.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 1 Agosti 2015

TAASISI YA ECG TOKA MISRI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR KATIKA UCHUMI

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri Mhandisi Amri Alouba akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar michoro iliyotengenezwa na Wataalamu wa ECG ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kuwa katika mazingira ya Biashara ya Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wafanyabiashara pamoja na wataalamu wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri waliopo Tanzania kuangalia maeneo ambayo wanaweza kuwekeza miradi ya Kiuchumi.
Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed Alef Sherief wa kwanza kutoka kushoto akimfahamisha Balozi Seif hayupo pichani fursa zinazotolewa na Taasisi yake katika kuwajengea Vijana uwezo wa kufanya Biashara.
Balozi Seif katika Picha ya pamoja na Wafanyabiashara na wataalamu wa ushauri wa Uhandisi kutoka Nchini Misri mara baada ya kufanya mazungumzo nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri Mhandisi Amri Alouba na Balozi wa Tanzania Nchini Misri Balozi Mohammed Hamza.

Kulia ya Balozi Seif ni Mtaalamu wa Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji ya ECG Mhandisi Sherif Meurad pamoja na Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed Alef Sherief. Picha na – OMPR – ZNZ.

                                                                           Na Othman Khamis Ame, OMPR

Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri imeamua kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya kusaidia Uchumi wa Zanzibar na ustawi wa Wananchi wake.

Kiongozi wa Ujumbe wa Wafanyabiashara wa Misri wanaotembelea Tanzania kuangalia maeneo wanayoweza kushirikiana na Serikali katika uwekezaji Mhandisi Amr Allouba alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mhandisi Amri Allouba ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya uhandisi ya { ECG } alisema Wataalamu wa Taasisi hizo wako tayari kuelekeza nguvu zao ndani ya ukanda wa Afrika ya Mashariki, Zanzibar ikiwa miongoni mwake kutokana na mazingira mazuri ya rasilmali pamoja na uwekezaji.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Uhandisi ya ECG alisema Wataalamu wa Taasisi hiyo tayari wameshaandaa michoro ya jinsi linavyoweza kujengwa eneo la Darajani na kubadilishwa kuwa katika mazingira ya kisasa ya Biashara ya Kimataifa.

Mhandisi Amr alifahamisha kwamba eneo hilo la Darajani upande wa iliyokuwa kituo cha Dala dala pamoja na Makontena linaweza kujengwa Vituo vya Biashara bila ya kuathiri mipango Miji iliyowekwa katika Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika urithi wa Kimataifa.

Alieleza kwamba mradi huo endapo unaweza kukubalika na Serikali ujenzi wake unaweza kuchukuwa miezi 12 hadi 18 baada ya kukamilika kwa michoro husika itayozingatia taratibu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Sayansi, Elimu na Utamaduni { Unesco } linalohusika na hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni ya Kimataifa ya AIKAN ya Nchini Misri Bwana Mohammed Alef Sherief alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi yake imekuwa ikitoa mafunzo ya biashara ili kuwajengea uwezo vijana kujimudu kimaisha baaada kumaliza masomo yao.

Bwana Sherief alisema mpango huo unaohusisha wataalamu waliobobea katika fani ya Biashara huandaliwa katika mazingira bora yanayotoa ushawishi kwa vijana kupenda kujiunga badala ya kubakia kuzurura mitaani na hatimae kujiingiza katika vikundi viovu.

Akitoa Shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Ujumbe huo wa Wafanyabiashara na wahandisi kutoka Nchini Misri kwa uwamuzi wake wa kutaka kusaidia taaluma katika sekta ya uwekezaji vitega uchumi hapa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa imo katika mipango ya kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda, uvuvi, vituo vya biashara pamoja na maeneo mengine jambo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itazingatia Michoro iliyotayarishwa na Wataalamu hao katika azma ya kufanikisha mipango yake.

Taasisi ya Ushauri wa Uhandisi katika miundombinu ya ujenzi, usarifu wa Miji, Majengo ya Kisasa pamoja na Vituo vya Kimataifa vya Biashara { ECG } ya Nchini Misri tayari imeshajenga Vituo Sita vya Kimataifa vya Kiabiashara katika Nchi za Qatar, Kuweit, Sudan, Kenya, Tanzania Bara na wenyeji Misri.

Mhandisi Amr Allouba amekuwa mshauri muelekezi aliyesimamia kujengwa kwa Kijiji cha Kisasa cha Kibiashara cha Kimataifa kikiopo katika vitongoji vya Mtaa wa Kadizani ndani ya Mji wa Cairo Nchini Misri.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni