MCHUANO wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajia kufanyika Oktoba
25, 2015 unaendelea maeneo mbalimbali ya nchini, huku vyama anuai
vilivyofanikiwa kuingia katika ushindani huo wa kisiasa vikinadi ilani
na sera zao kwa Watanzania ili kuwashawishi wachaguliwe.
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya kwanza kimemsimamisha mwanamke katika
ngazi ya juu ya uongozi. Kimemteuwa mwanamama, Samia Suluhu Hassan kuwa
mgombea mwenza wa mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho, John
Pombe Magufuli. Kwa mantiki hiyo endapo kitafanikiwa kushinda urais
Tanzania kwa mara ya kwanza mwanamke atashika nafasi ya juu ya madaraka
ndani ya Serikali.
Bi. Suluhu ambaye amewahi
kufanya kazi kama kiongozi katika Serikali zote mbili yaani Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar (Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar-SMZ) anauzoevu wa kutosha na elimu nzuri
inayomuongeze sifa ya kuimudu nafasi aliyopewa kwa sasa.
Ki
historia, Bi. Suluhu alizaliwa Januari 27, mwaka 1960 nchini na kupata
elimu yake ya msingi na sekondari Zanzibar, kabla ya kuendelea na elimu
ya juu kwa kozi mbalimbali katika vyuo vikuu vya Mzumbe nchini Tanzania,
Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza kwa ushirikiano na Chuo
Kikuu Huri cha Tanzania (OUT).
Mwanamama huyu pia
amefanikiwa kuchukua kozi ndogo ndogo anuai katika vyuo vya ndani na nje
ya Tanzania, vikiwemo vya; 'Institute of Management for Leaders,
Hyderabad, India', Zanzibar Institute of Financial Administration, ZIFA,
pamoja na National Institute of Public Administration, Lahore Pakistan.
Mgombea
huyo mwanamama amekuwa waziri na mbunge kwa zaidi ya miaka mitano
mfululizo na pia kufanikiwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge
Maalum la Katiba, nafasi ambazo kwa kiasi kikubwa zinamuongezea sifa ya
kuweza kuimudu nafasi aliyopewa kwa sasa anasema hii ni nafasi pekee
kwa akinamama wote bila kujali itikadi zao kumuunga mkono ili aweze
kushinda na kuweka historia nchini ya mwanamke kushika nafasi ya juu
kuliko zote nchini. Kwa sasa kiongozi huyu anazunguka mikoa mbalimbali
ya Tanzania Bara na Visiwani kuinadi ilani ya CCM.
Bi.
Suluhu anasema ilani ya CCM imepanga kufanya mengi mazuri kwa
Watanzania, lakini pamoja na hayo amejitolea kuhakikisha anawapigania
akinamama endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo ili kuweza kukabiliana
na changamoto anuai ambazo zimekuwa kero na kikwazo kwao.
Anazitaja
changamoto hizo ni pamoja na huduma za afya ya uzazi ambapo akinamama
wengi na watoto wachanga wamekuwa wakipoteza maisha katika eneo hilo.
Anasema licha ya ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM kufafanua zaidi itakavyo
boresha huduma za afya kiujumla, lakini atalisimamia na kuongeza nguvu
za ziada kuhakikisha akinamama wanapata huduma za kuridhisha maeneo
wanapopata huduma za afya ya uzazi.
Akihutubia
mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Mbulu Mjini anasema endapo CCM
itashinda uchaguzi huu imepanga kuajiri watumishi 15,000 wa sekta ya
afya wakiwemo madaktari 2020 ndani ya kipindi kifupi ili kuhakikisha
inaboresha zaidi huduma za afya maeneo mbalimbali nchini hasa huduma za
akinamama na watoto. Bi. Suluhu anasema hatua hiyo ni mpango maalumu wa
kuboresha huduma za afya kiujumla na hasa huduma za akinamama wajawazito
na watoto ambapo wamekuwa na changamoto katika huduma hizo.
