Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (kushoto) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) wakipitia baadhi ya kurasa za mwongo wa kufundishia kitabu cha Uraia wakati wa ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na TASAF wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (kushoto) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (katikati) huku Afisa Program Kitengo cha Uahulishaji Fedha (TASAF), Edith Mackenzie (kulia) akiwapitisha kwenye baadhi ya maeneo katika mwongozo wa kitabu cha kufundishia somo la Urai walipofanya ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na TASAF, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis (katikati) na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez (kushoto) wakiangalia zao la mboga ya Kisamvu walipotembelea shamba la Bi. Twajuana Mohamed (kulia) anayenufaika na mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mpango Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) ambapo ameweza kufuga Kuku wa kienyeji, kujenga choo cha kisasa, Kilimo pamoja na kukunua mabati ya kuezekea nyumba yake kupitia mradi huo wakati wa ziara ya siku moja katika kijiji cha Chasimba, kata ya Yombo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Bi. Twajuana Mohamed (kushoto) akiwa ameongozana na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga kukagua shamba la Bi. Mohamed ambaye amenufaika na mradi wa TASAF katika kujikwamua kiuchumi. Wa pili kulia ni Afisa Program Kitengo cha Uahulishaji Fedha (TASAF), Edith Mackenzie.
Balozi wa Spain nchini, Mh. Luis Cuesta Civis na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga kwenye picha ya pamoja na familia ya Bi. Twajuana Mohamed ambaye ananufaika na mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mpango Kunusuru Kaya Maskini (PSSN) sambamba na wajukuu zake.
Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
MRATIBU Mkazi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) nchini Tanzania Alvaro Rodriguez ametaka serikali za tawala za
mikoa na serikali za mitaa kuwezeshwa zaidi ili kuweza kuwatumikia
wananchi.
Aliyasema hayo wakati alipozuru
kijiji cha Chasimba mwishoni mwa juma akiwa na Balozi wa Hispania
Luis Cuesta Civis kuona miradi ya maendeleo inayofadhiliwa kwa pamoja
kati ya serikali ya Tanzania, Mashirika ya Umoja wa Mataifa na
Ubalozi wa Hispania.
Mratibu huyo alisema kwamba
mafanikio makubwa yanayoonekana katika kijiji cha Chasimba ni matokeo
ya ushirikiano mzuri wa wadau wa maendeleo na wanakijiji.
Alisema ushirikiano huo ni muhimu
katika kutokomeza umaskini uliokithiri katika jamii.
Alisema pamoja na mafanikio hayo
Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo wangelipenda kuona
serikali za mitaa zinawezeshwa zaidi ili kuweza kusaidia jamii kama
inavyofanyika sasa katika kijiji cha Chasimba.
Kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji
kadhaa nchini vinavyofaidika na mpango unaotekelezwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii, TASAF, ambao nao unachangiwa na mashirika ya
Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa maendeleo.
Alisema anapenda kuona kwamba maisha
ya wakazi wa kijiji hicho yanabadilika na kuwa kama ya mama Kicheko
ambaye ameondoka katika umaskini uliokithiri baada ya kutumia vyema
mradi uliofikishwa kijijini hapo.
Alitoa wito kwa wadau wa maendeleo
na mashirika ya kimataifa kusaidia kuwezesha serikali za mitaa na
mashirika yanayoapambana na umaskini nchini kuwezesha miradi ya
kuondoa umaskini kufanikiwa.
Bi. Kicheko ambaye mwaka mmoja
uliopita alikuwa hohehahe kwa sasa anatengeneza sabuni, ameboresha
nyumba yake kwa kuiwekea bati na ana kula mlo zaidi ya mmoja sasa.
Katika ziara hiyo, Mratibu huyo
alitaka kujua wananchi wa Chasimba katika miaka mitano hadi saba
ijayo wanataka kuwaje na kujibiwa kwamba wanataka kuwa na hali bora
zaidi ilivyo sasa na kuanzisha viwanda vidogo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF), Ladislaus Mwamanga, alisema mpango huo wa
miaka 10 ambao umeingia katika mwaka wa tatu umelenga kuwezesha afya,
elimu na lishe na sasa wanafanya kuwajengea uwezo wa kuweka akiba na
kuwekeza.
Alisema uwekaji akiba huo
unawezekana kwa kutoa ajira wakati wa vipindi vigumu.
Alisema mpango huo wa kukabili
umaskini uliokithiri unachangiwa pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la
Maendeleo la Uingereza, Shirika la maendeleo la Sweden na serikali ya
Tanzania.
Alisema kuna kaya milioni moja
zinazokula mlo mmoja ambazo zinatakiwa kubadilishwa kuwa katika hali
bora.
Aidha alisema wameshakamilisha
kutengeneza ramani ya umaskini baada ya kumaliza kuandikisha kaya
maskini zilizopo nchini.
Diwani wa kata ya Yombo ambapo
kijiji cha Chasimba aliyejitambulisha kwa jina la Idd alisema kwamba
ni matraajio yao katika miaka 10 ijayo kubadilika kabisa kutokana na
kijiji hicho kuwa na umeme na maji ya kutumia.
Alisema hata hivyo wanahitaji
msukumo zaidi ili kuwa na viwanda vidogo.
Naye balozi wa Hispania nchini, Luis
Cuesta Civis alisema kwamba amefurahishwa na matokeo ya fedha ambazo
nchi yake imezitoa zipatazo bilioni 1.3 za maendeleo ambazo nyingine
zimepelekwa TASAF.
Kijiji cha Chasimba kina kaya 197
zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III (PSSN)
ambapo tayari wamepewa ruzuku ya shilingi 43,227,190 katika mikupuo
9.
Imeelezwa kuwa kumekuwepo na
mafanikio makubwa tangu kuanza kwa mradi wa PSSN kijijini hapo.
Mafanikio hayo ni pamoja na kumekuwepo na ongezeko la wanafunzi
wanaoandikishwa na kuhudhuria shule, aidha madarasa matatu yamejengwa
na ofisi ya mwalimu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni