Imeelezwa kuwa wastani wa unyonyeshaji kwa watoto walio chini ya
miezi sita nchini sio mzuri na hivyo kuwa na uwezekano wa watoto
kudhoofika kwa kukosa maziwa ya mama ambayo yanakuwa na virutibisho
muhimu kwa ukuaji ya mtoto.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Joyceline Kaganda katika warsha
iliyoandaliwa na UNICEF ili kujadili jinsi uwekezaji mkubwa zaidi katika
kunyonyesha maziwa ya mama kunaweza kusaidia maendeleo kiuchumi na
kuokoa maisha ya watoto nchini.
Dkt. Kaganda amesema wastani wa unyonyeshaji
kwa watoto walio chini ya miezi sita ni asilimia 42 na wastani huo ni
mdogo hivyo kuashiria kuwa hali sio njema kwa watoto ambao hawapati
maziwa ya mama.
Amesema kiafya inatakiwa mtoto aanze kunyonya
nusu saa baada ya kuzaliwa na mtoto anyonye maziwa ya mama yake kwa
kipindi kisichopungua miezi sita na baada ya hapo anaweza kuanza kuwa
anachanganya na vyakula vingine kama uji na
maji.
“Hali sio nzuri ukiangalia wastani wa wamama
ambao wanawapa watoto wao maziwa ya kunyonya ni wachache na labda
inawezekana wengi wakawa hawatambui matatizo yanayoweza kutokea kama
hawatawanyonyesha watoto wao,” amesema Dkt.
Kaganda.
Aidha Dkt. Kaganda amesema kazi zinachangia
kina mama wengi kushindwa kuwanyonyesha watoto wao lakini wanaweza
kuweka utaratibu wa kuwa wanakamua maziwa yao na kuyahifadhi sehemu
nzuri ili hata kama wanapokuwa mbali na watoto wao, msimamizi
anayemuangalia mtoto aweze kumpa mtoto ili kumfanya apate virutubisho
muhimu kutoka kwenye maziwa ya mama
yake.
Nae Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman amesema katika
kusaidia Tanzania kuongeza wastani wa watoto ambao wananyonya wamekuwa
wakitoa elimu kwa kina mama wanaonyonyesha pamoja na familia zao ili
wajue umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya
mama.
Alisema watoto wengi wamekuwa wakipoteza
maisha kwa matatizo ambayo yanatokana na kukosa maziwa ya mama zao na
hivyo ili kuzidi kushughulikia tatizo hilo wanataraji kuanza kutoa elimu
kwa watumishi wa afya katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe na
wanataraji kutembelea zaidi maeneo ya vijijini kutokana maeneo hayo
kuonekana kutokuwa na elimu hiyo
zaidi.
“Watoto wamekuwa wakipata matatizo na
kupoteza maisha na hiyo inachangiwa na kutokunyonya kwa mama …
tumeshirikiana na serikali tunataraji kutoa elimu katika vijiji zaidi ya
15,000 kwenye mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya na tutafundisha pia mama
na familia umuhimu wa mtoto kunyonya,” alisema Bi.
Zaman.
Alisema baada ya kumalizika kwa mikoa hiyo
wataendeleza utoaji wa elimu nchi nzima ili jamii ya Tanzania itambue
umuhimu wa watoto kunyonya maziwa ya mama na pia kuwaomba waandishi wa
habari kutumia nafasi yao katika jamii ili kuwaelimisha watanzania
kuhusu tatizo hilo.
Katika makala zilizoandikwa katika jarida la
habari za afya la The Lancet linaonyesha kuwa uboreshaji wa kunyonyesha
maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha zaidi ya watoto 820,000 kila mwaka
duniani na Dola za Kimarekani Bilioni 302 kila mwaka.










Hakuna maoni :
Chapisha Maoni