Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
SIKU moja baada ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kumlipua
mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama kwa madai ya kufanya udalali na ufisadi
katika uporaji wa ardhi ya wananchi ,mkuu huyo amejitokeza mbele ya wanahabari
na kukanusha tuhuma hizo.
Katika utetezi wake Gama alirejea kauli yake aliyoitoa miaka
sita iliyopita ya kuwa yeye ni msafi huku akiitupia mzigo halmashauri ya wilaya
ya Rombo tuhuma za kiasi cha sh Mil 500 zilizotajwa kutolewa wawekezaji wa Kichina
kama fidia kwa wananchi katika ardhi kilipojengwa kiwanda cha kutengeneza
Saruji.
Alisema tuhuma zilizotolewa Bungeni dhidi yake si za kweli
na kwamba ni za kisiasa huku akitaja sababu ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo kuwa
ni kutokana na juhudi zake za kupambana na Pombe haramu katika wilaya ya Rombo pamoja
na Urejeshwaji wa wafanyabiashara katika soko la kati la mjini Moshi.
“Nataka niwaambie hii ni siasa,zipo issue nyingi zilizochangia
kuibuka kwa haya mambo ,lakini nawaambieni mbili tu,Issue ya kwanza Pombe Rombo,na
msimamo wangu juu ya Pombe Rombo ndio imeza hii,la pili ni soko la Moshi mjini,watu
wana agenda zao kwenye soko hilo wananchi wamerudi pale ,imewaumiza
watu.”alisema Gama.
“Watu walitaka Pombe ya Gongo ihalalishwe,mimi nimesema
hadharani anayetaka pombe ya Gongo ihararishwe si mwenzetu mu mshughulikie kwa maana
si mwenzetu sasa hili limeleta nongwa”aliongeza Gama.
Akitoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo ,Gama amekiri mtoto wake
aliyetajwa kwa jina la Mayunga Leonidas Gama kuhusika katika uanzishaji wa
kiwanda hicho huku akihakikisha kiwanda hicho kinajengwa katika mkoa wa
Kilimanjaro badala ya Bagamoyo kama walivyo pendelea wawekezaji hao.
“Kiwanda cha saruji kinachojengwa pale Rombo, nilikuwa na
uwezo wa kukipeleka popote ninapotaka mimi, lakini mimi binafsi ndiye niliyefanya
juhudi kiwanda kile kijengwe Kilimanjaro, mimi binafsi na wala sio mtu
mwengine, nimefanya juhudi hizo kwa lengo la kuongeza ajira kwa wananchi na
kuinua uchumi wa mkoa huu”, alisema Gama .
“Historia ya Kiwanda hiki iko wazi, nililipeleka hadi kwenye
kikao cha ushauri wa mkoa (RCC),nanaomba nieleweke kwamba, ni juhudi zangu na
za mtoto wangu, nilitamka kwenye kikao kile na wala sikuficha, mtoto wangu
ambaye ametajwa yeye ana rafiki yake wa kichina, wala si kweli kwamba hii kampuni
mimi nimekwenda kuichukua China kwa gharama za serikali” aliongeza Gama.
Alisema katika kikao hicho (RCC), Mbunge wa Rombo, Joseph
Selasini, Mbunge wa Vunjo, Dkt. Augustino Mrema na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo, walishiriki katika kikao hicho na kwamba baada ya mvutano ndipo
makubaliano yakawa kiwanda kijengwe wilaya ya Rombo.
“Toka siku ile mimi kama mkuu wa mkoa nikakabidhi madaraka
wilaya ya Rombo,kwa hiyo shughuli zote za ujenzi ,shughli zote za kutafuta viwanja
ziifanywa na halmashauri ya wilaya ya Rombo na sio Gama”alisema Gama.
Alisema waliolipa fidia na kununua viwanja ni halmashauri ya
wilaya na hata eneo kilipojengwa kiwanda hicho ni mali ya halmashauri ya wilaya
ya Rombo na si cha mwekezaji kama inavyoelezwa .
“Nimeelezwa kweye tuhuma kuwa
nimepewa milioni 500,hii ni hadithi ya kisiasa ,sijapokea kiasi hicho cha fedha
wala sikijui,hata hizo hisa 20,000 nilizoambiwa ninazo kwa kweli sina ,kama
ningekuwa nazo ni Haki yangu kwa sabau sijavunja sharia lakini sina hata hisa
moja.”alisema Gama.
“Swala mtoto wangu kuwa na hisa si dhambi na ni haki yake
kisheria,kwa sababu yeye ndiye aliyewatafuta hao watu na ni rafiki zake ,wala
si mimi niliyewaleta kama amenunua hisa huko ni hiari yake,mimi sina hisa kama
Gama,sijapokea milioni 500 kama gama,mimi si dalali na kama ni udalali wa ardhi
hiyo itakuwa ni halmashauri ya wilaya ya Rombo na si gama.”alisema Gama.
Alipoulizwa endapo kama halmashauri ya wilaya ya Rombo
itakuwa inamiliki sehemu ya hisa katika kampuni hiyo kutokana na utolewaji wa ardhi
yake ,Gama alisema wenye majibu ni halmashauri ndio watakuwa wanajua ni mikataba
gani wameingia na wawekezaji hao.
Kuhusu eneo la Uwekezaji wa soko la Lokolova, Gama alisema ameshangazwa
na kauli za kuwa yeye ni fisadi wa ardhi katika eneo hilo wakati makubaliano ya
kuanzishwa kwa soko la kimataifa na mji mdogo wa kibiashara ulipitishwa katika
kikao cha RCC ambacho pia Mbunge wa Vunjo, Dkt. Augustino Mrema alihudhuria na
kusifia mpango huo.
Sakata la Kiwanja cha Mawenzi, Gama alisema yeye kama mkuu
wa Mkoa, alichokifaya ni kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kufuata Sheria
za umilikishwaji wa Ardhi ili kuepusha Halmashauri kufilisiwa kwa kukiuka taratibu.
Juzi wakati akiwasilisha bungeni maoni ya kambi rasmi ya
upinzani kuhusu bajeti ya wizara ya ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi kwa mwaka
wa fedha 2015/2016,msemaji mkuu wa kambi hiyo Halima Mdee alimrushia tuhuma
Gama za kuhusika katika kutumia fedha za serikali kwenda nchini China kutafuta
watu wawili wanaotajwa kama wawekezaji.
Katika taarifa hiyo Mdee alidai katika hali isiyo ya kawaida
naya kushangaza watu hao katika ardhi iliyokwisa lipiwa fidia kwa fedha za umma
,ilianzishwa kampuni binafsi ya Jun Tu Investment International Company Ltd .Mwisho.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni