Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Hayo yamewekwa bayana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi wakati wa wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Bw. Samkyi alisema TABD imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu maalum kwa sekta ya kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye tija kwa wakulima nchini.
“Benki imejipanga kutoa mikopo yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani katika tasnia za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima wadogo wadogo, hatahivyo, hata wale wakulima wa kati na wakubwa watahudumiwa.
Bw. Samkyi imejidhatiti katika kufanya tathmini ya kina katika mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi kwa minajili ya kuongeza thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera ya TADB ni kutathmini mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na uwezo wa ushindani kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi na kupunguza umaskini,” aliongeza.
Katika hafla hiyo, jumla ya vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo 857, vilimiza vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Kwa mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya vikundi 89 vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama Amina Masenza aliwasihi wakulima kutumia mikopo hiyo kwa malengo waliyojiwekea na walivyokusudia.
“Naamini, wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya mikopo hii iweze kuona matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao mmeweza kubahatika kupata fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za TADB,” aliwasihi.
Mama Masenz aliwaomba wakulima hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua vilivyo, hasa nia ya kutoka katika kiwango fulani cha maisha kwenda katika hatua nyingine za juu zaidi kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora wa kimaisha kwa ujumla kupitia huduma za TADB.
“Nawasihi kutotumia pesa hizi kinyume na malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa kufanya hivyo, siyo tuu tunaiua Benki yetu bali pia tunajimaliza wenyewe kiuchumi. Wito wangu kwenu ni kujipanga kwa dhati ili kuweza kutimiza malengo makuu ya mikopo hii ambayo ni kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8 Agosti 2015 mjini Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na wadau wengine wa maendeleo ili Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za kimaendeleo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni