliwa utaratibu maalum wa kuendesha biashara zao.
Ndugu Abdulhakim Haji Hafidh alieleza kwamba ujenzi wa Mnara huo unaotarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 5 ambapo hadi sasa matengenezo ya mnara huo yameshagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 3.8.
Naye Mshauri Muelekezi wa Mradi wa Ujenzi wa Mnara wa Kumbu kumbu ya Mapinduzi Bwana Habib Nour alimfahamisha Balozi Sei kwamba sehemu ya juu ya mnara huo imetengenezwa kitaalamu itakayowawezesha wananchi kupata huduma za vinywaji huku ikiwa inazunguuka ili kuwapa raha na burdani wananchi hao.
Bwana Habib Nour alisema mradi wa Ujenzi huo unaotarajiwa kuzunguukwa na Bara bara ukijumuisha Camera maalum za CCTV kwa ulinzi na usalama wa eneo hilo umefikia asilimia 95% ya ujenzi wake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar





Hakuna maoni :
Chapisha Maoni