Aidha
anaongeza kuwa mpango mwingine ni kuwawezesha akinamama na vijana
kiuchumi kupitia vikundi vyao. Anabainisha kuwa eneo hili Serikali ya
CCM kupitia ilani yake imetenga shilimi milioni 50 kwa kila kijiji fedha
ambazo zitakuwa zikikopeshwa makundi hayo kwa masharti nafuu ili waweze
kujikwamua kiuchumi.
Anasema eneo hilo pia halmashauri zitasimamiwa
kutoa asilimia tano ya mapato kuwaunga mkono akinamama na vijana ili
kuchochea maendeleo yao. Ili kukuza biashara zao Bi. Suluhu anasema
Serikali itasimamia kuhakikisha asilimia 30 ya tenda ndogondogo za
halmashauri mbalimbali zipewe vikundi vya akinamama na vijana.
Anaeleza
kuwa ili kuongeza thamani kwa mazao yatakaokuwa yakizalishwa na vikundi
hivyo kupitia miradi ya kilimo imepanga kujenga viwanda vingi maeneo
mbalimbali ya nchi ambavyo vitayaongezea thamani mazao na pia kuzalisha
ajira kwa asilimia 40, jambo ambalo pia litakuza uchumia wa akinamama na
vijana.
Mwanamama huyo shupavu anabainisha
kuwa kutokana na suala la kero ya maji pia kuwaumiza zaidi akinamama
ilani ya chama chake imedhamiria kumalizia miradi ya maji na kuanzisha
mingine anuai ili kukabiliana na changamoto ya kero ya maji safi na
salama iliyopo maeneo mbalimbali ya nchini vijijini ama mjini.
Bi.
Suluhu anasema Serikali watakayoiunda itaendelea kushughulikia kero ya
maji katika vijiji vyenye ukame na kuhakikisha kila kijiji kinapata maji
safi na salama kwa matumizi. Lakini ili kumaliza kabisa kero hiyo
anasema Serikali itaunda mfuko wa maji ambao utashughulikia kero za
huduma za maji safi na salama.
Anasema migogoro
yoyote inayosababisha mapigano idadi kuwa inayoathirika ni wanawake na
watoto, hivyo Serikali itakayoundwa na CCM itahakikisha inapima ardhi
yote ya vijiji pamoja na Wilaya na kuainisha mipaka ili kukomesha
migogoro ya ardhi inayochangia mapigano ya wakulima na wafugaji baadhi
ya maeneo ya Tanzania mara kwa mara.
Anasema mara baada ya kupima ardhi na kuweka
mipaka kati ya maeneo ya wakulima na wafugaji watahakikisha mipaka hiyo
inatambulika na kuheshimiwa na jamii zote mbili ili kuzuia migogoro na
mapigano ambayo yamekuwa na uhasama mkubwa na kupoteza uhai na mali za
raia wasio kuwa na hatia katika maeneo yenye mgogoro.
Hata
hivyo katika kampeni zake mara zote amemalizia kwa kuwaomba wananchi
kutunza amani iliyoasisiwa na viongozi wetu wa taifa kwa kutokubali
kuyumbishwa na kushawishia kuvuruga amani ya nchi. "...Tusikubali
kuchokozwa na kuchokoseka na kuvuruga amani...bila amani hakuna
maendeleo," alisema Bi. Suluhu.
Anawataka
viongozi wa siasa kuacha kutoa vitisho kwa wapiga kura kwani hali hiyo
ni kuibaka demokrasia hivyo CCM na vijana wake hawatakuwa tayari kuona
demokrasia inabakwa nchini na wapuuzi wachahe. "...Vijana wa CCM naomba
mkikamata kibaka wa demokrasia shughulikeni naye kidogo kabla ya
kumpeleka polisi...CCM itashinda kwa kishindo," alisema Nape Nnauye.
Miongoni
mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kulingana na taarifa ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni pamoja na CCM, CUF, CHADEMA, UMD, NCCR-
Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, TADEA, TLP, UDP, DEMOKRASIA MAKINI, CHAUSTA,
DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMMA na
ACT-Wazalendo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com





Hakuna maoni :
Chapisha Maoni