Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha Wananchi kuwakataa Madereva wanaoendesha vyombo vya moto ambao baadhi yao wanashindwa kuzingatia sheria za usalama Bara barani.
Amesema wapo madereva wanaochukuwa abiria kupindukia kiwango kinachokubalika hasa kipindi hichi cha Kampeni na kuendesha vyombo vyao kwa mwendo wa kasi licha ya tahadhari zinazoendelea kutolewa kila siku na Jeshi la Polisi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo baada ya kuwapa pole majeruhi Tisa waliolazwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja wakipatia matibabu kufuatia ajali Tatu za vyombo vya moto zilizotokea wakati wafuasi wa Chama cha Mapinduzi wakirejea kutoka kwenye Mkutano wa Kampeni ya Uchaguzi Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema Serikali Kuu kamwe haipendelei kuona Wananchi wake wanakuwa katika hali ya wasi wasi wakati wanapotumia usafiri wa Bara bara katika shughuli na harakati zao za Kimaisha.
Akiwakagua Majeruhi hao mapema asubuhi Balozi Seif Ali Iddi amewatakia matibabu mema na kuwaombea kwa Mungu wapone haraka ili warejee katika familia zao kuendelea na maisha yao ya kila siku.
Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa Mahatuti { ICU } kiliopo Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Raya Moh’d alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hali za wagonjwa hao zinaendelea vyema na hakuna mtu aliyefariki katika matukio hayo.
Hata hivyo Bibi Raha alisema Said Ali Juma mwenye Umri wa Miaka 23 Mkaazi wa Mtaa wa Sogea aliyelazwa katika chumba Mahatuti { ICU }hivi sasa amepata nafuu kidogo ikilinganishwa na muda aliolazwa hospitalini hapo kwa matibabu.
Alisema Mgonjwa Said ambae amepata mshtuko wa kichwa kwa sasa anaweza kuonyesha ishara ya lile analolihaji kuhudumiwa hali inayoleta matumaini na faraja hata kwa wauguzi wenyewe.
Naye Ramadhan Hussein Masoud akiwa miongoni mwa majeruhi wa ajali hizo alimueleza Balozi Seif kwamba Dereva wa Gari aliyokuwa akisafiria ainaya Noha alikuwa akiendesha gari hiyo kwa mwendo wa kasi na kupuuza ushauri waliokuwa wakimpa.
Katika kukabiliana na ajali zinazoweza kuepukwa Uongozi wa Chama cha Mapinduzi umeagiza Gari zote zinazokwenda kwenye Mikutano ya Kampeni ya Chama hicho Madereva wake watalazimika kufuata utaratibu uliowekwa wa magari yao kurudi mikutanoni kwa pamoja.
Utaratibu huo utakaoongozwa na Gari ya Polisi utasaidia kuepuka ajali pamoja na kuwadhibiti madereva wasiozingatia sheria za usalama Bara barani ambao wengine huamua kufukuzana bila ya kujali maisha ya wenzao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni