.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 14 Februari 2016

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR ASEMA HAONI HAJA YA KUREJEWA MAZUNGUMZO NA MAALIM SEIF

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani hapo uwanja wa ndege wa Pemba kabla ya kurejea Unguja baada ya kumaliza ziara ya Siku Tatu Kisiwani Pemba. Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai na Kushoto ya Balozi Seif ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Panadu Ameir Kificho.
Balozi Seif akijibubaadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari alipokutana nao uwanja wa ndege wa Pemba baada ya kukamilisha ziara yake ya siku Tatu Kisiwani humo. Kushoto ya Balozi Seif ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Mh. Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Dr. Maua Daftari. Picha na – OMPR – ZNZ.

Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwa vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeshatangaza Tarehe ya Kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yeye binafsi haoni umuhimu wa kurejewa kwa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein .

Alisema mazungumzo hayo kwa sasa hayana tija yoyote kwa vile Wananchi katika kipindi hichi wameanza kujiweka tayari wakijiandaa kupiga kura kufuatia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } kufuta matokeo ya uchaguzi Tarehe 28 Oktoba mwaka 2015.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Uwanja wa ndege wa Pemba akijiandaa kurejea Kisiwani Unguja baada ya kumaliza ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba kukagua shughuli mbali mbali za Maendeleo akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali Balozi Seif Ali Iddi alisema iwapo yapo malalamiko yoyote muhusika wake ana wajibu wa kwenda Mahakamani kwa hivi sasa.

Balozi Seif alisema mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi {CUF } Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif ambae yeye binafsi ndie aliyeamua kujiondoka kwenye maendeleo ya vikao vya mazungumzo hayo.

Alisema kinacholikabili Taifa kwa wakati huu ni suala la marejeo ya uchaguzi na kuwaomba watu walioamua kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio ni vyema wakabakia nyumbani ili kutoa fursa kwa wenzao waliokubali kushiriki watumie haki yao ya Kidemokrasia kuwachaguwa Viongozi wanaowataka.

Balozi Seif alifahamisha kwamba hata yeye anaheshimu maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Z anzibar ambayo haiwezi kuingiliwa na chombo chochote licha ya kwamba Tayari alikuwa ameshashinda na kupewa cheti kinachothibitisha kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda.

Tupo tuliokwishashinda kwenye chaguzi zetu za Majimbo na kupewa vyeti vinavyothibisha ushindi huo lakini baadhi yetu kwa nini tuendelee kushutumu maamuzi ya tume ambayo kutokana na sababu za msingi ilizoeleza za kujitokeza kwa dosari kadhaa kwenye zoezi zima ikalazimika kufuta matokeo na uchaguzi wote ? ”. Aliuliza Balozi Seif.

Akizungumzia uvumi uliojitokeza wa kuwepo kikundi cha Vijana wanaopiga watu katika badhi ya maeneo maarufu Mazombi Balozi Seif alisema hana taarifa yoyote iliyomfikia akiwa kama Kiongozi wa Juu wa Serikali kuhusu shutma hizo.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa agizo kwa vyombo vya Ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya shutuma hizo na pale itakapobainika kuwepo kwa shutma hizo vifanye juhudi ya kuwakamata wahusika hao na kuwafikisha mbele ya Doli ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Balozi Seif alieleza kwamba nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ile ya Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania ni kuiona nchi inaendelea kubakia katika hali ya amani na utulivu wakati wote kabla na baada ya uchaguzi.

Aliwaasa na kuwaomba Wananchi wa maeneo mbali mbali Kisiwani Pemba kuendelea kuishi kwa amani na upendo na kushirikiana katika mambo yao bila ya kuendekeza zaidi itikadi zao za Kisiasa ambazo tayari zimeshaonyesha muelekeo mbaya.

Alieleza kwamba matokeo ya sasa yaliyojichomoza katika hujuma za moto sambamba na baadhi ya watu kuanza kuashiria vitisho dhidi ya wananchi wenzao walioamua kushiriki uchaguzi wa marejeo kwa kuwatilia X nyumba zao yanaonyesha safari ya hatari katika maisha miongoni mwa jamii.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni