MFUKO
wa Maendeleo ya Mtaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) umetoa msaada wa
shilingi bilioni 2.4 kama kianzio cha mtaji kwa waandaaji wa miradi
kutoka sekta binafsi na umma.
Katika hafla iliyofanyika leo na kufunguliwa na
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Kagyabukama Kiliba hawala sita
zilikabidhiwa wawakilishi wa waendeshaji katika miradi iliyotawanyika
sehemu mbalimbali nchini.
Pamoja
na hawala hizo za bilioni 2.4 imo pia shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya
miradi yenye mwelekeo wa kibiashara inayoandaliwa na mamlaka za serikali
za mitaa nchini Tanzania.
Miradi iliyopewa kianzio cha mtaji ni pamoja na halmashauri
ya mji wa Kibaha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha basi na soko la
kisasa, halmashauri ya manispaa ya Moshi kwa ajili ya kituo cha kisasa
cha mabasi cha biashara na manispaa ya Ileje kwa ajili ya ujenzi wa
mnara wa redio kwa kushirikiana na sekta
binafsi.
Mradi
mwingine ni wa uzalishaji wa umemejua (mtandao wa vijijini)
unaotekelezwa wilaya ya Korogwe na kampuni binafsi ya Ensol, mradi
binafsi wa uzalishaji umeme kwa maji unaoendeshwa na wanawake wa wilaya
ya njombe vijijini na mradi mdogo binafsi wa uzalishaji umeme wa Maguta
uliopo wilayani Kilolo.
Akizungumza kumkaribisha mgeni rasmi kutoa hundi hizo, Mkuu
wa UNCDF nchini Tanzania Peter Malika alisema msaada uliotolewa umelenga
kuonesha mafanikio ya program ya mradi wa fedha za nahalia (LFI) wa
UNCDF katika kusaidia waandaaji wanaojishughulisha na miradi inayotoa
mchango katika maendeleo ya uchumi ya maeneo
husika.
“Licha
ya kuongezeka kwa upatikanaji wa mtaji wa uwekezaji kutoka vyanzo vya
umma na binafsi kwa ajili ya miundombinu, ni kiasi kidogo sana
kinachofikia miundombinu ambayo inaunda uti wa mgongo wa michakato ya
uchumi. LFI ilibuniwa ili kushughulikia changamoto hizi na uliundwa ili
kuonyesha kwamba miradi ya miundombinu ambayo inapewa kipaumbele na
serikali za mitaa na jamii inaweza kuvutia fedha endapo matatizo ya soko
la mtaji yaliyopo yatashughulikiwa” alisema
Malika.
Aidha
Malika alisema katika mwaka huu timu ya LFI ilitoa msaada wa kiufundi wa
kulenga na kianzio cha mtaji kwa zaidi ya miradi 30,tisa kati ya hiyo
ikiwa katika hatua za juu na kwa hiyo kuwa tayari kupokea uwekezaji
ikiwemo miradi tisa iliyotunukiwa msaada
jana.
Tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2012 LFI-T imesaidia zaidi ya miradi ya maendeleo
ya mahalia 30 nchini Tanzania katika hatua mbalimbali tangu uwekaji
mipango hadi kuwa tayari kupokea uwekezaji kwa kufanyakazi kwa karibu na
Tamisemi na taasisi za fedha.
Aidha
LFI-T inasaidia miradi katika mikoa 18 iliyo katika sekta mbalimbali
ikiwamo ya usindikaji mazao ya kilimo, tabia nchi, nishati salama na
uzalishaji wa bidhaa za viwandani.
Naye Naibu Katibu Mkuu Kiliba akizungumza na
hadhara kabla ya kutunuku hawala hizo sita alisifu kazi ya ubunifu
iliyofanywa na UNCDF katika utoaji fedha kwa maendeleo ya jamii na
kusema hiyo ndiyo njia sahihi ya kusababisha
maendeleo.
Pia
aliwapongeza waanzishaji wa miradi walipookea kianzia cha mtaji wa
uwekezaji kutoka UNCDF na kuwatakia mafanikio mema huku akisema kwamba
serikali ya Tanzania inakaribisha uendelezwaji wa program ya
LFI-Tanzania.
Kiliba
alisema kwamba wizara yake imeanzisha kitengo maalumu cha kuhakikisha
kwamba miradi ya ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika
halmashauri inafanikiwa.
Mmoja wa wakurugenzi wa halmashauri waliopewa mtaji huo wa
kianzio, Jenifa Omolo kutoka halmashauri ya mjui wa Kibaha alishukuru
UNCDF kwa kufanikisha halmashauri ya Kibaha kuwa na soko la kisasa na
kituo cha basi cha kisasa.
AlisemaUNCDF na Tamisemi wamekuwa mstari wa mbele katika
kuwezesha kutekelezwa kwa wazo hilo kuanzia mwanzo hadi sasa wanapopata
mtaji huo.
Alihimiza halmashauri nyingine nchini kupata msaada wa
kiufundi kwa mawazo yao kutoka UNCDF ili kuwa na uwezo wa kusimamia
maendeleo ya umma na jamii.
“Hatuna soko katika mji wetu, kuna magenge tu na tuna kituo
kidogo tu cha mabasi ambacho hakikidhi mahitaji- hizi zimekuwa
changamoto kubwa kwetu kwa zaidi ya miaka kumi. Mji wetu unakua na sasa
tunahitaji kuwa na miundombinu ya kisasa” alisema Omolo na kuongeza kuwa
mji wa Kibaha una wajibu wa kutoa huduma bora na kwamba miundombinu
mipya na ya kisasa itasaidia kuongeza mapato kwa mji
huo.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni