Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeazimia kujenga skuli Kumi Mpya za Msingi katika kiwango cha Ghorofa kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo fedha kwa ajili ya kazi hiyo tayari zimeshatengwa.
Alisema kutokana na ongezeko la idadi ya watu hasa katika maeneo ya Mji hususan Wilaya ya Magharibi “A” na “B” Skuli za msingi zimekuwa na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi madarasani.
Dr. Shein alieleza hayo wakati akizungumza na wazazi, walimu, wanafunzi na wananchi wa Mtaa wa Tomondo ndani ya Jimbo la Dimani Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuweka Jiwe la msingi la Ujenzi wa Skuli Mpya inayojengwa katika eneo la Tomondo Wilaya ya Mgharibi “B “.
Alisema Serikali imekuwa ikichukuwa jitihada mbali mbali katika kuhakikisha kwamba Watoto wote wa Zanzibar waliofikia umri wa kwenda skuli wanaanza masomo ya msingi ili haki hiyo.
Dr. Shein alieleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa Nchi chache Duniani zilizofikia kiwango cha watoto wake wote waliofikia umri wa kwenda skuli hupata fursa hiyo kwa asilimia 100% hadi mwaka huu wa 2015 na kupindukia kiwango kilichowekwa na Umoja wa Mataifa na Maendeleo ya Milenia.
Rais wa Zanzibar alizishukuru jitihada zinazochukuliwa na Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini kwa kushirikiana na Viongozi wao katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza majengo ya Skuli na kuanzisha ujenzi wa skuli mpya.
Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuondoa tatizo la uhaba wa nafasi madarasani na kupunguza masafa kwa watoto wadogo kufuata masomo katika skuli za maeneo ya mbali.
Dr. Shein aliwahakikishia Wananchi kwamba Serikali inathamini jitihada hizo na itaendelea kuziunga mkono kwa vitendo ili lengo la kuwapatia haki yao ya Elimu Watoto liweze kufikiwa kwa shabaha ile ile ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Tarehe 12 Januari mwaka 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Katika kuimarisha sekta ya Elimu Nchini Rais wa Zanzibar alisema Serikali imeandaa Sera na kutekeleza mipango tofauti ili kuongeza fursa za Elimu kwa Vijana hapa Nchini.
Alisema hivi sasa Serikali inatekeleza Sera ya Elimu ya mwaka 2006 ambayo imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu iliyo bora kwa watu wote bila ya ubaguzi.
“ Hii ni dhamira ya kutoa elimu bila ya ubaguzi kwa Wananchi wote kama ilivyodhihirishwa kwa tamko la “Elimu Bure “ lililotolewa na marehemu Mzee Abeid Amani Karume Tarehe 23 Septemba , 1964 “. Alisema Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba Serikali imetafakari na kuzingatia changamoto iliyolazimika wazazi kuchangia baadhi ya gharama ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora.
Dr. Shein alifahamisha kwamba uamuzi wa Serikali kwa sasa ni kulibeba jukumu hilo kuanzia mwezi Julai mwaka huu wa 2015 ikiwa ni utekelezaji wa tamko alilolitoa katika kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Aliwakumbusha wazazi na walezi kufuatilia watoto wao kwa kushirikiana na walimu ili kuondokana na tatizo la utoro kwani bila ya jitihada za pamoja azma hiyo haitafikiwa.
Alisema jitihada za pamoja zina mchango muhimu kwa kuwa na kizazi bora kilichoelimika na chenye maadili mema yanayozingatia utamaduni wa malezi ya pamoja ambapo kuna haja ya kuyaendeleza ili kuinusuru jamii kutokana na changamoto zinazotokana na utandawazi.
Akisoma Risala ya walimu,wanafunzi na wazazi wa Tomondo Mwalimu Hadra Mkubwa Said alisema azma ya ujenzi wa skuli ya Tomondo imefikiwa baada ya Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Dimani kuamua ijenge skuli kwa lengo la kuwaondoshea usumbufu watoto wa maeneo ya Tomondo.
Mwalimu Hadra alisema kwamba vikao karibu 49 vilifanyika katika kuwashajiisha wananchi wa maeneo hayo kuunga mkono Kamati hiyo jambo ambalo lilipata vikwazo kwa uzito wa kuungwa mkono na baadhi ya wazazi wa eneo hilo.
Alifahamisha kwamba lengo la Kamati hiyo ni kuhakikisha kwamba Skuli hiyo inaendelea kukua hadi kufikia darasa na saba ikiwa na shabaha ya kuwa na majengo zaidi sambamba na maabara na huduma nyengine za skuli.
Akitoa taarifa ya Ujenzi wa skuli mpya ya Tomondo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ambae pia ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Dimani Mh. Abdulla Sharia Ameir alisema ujenzi wa skuli hiyo ni kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo la Dimani mwaka 2010.
Mh. Abdulla Sharia aliwahakikishia wananchi na wazazi wa Jimbo la Dimani kwamba madarasa mengine Matatu yataendelea kujengwa chini ya usimamizi wake licha ya kwamba atakuwa nje ya utumishi wa Jimbo hilo.
Mbunge huyo anayemaliza muda wake wa Jimbo la Dimani alikanusha uvumi uliotolewa na baadhi ya watu wa kumtuhumu kuiacha CCM na kujiunga na upinzani na kusema kwamba hizo zilikuwa njama za kutaka kumvunja moyo aache juhudi hizo za kuwaletea maendeleo Wananchi wa Jimbo hilo.
Aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuacha mlango wazi kwa kumpa ushirikiano katika azma yake ya kuendelea kutandika maendeleo ya Elimu ndani ya Jimbo hilo.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahara Hamad alisema ujenzi wa skuli hiyo umeleta Ukombozi mkubwa kwa watoto wa Mtaa wa Tomondo na maeneo jirani ambao walikuwa wakifuata elimu katika masafa marefu.
Mh. Zahra aliupongeza uongozi wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mbunge wa Jimbo la Dimani kwa ujasiri iliyochukuwa ya kuwaondoshea matatizo watoto wao.
Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itahakikisha kwamba ifikapo Mwezi Januari mwaka 2015 skuli hiyo inaaza kutoa huduma baada ya kupatiwa vikalio kwa kuchukuwa wanafunzi katika mfumo uliopo wa mikondo miwili.
Ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Tomondo wenye jengo lenye madarasa manne na Ofisi ya Mwalimu Mkuu ulioanza Tarehe 13/5/20p15 na kutarajiwa kukamilika Tarehe 20p/9/20p15 unakisiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 120,000,000/- hadi kukamilika kwake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni