Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha na – OMPR – ZNZ.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ahadi alizotoa kwa Wananchi wa Jimbo hilo wakati akiwatumikia ndani ya Kipindi cha Miaka 10 iliyopita atahakikisha kwamba anazikamilisha kabla ya kuanza kwa kipindi chengine cha Uongozi baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema yeye bado anaendelea kuwa Kiongozi wa Jimbo hilo kwa vile jukumu la kuwatumikia Wananchi wa Maeneo hayo uko mikononi mwake na wala hafanyi kampeni kwa mujibu wa kanuni kwa vile muda wa kufanya hivyo haujafika licha ya kwamba unakaribia.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kiomba Mvua katika hafla fupi ya kukabidhi mchango wa shilingi Milioni 5,000,000/- kwa Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } zitakazotumika katika ujenzi wa Kibanda kwenye Kisima Kilichochimbwa na Mamlaka hiyo kitakachosambaza maji katika kijiji hicho na vile vya jirani.
Alisema Wananchi wa Kijiji cha Kiomba Mvua wamekuwa wakikabilia na tatizo la huduma za maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambapo yeye kama kiongozi aliwaahidi kufanya juhudi kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kutatua changamoto hiyo ya muda mrefu.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na Serikali ya Ras AL-Khaimah wa kusaidia ujenzi wa visima katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba msaada utakaowakomboa Wananchi walio wengi hasa akina Mama.
Hata hivyo alieleza na kufafanua kwamba Visima vinavyofadhiliwa na Serikali ya Ras Al – Khaimah lazima Viongozi wa Majimbo wachangie ili kuunga mkono miradi hiyo iende kwa haraka.
Balozi Seif aliahidi pia kuchangia Mabomba ya Kusambazia Maji kutoka kwenye Kisima hicho na kuwaomba Wananchi hao kujitokeza kwa wingi wakati wa uchimbaji wa Mitaro ya kulaza Mabomba hayo.
Akipokea mchango huo wa shilingi Milioni 5,000,000/- Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu alisema Mamlaka hiyo inaendeleza jitihada za kuimarisha miundo mbinu ya sekta ya Maji ili kuwaondoshea usumbufu unaowapata Wananchi katika baadhi ya maeneo hapa Nchini.
Dr. Garu aliwahakikishia Wananchi hao wa Kijiji cha Kiomba Mvua kwamba Kisima hicho kina maji ya kutosha na ujenzi wa miundo mbinu iliyobakia kwenye kisima hicho itamalikia kwa haraka kama ilivyopangwa ilikuwapa faraja Wananchi hao ya kupata huduma ya maji safi badala ya kutumia yale yasiyo salama kwa afya zao.
Mapema Sheha wa Shehia ya Kiomba Mvua Bwana Mzee Ramadhan Mzee aliwanasihi na kuwatahadharisha Wananchi hao kujiepusha na tabia ya uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo la Kisima ili huduma ya maji itakayotoka eneo hilo iendelee kuwa salama.
Wakati huo huo Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi mchango wa Shilingi Milioni 5,000,000/- akitekeleza ahadi aliyotoa ya kusaidia kuifanyia matengenezo makubwa Ofisi ya Tawi la Chama cha Mapinduzi ya Kinduni.
Matengenezo ya Ofisi hiyo yamekisiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 8600,000/- ambazo Balozi Seif aliahidi kutoa kwa awamu kadri hali itakavyomruhu kufanya hivyo.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi Balozi Seif aliwakumbusha Viongozi pamoja na Wanachama wa CCM wa Tawi hilo kuwachagua Viongozi makini watakaokubali kushirikiana na Wananchi katika harakati za maendeleo yao.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba kipindi cha miaka Mitano ni kikubwa mno endapo Wananchi hao watafanya makosa kwa kumchagua Kiongozi maslahi na kusubiri aondoke madarakani muda ambao utakuwa umeviza maendeleo yao.
Akipokea mchango huo kwa Niaba ya Wanachama hao wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Kinduni Katibu wa CCM wa Tawi hilo Nd. Shaaban Mohammed alimpongeza Balozi Seif kwa uungwana wake wa kutekeleza ahadi anazotoa katika kipindi kifupi.
Nd. Shaaban alisema jitihada za Balozi Seif ambazo ziko wazi na kushuhudiwa na Jamii katika maeneo mbali mbali Nchini zimekuwa zikileta faraja na nguvu kwa Wanachama pamoja na Wananchi Wazalendo.
Mapema Mke wa Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alisema jukumu la kuwachagua Viongozi bora wanaofaa kusimamia changamoto zinazowakabili Wananchi limo mikononi mwa Akina Mama.
Mama Asha alisema kwamba asilimia kubwa ya wapiga kura katika majimbo mbali mbali Nchini iko kwa akina Mama. Hivyo fursa hiyo kubwa waliyoipata akina mama hao wana wajibu wa kuitumia vyema.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni