
Wachezaji watano kutoka katika kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) wanaondoka leo jijini Dar es salaam kuelekea nchini Afrika Kusini katika klabu ya Orlando Pirates kwa ajili ya kufanya majaribio.
Vijana hao wanakwenda katika klabu ya vijana ya Orlando Pirates kufanya majaribo ambapo makocha wa vijana wa klabu hiyo watapata nafasi ya kuwatazama katika mazoezi na michezo ya kirafiki.
Nafasi hiyo imepatikana kufuatia mazungumzo ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Rais wa klabu hiyo Irvin Khoza kuomba vijana hao kupata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu hiyo na endapo watafuzu, watajiunga na timu ya vijana ya Orlando Pirates.
Msafara huo wa wachezaji utaongozwa na Mkurugenzi wa Ufudndi wa TFF, Salum Madadi ambaye atakua na vijana hao katika kipindi chote cha majaribio nchini Afrika Kusini.
Wachezaji hao ni Asaad Ali Juma (Zanzibar), Maziku Aman (Dodoma), Issa Abdi (Dodoma), Kelvin Deogratias (Geita) na Athumani Maulid (Kigoma).
Shirkisho la Mpira wa Miguu nchini linawatakiwa kila la kheri vijana hao katika majaribio yao huko nchini Afrika Kusini.

Timu ya taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15) leo inashuka dimbani kucheza na timu ya kombaini ya mkoa wa Morogoro (U15) katika mchezo wa kirafiki utakochezwa majira ya saa 10 jioni mjini Morogoro.
U-15 ambayo imeweka kambi ya takribani ya wiki moja mjini humo, imekuwa ikifanya mazoezi chini ya kocha wake Mkuu Bakari Shime ambaye amekuwa akiwaita vijana kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya mazoezi na kucheza michezo ya kirafiki.
Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya program ya timu ya vijana ya TFF, ambapo kocha anapata nafasi ya kuona maendeleo ya vijana wake baada ya kuwa wamefanya mazoezi na kuongeza vijana wengine katika kikosi hicho baada ya kuwa amerdhika na uweo wao katika michezo hiyo wanayocheza.
Timu hiyo ya U-15 inaandaliwa kwa ajili ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika nchini Madagascar mwaka 2017.
U-15 wanatarajiwa kucheza michezo miwili na kombaini ya mkoa wa Morogoro leo jumamosi na kesho jumapili, kabla ya kuvunja kambi na vijana kurejea makwao na kukutana tena mwishoni mwa mwezi Septemba kwa ziara ya mkoa mwingine.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetuma salam za rambi rambi kwa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa pwani (COREFA) kufuatia kifo cha mwamuzi mstaafu wa FIFA na kamishina wa TFF, Gilbert Mando kilichotokea jana mjini Bagamyoyo.
Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, TFF inawapa pole familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki na kusema wako pamoja katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo.
Marehemu Gilbert Mando alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya figo mpaka umauti ulipomfika jana jioni nyumbani kwake eneo la Bong’wa Bagamoyo, taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni