Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataifungua Zanzibar katika Nyanja zote za maendeleo.
Amesema inawezekana kuibadilisha Zanzibar kimaendeleo kutokana na fursa nyingi zilizopo ikiwemo sehemu ilipo Zanzibar kijiografia, hali inayoifanya kuwepo katika eneo la kimkakati kimaendeleo.
Maalim Seif ameeleza mkakati huo wakati akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya garagara kwa ajili ya majimbo ya Mtopepo na Mwera.
Amesema mbali na nafasi hiyo ya kijiografia Zanzibar pia imebahatika kuwa na mandhari nzuri ukiwemo Mji mkongwe wa Zanzibar ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii.
Ametaja fursa nyengine za kimaendeleo zilizopo Zanzibar kuwa ni pamoja ardhi yenye rutba ambayo inakubali kuotesha mazao yote ya matunda, na kwamba iwapo itatumika vizuri inaweza kubadilisha hali ya uchumi wa Zanzibar.
Sambamba na hilo Maalim Seif ambaye pia ni mpiga kura wa jimbo hilo la Mtopepo amesema Zanzibar imebahatika kuwa na rasilimali ya mafuta na gesi asilia ambayo inatarajiwa kuchimbwa siku chake baada ya uongozi wake iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi na kuweza kuwanufaisha wananchi wote.
Amefahamisha kuwa miundombinu hiyo atakayoijenga itaweza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi bila ya matumaini ya kupata maendeleo.
Nae mgombea uwakilishi wa jimbo la Mtopepo Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema iwapo atachaguliwa kuliongoza jimbo hilo, atakamilisha miradi ya maji safi na salama, ili wananchi wote wa jimbo hilo waweze kupata maji majumbani mwao.
Aidha emesema anakusudia kujenga skuli mpya ya msingi na sekondari katika jimbo hilo ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wanaoupata, ikiwa ni pamoja na kupunguza msongomano wa wanafunzi madarasani.
Mhe. Mazrui pia ameahidi kuzijenga barabara za ndani za jimbo hilo ili ziweze kupitika wakati wote, sambamba na kuweka usafiri ambao utawasaidia zaidi wazee wa jimbo hilo.
Ameahidi kuwanunulia kompyuta wanafunzi wote wa jimbo hilo watakaofaulu kuingia vyuo vikuu ili kurahisisha shughuli zao za kimasomo.
Mapema akitoa salamu wa wanawake, mwakilishi wa viti maalum anayemaliza muda wake Mhe. Zahra Ali Hamad, amesema vijana wengi hasa wa kike wamekata tamaa kutokana na ukosefu wa ajira, na kwamba zaidi ya vijana elfu mbili waliosomea fani ya uwalimu kati ya mwaka 2007-2008 bado hawajaajiriwa.
Hivyo amewaomba vijana kukipigia kura Chama Cha CUF ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo na kuwakwamua kimaendeleo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni