.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 21 Septemba 2015

QATAR YAONYESHA NIA YA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA UTALII VISIWANI ZANZIBAR


                                                                                                      Picha na – OMPR – ZNZ.

Qatar imeelezea shauku yake ya kutaka kuwekeza miradi ya Uchumi katika Sekta ya Utalii kupitia Taasisi na mashirika yake kutokana na rasilimali pamoja na mazingira bora ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar katika azma yake ya kumarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim Al – Maadad wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Abdulla Jassim Al – Maadad alisema yapo Mashirika na Taasisi kadhaa zinazojishughulisha na mausla ya sekta ya Utalii Nchini Qatar mbazo zinaweza kuitumia fursa ya uwekezaji iliyopo katika Visiwa vya Unguja na Pemba kwa vile miundo mbinu ya sekta hiyo tayari imeshaimarishwa vyema na Serikali.

Alisema mazingira mazuri yanayovizunguuka Visiwa vya Zanzibar katika uwekezaji yamempa matumaini ya kuitumia nafasi yake ya Kidiplomasia kujaribu kuyashawishi mashirika na Taasisi za Utalii Nchini mwake kuitumia nafasi hiyo adimu.

Balozi Abdulla Jassim Al – Maadad aliahidi kwamba uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Qatar na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla unastahiki kuimarishwa zaidi hasa kutokana na Wananchi wa pande hizo mbili kukaribia kushabihiana Kiutamaduni.

Alisema ipo haja kwa Taasisi za Utamaduni za pande hizo mbili kufanya mazungumzo ya pamoja yatakayotoa fursa kwa vikundi vya utamaduni vya pande hizo mbili kutembeleana sambamba na kufanya maonyesho ya pamoja katika azma ya kudumia uhusiano huo.

“ Ipo mikataba kadhaa ya ushirikiano iliyowahi kutiwa saini na viongozi wa pande hizi mbili. Sasa si vibaya pia tukauangalia utamaduni ambao ndio Seka Mama inayochangia kuwaunganisha haraka Wananchi wa Mataifa mawili tofauti ”. Alifafanua Balozi wa Qatar Nchini Tanzania Bwana Abdulla Jassim AL-Maadad.



Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Balozi wa Qatar Nchini Tanzania kwamba Mataifa hayo yanafanana katika masuala ya kiutamaduni jambo ambalo linastahiki kuimarishwa zaidi katika sekta ya uwekezaji.

Balozi Seif alisema Qatar kupitia shirika lake ya usafiri wa Anga inaweza kuanzisha safari za ndege zake kati ya Qatar na Zanzibar kwa vile Zanzibar tayari imeshaimarisha miundombinu ya uwanja wake wa Ndege katika kiwango kinachokubalika Kimataifa.

Alisema Qatar ina uzoefu mkubwa katika kusimamia masuala ya usafiri wa Anga jambo ambalo Wataalamu wake wanaweza kutumia fursa waliyonayo katika kufanya utafiti wa kuanzisha safari hizo.

Alifahamisha kwamba Zanzibar imekuwa kituo kikubwa katika usafiri wa Anga chenye uwezo wa kuwaunganisha wasafiri wa Kimataifa kuendelea na safari zao mahali popote Duniani.

Akizungumzia suala la Mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyopo Duniani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Qatar Nchini Tanzania kwamba Zanzibar imekuwa ikijiandaa na mikakati mbali mbali katika kukabiliana na mabadiliko yoyote ya Tabia Nchi yanayoweza kutokea.

Alishauri wataalamu wa Nchi hizo mbili wakaandaa mipango ya kushirikiana katika kufanya utafiti wa pamoja utakaosaidia nguvu zaidi katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Ushirikiano wa Kimataifa uliopo unaoyaunganisha Mataifa ya Ghuba ambao umeleta mabadiliko makubwa ya Kiuchumi kwa Mataifa hayo.

Balozi Seif alisema Dunia imekuwa ikishuhudia jinsi Mataifa ya Ghuba yanavyozidi kuimarika Kiuchumi kutokana na ushirikiano huo unaochangia kuleta ustawi mzuri kwa raia wa Mataifa hayo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni