Tanzania imetimiza masharti yote ya
kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka
Shirika la Maendeleo ya Milenia la
Millennium Challenge Corporation (MCC) la Marekani na itaanza kupata
na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi ya
MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya
Mpango wa MCC-2.
Habari hizo njema zimetangazwa
Jumamosi, Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu wa MCC, Bi. Dana J. Hyde
katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriot Essex House,
New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Bwana
Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC. Rais Kikwete yuko
New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa.
“Hongera Mheshimiwa Rais kwa
sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya
kupata fedha nyingine chini ya
mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa
Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Bi. Hyde
amemwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo
Waziri wa Nchi za Fedha wa Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.
Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete
kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti
wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana John Kerry, imeafiki
kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya
kupata fedha za MMC kuwa ni kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na
rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.
MCC imetoa taarifa ya kuthibitisha
kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi
ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya kuthibitisha
kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa
kukabiliana na rushwa.
Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa
na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na
nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua
aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo.
Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi
ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi,
Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo
kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC Bi.
Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI)
Balozi Mark Green.
Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa
mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wamajadiliano, upitishaji na
utekelezaji wa MCC–1.
Bi. Hyde amesema sasa linalobakia ni
kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni
hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2
yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania ikiwa ni
pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi nchini. Kiasi cha
asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10
ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa
MCC-1.
Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC,
Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na
sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698
(sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1 basi
Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za
maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita.
Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania
wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi
ambacho kimepata kutolewa na
Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium Challenge Corporation na
kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata
kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1
zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga,
Tanga-Horohoro na
Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga
upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya
Dar es Salaam na Morogoro na
zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa
10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo vile vile zilitumika
kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi
kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara
zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa
kiwango cha lami.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
27 Septemba, 2015

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni