Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Asasi
za Kiraia zina nafasi kubwa katika utatuzi wa migogoro na kuleta amani
hususan katika eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa
ujumla.
Balozi Mulamula aliyasema hayo jana wakati
akifungua mkutano wa Wenyeviti wa Asasi za Kiraia kutoka Nchi za Maziwa
Makuu unaofanyika kwa siku mbili katika Hoteli ya Golden Tulip, Jijini
Dar es Salaam.
Balozi Mulamula ambaye pia aliwahi kuwa Katibu
Mtendaji wa Kwanza wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu alisema kuwa kwa
uzoefu wake utatuzi wa migogoro, kulinda amani na katika kuhakikisha
demokrasia na utawala wa sheria vinafuatwa kila chombo kina nafasi na
umuhimu wake na kwamba Asasi za Kiraia zina nafasi kubwa zaidi kwani
zinawakilisha maoni ya wananchi.
“Asasi za Kiraia ni chombo muhimu sana katika
kuhakikisha amani inakuwepo hususan katika Ukanda wa Maziwa Makuu kwani
zinawawakilisha wananchi moja kwa moja hivyo ni vizuri kutambua nafasi
yenu”, alisema Balozi Mulamula.
Aidha, aliipongeza Asasi hiyo ya ambayo kwa kiasi
kikubwa imefanikiwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2011 na kusisitiza ijikite
zaidi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria
katika nchi za Ukanda wa Maziwa makuu vinafuatwa na kutekelezwa
kikamilifu.
“Najua mnazijua hadidu za rejea na wajibu wenu kama
Asasi za
Kiraia, ni kuhakikisha nchi wanachama zinafuata misingi ya sheria,
utawala bora na ule wa sheria ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara
katika eneo letu la Maziwa Makuu”, alisisitiza Balozi
Mulamula.
Awali akimkaribisha Balozi Mulamula kuzungumza,
Mwneyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere, Mzee Joseph Butiku alisema kwamba mkutano huo wa Wenyeviti wa
Asasi kutoka nchi wanachama wa Maziwa Makuu ni muhimu sana hususan
katika kipindi hiki ambapo pamoja na mambo mengine utaandaa na kupitisha
agenda za Asasi hiyo zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi
unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2016.
Aidha, aliongeza kuwa wakati umefika kwa Nchi
Wanachama wa Maziwa Makuu kutambua mchango wa asasi za kiraia na kuzishirikisha
ipasavyo katika msuala muhimu hususan yale ya utatuzi wa migogoro ili
kuleta tija kwenye eneo hili la Maziwa Makuu ambalo kwa kiasi kikubwa
limekuwa na migogoro ya kisiasa na kikabila.
Mkutano huo wa siku mbili uliwashirikisha Wenyeviti
wa Asasi kutoka nchi zote 12 wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu
ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Jamhuri
ya Congo, Angola, Sudan na Zambia.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni