Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuwa
mstari wa mbele katika kulinda na kuhakikisha amani iliyopo nchini
inadumu.
Balozi Mulamula ametoa wito huo
wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Alliance Française,
Jijini Dar es Salaam.
Balozi Mulamuala ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema kuwa kila Mtanzania anao
wajibu wa kuchangia katika amani ya nchi huku akiwataka vijana ambao ni
wengi kuhakikisha wanailinda amani iliyopo kwa ajili ya kujiletea
maendeleo yao na vizazi
vijavyo.
Aliongeza kuwa fursa mbalimbali
zikiwemo za uongozi na maisha bora hazipatikani kwa kutumia
nguvu wala vurugu na kuwataka vijana kujikita katika elimu, kufanya kazi
kwa bidii na uadilifu ili kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwa
viongozi wanaofaa hapo baadaye.
“Nahamasika kwamba vijana ambao
ni asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania wanao wajibu mkubwa katika
kulinda amani ya nchi yetu na ninaamini kuwa kijana anaweza kuwa
kiongozi popote pale alipo na katika lolote analolifanya hivyo nawaomba
mjijenge kwenye elimu, bidii katika kazi na kuwa waadilifu ili muwe
viongozi bora baadaye”, alisema Balozi
Mulamula.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015, Balozi Mulamula
aliwahakikishia wananchi kuwa utakuwa wa amani na utulivu na kwamba
wananchi wote wanao mchango mkubwa wa kuhakikisha amani inakuwepo wakati
wote wa uchaguzi hadi hapo utakapokamilika.
Vile vile alitoa rai kwa
wananchi kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka badala
ya kuingia mitaani na kusababisha uvunjifu wa
amani.
“Tumieni fursa iliyopo kuchagua
viongozi bora. Kura yako ndio amani yako. Hivyo nawaomba wote wenye
sifa mjitokeze kupiga kura wakati ukifika” alisisitiza Balozi
Mulamula.
Awali akizungumza kwenye
maadhimisho hayo, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa
nchini, Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa maadhimisho hayo ya 33
yanayobeba kauli mbiu isemayo Ushirikiano kwa ajili
ya Amani; Utu kwa Wote yamefanyika wakati muafaka
huku Tanzania ikijiandaa na uchaguzi mkuu na kuwataka vijana kuzingatia
utawala wa sheria kwani kupanga ni kuchagua na kwamba amani
ndio kitu cha kwanza.
Aidha, katika ujumbe wake
kwenye maadhimisho hayo uliosomwa na Bw. Rodriguez, Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Bw. Ban Kimoon ametoa wito kwa nchi zote duniani
zinazokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani kuweka silaha chini na
kurejea katika meza za mazungumzo. Aidha amezitaka nchi zote duniani
kuwekeza kwa vijana ambao ndio wajenzi wa
amani.
Akiwasilisha mada wakati wa
maadhimisho hayo kuhusu Wajibu wa Raia
katika Kutunza Amani”Kamanda wa Kwanza
wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa kupambana
na Waasi huko DRC, Meja Jenerali, James Mwakibolwa alisema kuwa
Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kutokana na juhudi za viongozi katika
kuhakikisha amani inadumishwa na vilevile ushirikiano mkubwa wa
wananchi kwa serikali
yao.
Aidha, aliongeza kuwa ili amani
iliyopo idumu ni muhimu kuwa na viongozi thabiti wanaotenda haki na pia
elimu ya uraia itolewe kwa wananchi kwani amani ikitoweka kila mtu
ataathirika kwa namna moja au
nyingine.
“Nimekuwa kwenye maeneo ya vita
na ukosefu wa amani na nimejifunza kuwa amani ikitoweka si rahisi
kuirejesha. Hivyo nawasihi Watanzania wenzangu kudumisha amani kwa kutii
sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama pale
inapohitajika ili nchi iendelee kuwa na amani na kukuza uchumi kwa
maendeleo ya nchi” alisema Meja Jenerali
Mwakibolwa.
Siku ya Kimataifa ya Amani
huadhimishwa duniani kote tarehe 21 Septemba kila mwaka ambapo
maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa
Wote” Mwisho
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni