TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na
kunusa harufu ya ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati
mpya tatu.
Wazi Mkuu ambaye alikagua eneo la ujenzi wa gati hizo jana
(Jumamosi, Februari 27, 2016), alisema anazo taarifa juu ya utolewaji
wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu
wa manunuzi kupitia PPRA ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.
Aliwaomba wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia
suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuleta ajira kwa
wana Mtwara. "Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali
hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa
yataongezeka", alisema.
"Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo
moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi
tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai
kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu.
Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi," aliongeza.
"Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati
zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi
tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho
watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine."
"Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji
kutumbuliwa. RCC ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote
ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bosi hiyo wanatoa
vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam. "
Alimtaka mkuu wa bandari ya Mtwara (Port Master) Bw. Prosper
Kimaro awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo
kwani kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na
ujanja wa watu wachache.
"Hapa si kuna mtu alitaka kuiba sh. milioni 300 kwa kufoji
saini za wakubwa wake? alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na
Bw. Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi
huo haujakamilishwa.
Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao
wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, Waziri Mkuu
aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba kiasi
cha sh. bilioni 13.8/- kimekwishatengwa na Wizara na kitatolewa
mapema mwezi ujao.
Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo
zinatumiwa kuingiza sukari na mchele mchezo ambao unaikosesha
Serikali mapato. "Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo
wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa
kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa
kodi ya Serikali," alisisitiza.
Naye, Mkuu wa bandari hiyo, Bw. Kimaro wakati akitoa taarifa ya
utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema bandari hiyo
ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa gati ya
kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo na kwamba hivi
sasa wamekwishapata winchi ya bandarini (harbour crane) yenye uwezo
wa kubeba tani 100 na tayari wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 28, 2016.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni