WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema serikali inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Nanganga, Ruangwa hadi Nachingwea.
Hatua hiyo itawezesha kutatuliwa kwa kero ya changamoto ya miundombinu ya barabara inayowakabili wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema barabara hiyo ambayo kwa sasa haipo katika hali nzuri itajengwa kwa kiwango cha lami, ambapo serikali inatarajia kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Hayo yamesemwa jana jioni (10 Aprili, 2016) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Likunja, Nkowe na Namahema katika mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi.
Amesema serikali imejipanga katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwamba mara baada ya kumalizika kwa upembuzi yakinifu ujenzi wa barabara hiyo utaanza, hivyo amewataka wananchi kuwa na subira.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka wananchi wa vijiji hivyo kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi zao za kisiasa kwa sababu uchaguzi ulishamalizika tangu Oktoba 25 mwaka jana.
“Mimi nitaendelea kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwahudumia, nawaomba tushirikiane na tuweke kando masuala ya itikadi za vyama, sasa ni wakati wa kazi, hivyo ni bora tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo ya Ruangwa jambo ambalo linawezekana.
Hata kama wewe ambaye najua ulinichukia mimi nimekusamehe kutoka moyoni, wewe ni wangu hata kama hukunichagua nitakuhudumia na kukutumikia kwa sababu mimi ndiye mbunge wako hivyo naomba tushirikiane,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya aliomba wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wilaya yao na hatimaye iweze kupiga hatua.
MWISHO
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni