.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 8 Julai 2015

BALOZI SEIF AFUTARI PAMOJA NA WATOTO YATIMA WA KITUO CHA RAHMAN MJINI DODOMA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza
umuhimu wa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kujenga utamaduni wa
kufutari pamoja ili kudumisha utaratibu uliotiliwa nguvu na Kiongozi
wa Dini hiyo Mtume Muhammad { SAW } na kuendelezwa na maswahaba
waliomfuata.
 
Balozi Seif ametoa sisitizo hilo kwenye hafla ya Futari ya pamoja
aliyowaandalia Watoto Yatima wanaolelewa katika Kituo cha malezi ya
Watoto yatima cha Kiislamu cha Rahman Kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma.
 
Futari hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Dini ya
Kiislamu wa Mji wa Dodoma wakiambatana na baadhi ya Viongozi wa
Serikali na Kisiasa ilifanyika katika Makazi yake yaliyopo Mtaa wa
Farahani Mjini Dodoma.
 
Balozi Seif alisema mijumuiko hiyo ya waislamu mara kadhaa husaidia
kuongeza upendo, ushirikiano na mahaba baina yao jambo ambalo huongeza
nguvu za pamoja katika jitihada zao za kusimamisha Dini ya Mwenyezi
Muungu.
 
Akiwapatia  sadaka katika kujiandaa  kusherehekea siku kuu ya Iddi El
- Fitri wanafunzi hao wa Chuo cha Malezi ya Kiislamu ya watoto Yatima
cha Rahman Balozi Seif aliwaombea kusherehekea siku kuu hiyo kwa
amani,salama na upendo.
 
Akitoa shukrani kwa niaba ya waalikwa wa futari hiyo Sheikh Shaaban
Kitila wa Masjid Nunge alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif kwa ukarimu wake wa kuwakusanya wauminbi wenzake kwenye
futari ya pamoja.
 
Sheikh Kitile alisema kufutarisha ni jambo la sunna lililosisitizwa na
Mtume Muhammad { SAW } linalotoa nafasi kwa waumini wa dini ya
Kiislamu wasio na uwezo kupata futari inayoleta faraja kwao.
 
Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Rahman kinachosimamiwa na
Ustaadhat Rukia Khamis { Maarufu Mama Abdullah } kimeanzishwa mwaka
2007 kikiwa na wanafunzi 20 ambapo hivi sasa kinahudumia watoto yatima
wapatao 70.
 
Balozi Seif amejiwekea utaratibu wa kufutari pamoja na Watoto hao wa
Kituo cha kulelea Watoto yatima Mjini Dodoma napokuwa katika shughuli
zake za kikazi akiwa Mjini Humo ndani ya Mfungo wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
 
Wakati Kumi la Pili ya Maghfira likimalizika na kuingia kumi la Mwisho
la Kuachwa huru na Moto ndani ya Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Radhani
waumini wa Dini ya Kiislamu wamekuwa wakiendelea kujumuika katika
futari ya pamoja katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni