Utangulizi
1.1 Jana, tarehe 30
Novemba, 2015, mahakama jijini London ilitoza Standard Bank $ 32.2
milioni. Kati ya hizo $ 16.8 milioni ni faini inayolipwa kwa Serious
Fraud Office (SFO), $8.4 milioni ni “disgorgement of profits”; na $ 7
milioni zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania. Fedha hizo ni $ 6 milioni
ambazo tulitozwa isivyostahili na $ 1 milioni ni riba ya fedha hizo.
Fedha tunazorejeshewa zililipwa isivyostahili kwa kampuni ya Kitanzania
iitwayo EGMA. Kesi inayohusika ilifunguliwa na SFO dhidi ya Standard
Bank.
1.2 Mwaka
2012/13, Serikali ya Tanzania iliamua kukopa fedha ($600 milioni) kwa
ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Huu ni utaratibu wa kawaida,
ambapo Serikali inaingia mkataba na Benki moja (Lead arranger) ambayo
inatafuta fedha kutoka kwenye benki na taasisi nyingine za fedha. Ni
utaratibu wa kawaida pia kuwa Lead Arranger analipwa ada kwa kazi hiyo.
1.3 Serikali
ya Tanzania ilitoa kazi hiyo kwa Standard Bank, kupitia Stanbic (T)
Ltd. Fedha tulizohitaji, $600 milioni ambazo wakati huo zilikuwa sawa na
Sh.947,673,240,000.00 zilipatikana na zikatumika kama ilivyokusudiwa.
Standard Bank ililipwa asilimia 2.4 ya fedha hizo kama ada yao. Mkopo
ulikuwa na masharti ya grace period ya miaka miwili na nusu na kulipwa
kwa miaka 7 (2019).
2.0 Uchunguzi Nchini Tanzania
2.1 Mwaka
2013 kulikuwa na matatizo kwenye Stanbic Bank (T) Ltd, wakati huo
ikiongozwa na Bwana Bashir AWALE. Kwa kutumia mamlaka yake chini ya
Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha
Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ilifanya
ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) benki hiyo.
2.2 Wakaguzi
wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine, walibaini malipo yasiyokuwa ya
kawaida kuhusiana na kampuni ya Kitanzania inayoitwa EGMA. Malipo hayo
yalikuwa kinyume na taratibu za kibenki, na baadhi ya watumishi wa
Stanbic Bank (T) walishindwa kuvumilia hali hiyo. Wakaguzi wa Benki Kuu
walifuatilia malalamiko hayo na kujiridhisha kuwa uongozi wa Stanbic
Bank (T) ulifanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu zinazokubalika
kibenki.
Fedha kiasi cha $ 6 milioni kiliingizwa kwenye akaunti ya EGMA
na siku chache baadaye zilitolewa zote kwa fedha taslimu na wala benki
haikukusanya kodi ya zuio (withholding tax) kwa mujibu wa sheria ya
mapato ya kodi ya mwaka 2004 kutokana na mapato ya Standard Bank kwa
kazi ya ushauri iliyoifanya.
2.3 Kama
ulivyo utaratibu, Benki Kuu ilitoa taarifa ya ukaguzi kwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Stanbic Bank (T) Ltd na kuitaka Bodi hiyo kuchukua hatua za
kurekebisha kasoro ndani ya benki, pamoja na kutoa taarifa kwa Financial
Intelligence Unit kuhusiana na miamala yenye mashaka kwenye akaunti ya
EGMA kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering Act 2006.
2.4 Taarifa
tulizopewa ni kuwa bodi ilikutana na kuchukua hatua zinazostahili,
ikiwemo kutoa taarifa FIU kuhusiana na miamala kwenye akaunti ya EGMA,
na kwa Wizara ya Fedha kuhusiana na kodi ya zuio.
2.5 Vile
vile tumesikia kuwa bodi ya Standard Bank iliona kuwa makosa
yaliyobainishwa na wakaguzi wa Benki Kuu ya Tanzania yalistahili
kutolewa taarifa kwa SFO nchini Uingereza ambao walianzisha uchunguzi
ambao hatimaye ulipelekea kesi kufunguliwa.
3.0 Udanganyifu ulivyofanyika
3.1 Kwa
taarifa zilizopo, inaelekea kuwa Standard Bank ilipanga kututoza ada ya
asilimia 1.4 tu, yaani $ 8,400,000. Hata hivyo ukafanyika ujanja wa
kudai kuwa ati anahitajika local agent wa benki hiyo, ambaye naye alipwe
asilimia 1 nyingine, na kufikisha ada yote kuwa asilimia 2.4
($14,400,000).
3.2 Local
agent huyo alikuwa kampuni ya EGMA, ambayo miamala yao kuhusiana na hizo
$6,000,000 walizochukua ndiyo ilishtua wakaguzi wa Benki Kuu na taarifa
kutolewa kwa Bodi ya Stanbic (T) Ltd na hatimaye Standard Bank, SFO na
Mahakama Uingereza.
4.0 Uchunguzi Uingereza
4.1 Tarehe
29 Septemba, 2015, Mkuu wa Idara ya Rushwa kwenye SFO aliiandikia Benki
Kuu, akiomba ushirikiano wa Benki Kuu kwenye uchunguzi na uendeshaji wa
kesi dhidi ya Standard Bank Plc (ambayo sasa inajulikana kama ICBC
Standard Bank Plc).
4.2 Tarehe
29 Oktoba, 2015, Benki Kuu, iliiandikia SFO kutoa taarifa kuhusu
ukaguzi-lengwa ambao Benki Kuu iliufanya tarehe 15 – 19 Julai, 2013
kwenye Benki ya Stanbic Bank (T) Ltd.
Ushahidi huo kutoka Benki Kuu
ulikuwa sehemu ya ushahidi uliosaidia SFO kushinda kesi. Katika kipindi
chote ambacho SFO ilikuwa inafanya uchunguzi, ilishirikiana na taasisi
zetu ikiwamo TAKUKURU, Benki Kuu, FIU na wengine. Mafanikio haya
yaliyopelekea kwenye uamuzi wa Tanzania kurejeshewa $ 7 milioni (Sh.15
bilioni/=) yametokana na dhamira ya kweli ya Serikali ya Uingereza na
Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa.
5.0 Hitimisho
5.1 Tunaishukuru
Serikali ya Uingereza, pamoja na SFO, kwa kuonesha njia katika kusaidia
nchi maskini zinazodhulumiwa na wapokea rushwa na watoa rushwa. Maana
zipo nchi nyingine tajiri ambazo wanapigia kelele rushwa kwa kuangalia
upande wa mpokeaji tu, na kusahau makampuni makubwa kutoka kwao
yanayopenda kuhonga watu wetu.
Natoa wito kwa nchi nyingine tajiri kutoa
ushirikiano kama huu wa Serikali ya Uingereza. Nazishukuru taasisi
zetu, Benki Kuu, na TAKUKURU, FIU na wengine kwa kutimiza wajibu wao na
kutoa ushirikiano kwa SFO uliowezesha SFO kushinda kesi hii, na sisi
kurejeshewa fedha ambazo zitatumika kutatua matatizo yetu ya maendeleo
na kero za wananchi.
5.2 Baada ya
ushindi huo uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili tujue hizo $ 6
milioni zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu tujue ni nani.
Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya EGMA ambao kwa
taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Bwana Harry KITILLYA,
aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bwana MBOYA
ambaye ni marehemu na Bwana Gasper NJUU.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni