Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Mohamed Gharib Bilal amewaasa Watanzania hususan wakazi wa eneo la
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro kufanya jitihada za makusudi kutunza maeneo
yanayozunguka Mlima huo ili uendelee kuwa kivutio kikubwa cha utalii
nchini kwa ajili ya maendeleo yao na kwa Taifa kwa
ujumla.
Hayo
yamesemwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais-Mazingira, Mhe. Binilith Mahenge (Mb.) alipowasilisha hotuba wakati
wa tukio la upandaji miti ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka
70 ya
Umoja wa Mataifa lililofanyika leo katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro,
Kijiji cha Marua, Mkoani
Kilimanjaro.
Mhe.
Bilal alisema kuwa, Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi Afrika,
unaosimama peke yake na wenye barafu kwa mwaka mzima pamoja na kwamba
hali ya hewa ya Tanzania ni joto sana ni moja ya vivutio vikubwa vya
utalii ambavyo vinachangia kwenye pato la taifa na hata kipato cha
mwananchi mmoja mmoja kwa Kilimanjaro na maeneo yanayozunguka mkoa
huo.
“Nawaasa wazee wangu na wakazi wote wa Kilimanjaro kuwa na
jitihada za makusudi kutunza maeneo yanayozunguka mlima huu na
tusisubiri watu kutoka Dar es Salaam na maeneo mengine ya mbali kufanya
kazi hiyo”, ilisisitiza sehemu ya hotuba ya Dkt.
Bilal.
Akizungumzia matukio kuelekea maadhimisho ya miaka 70 ya
Umoja wa Mataifa ambayo yatafikia kilele tarehe 24 Oktoba mwaka huu,
Mhe. Bilal alipongeza na kuwashukuru waandaji wa shughuli hiyo
wakiongozwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Timu
ya Umoja wa Mataifa hapa nchini na TANAPA kwa kuwekea msisitizo umuhimu
wa kulinda na kutunza
mazingira.
Aliongeza kuwa japo hapo awali, Umoja wa Mataifa uliundwa kutokana na
vita na mapigano yaliyojitokeza duniani miaka ya nyuma anafarijika
kuona Umoja huo kwa sasa umebadilika na umekuwa ni chombo cha kupigania
na kutetea haki za binadamu na utunzajia wa mazingira.
“Nichukue fursa hii kupongeza Kaulimbiu ya Maadhimisho ya
miaka 70 ya Umoja wa Mataifa inayosema “Umoja wa Mataifa wenye Nguvu,
Dunia Bora” na ile kaulimbiu yetu ya hapa nchini inayosema:”Dunia Moja
Watu Bilioni Saba; Kutunza Mazingira ni Wajibu Wetu”. Hivyo ni wajibu wa
kila mmoja wetu kutunza mazingira ili kuhakikisha watu hao bilioni saba
hawaangamii,” alisema Mhe. Dkt.
Bilal.
Mhe.
Dkt. Bilal aliongeza kusema kuwa, wakati umoja wa Mataifa ukiadhimisha
miaka 70 mwaka huu, pia utakuwa na matukio mengine matatu makubwa ambayo
ni kuhitimisha utekelezajii wa Malengo ya Milenia, Kupitishwa kwa agenda
mpya ya Maendeleo Endelevu baada ya mwaka 2015 na kupitishwa kwa mkataba
mpya wa Mambadiliko ya Tabianchi utakaorithi Itifaki ya sasa ya
Kyoto.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Mhe. Leonidas Gama, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Mhe. Novatus
Makunga alisema kuwa Mkoa huo umejitahidi kuchukua hatua mbalimbali za
kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro
ikiwemo kusitisha vibali vya uvunaji wa miti ya mbao na kuni; kuhimiza
matumizi ya nishati mbabadala kwenye taasisi za shule, vyuo na magereza;
kuhamasisha wananchi kupanda miti kwenye vyanzo vya maji pamoja na
kuhifadhi misitu ya asili.”Tunapongeza Taasisi zote zilizoamua kuchagua
Mkoa wetu kwa maadhimisho haya ya upandaji miti kwani yameongeza uelewa
na ari kwa wananchi kuwa utunzaji mazingira ni jukumu la kila mmoja
wetu”, alisema Mhe.
Gama.
Naye
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez
alisema kuwa Umoja wa Mataifa unajivunia miaka 70 ya mafanikio katika
kukabiliana na changmoto mbalimbali zinazoikabili duniani kama vita,
uharibifu wa mazingira, ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba
maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mafanikio hayo na kuongeza
juhudi zaidi katika kukabiliana na changamoto hizo ili kuzimaliza
kabisa.
Aliongeza kuwa Umoja huo utaendelea kushirikiana kwa karibu
na Tanzania ili kuiwezesha kufikia malengo ya maendeleo na kutoa wito
kwa Serikali kuridhia Malengo mapya ya maendeleo
endelevu.
Kwa
upande wake Kiongozi wa Mabalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Filberto
Ceriani Sebregondi alisema kuwa Umoja huo utaendelea kusaidia miradi
mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo ile ya utunzaji misitu, maji na
kilimo pamoja na kuimarisha wakala mbalimbali za taifa ili kweza
kukabiliana na Mabadiliko ya
tabianchi.
Tukio hilo la upandaji miti ambalo ni sehemu ya maadhimisho
ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa ambayo yatafikia kilele tarehe 24
Oktoba, 2015, lilihudhuriwa na Watendaji kutoka Serikalini akiwemo
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, Mabalozi na
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na
Wananchi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni