TUME ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (THBUB) imepokea taarifa ya tarehe 27 Januari, 2016 kutoka
Bungeni kuhusu uamuzi wa Serikali kupunguza matangazo ya moja kwa
moja (Live) ya vikao vya Bunge kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).
Tume inafanyia uchambuzi taarifa hizo ili kuona kama uamuzi huo
hautaingilia haki ya wananchi kupata habari chini ya Ibara ya 18(d),
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha Tume imesikitishwa na vurugu
zilizotokea Bungeni baada ya uamuzi huo kutolewa ambapo zilisababisha
askari wa kutuliza ghasia (FFU) kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge.
Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977 inatamka kuwa, “ ...Bunge...
ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na
madaraka, kwa niaba ya Wananchi, kusimamia na kuishauri Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii”.
Mantiki ya Ibara hii ni kwamba Bunge
ni muhimili wa kitaifa unaowakilisha wananchi kuisimamia na kuishauri
Serikali (executive) na vyombo vyake katika kutekeleza majukumu yake
(executive) na si kinyume chake.
Tume inaamini kwamba vurugu siyo
njia sahihi ya kupata muafaka wa mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge
hawakubaliani nayo.
Aidha, Tume inatamka kwamba kitendo
cha askari wa kikosi cha FFU kuingia bungeni kuwatoa Wabunge
waliokuwa wakifanya vurugu ni kitendo kilichodhalilisha Bunge kama
muhimili muhimu wa Taifa na ni kitendo cha aibu kwa Taifa.
Mwisho, Tume inatoa rai kwa uongozi
wa Bunge na Wabunge wote kuzingatia kanuni za Bunge katika kutekeleza
shughuli za Bunge.
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA
BORA
Januari 29, 2016

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni