Mwanzilishi wa Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation), Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa (kushoto), mgeni rasmi Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji (kulia) pamoja na Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Mkapa Foundation, Balozi Charles Sanga wakiwasili katika sherehe za miaka 10 ya Mkapa Foundation zilioambatana na harambe ya kutunisha mfuko wa taasisi hiyo zilizofanyika kwenye ukumbi wa Golden Jubilee Tower. (Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu (kushoto) akimkabidhi zawadi ya picha aliyoinunua kwenye harambee kwa shilingi Milioni 5.5 mgeni rasmi Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji (katikati) ambapo mnada wa picha hiyo uliendeshwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi.
Katika kusherekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Benjamin Mkapa, imefanyika harambee ambapo jumla ya Bilioni moja na Milioni mia moja na sabini zimechangishwa na wadau mbalimbali ambao wanasapoti taasisi hiyo inayojishughulisha kusaidia jamii.
Baadhi ya watu ambao wamechangia pesa ni pamoja na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limeted (METL Group), Mohammed Dewji ambaye amechangia kiasi cha Milioni 210 akiwa kama mgeni rasmi katika sherehe za kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Benjamini Mkapa (Mkapa Foundation) ambapo Milioni 200 imetolewa na Taasisi ya Mohammed Dewji (Mo Dewji Foundation) na Milioni 10 imetolewa na MeTL Group.
Akitoa hotuba katika sherehe hiyo, Mohammed Dewji amesema kuwa ametoa msaada huo ili kuiongezea nguvu Taasisi ya Benjamin Mkapa (Mkapa Foundation) katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ya Watanzania.
Alisema kuna changamoto nyingi nchini ambazo zimekuwa zikijitokeza na ili kukabiliana nazo zinahitajika taasisi kama ya Benjamin Mkapa ili ziweze kusaidiana na Serikali na ili waweze kutatua changamoto hizo zinahitajika sekta binafsi kusaidiana nao kukabili changamoto hizo.
“Nimekuwa mstari wa mbele kusaidia sehemu ambazo zinaonekana kuwa na mahitaji na changamoto nchini zipo nyingi haina jinsi inabidi kushirikiana ili kupambana na changamoto hizo,” alisema Dewji.
Aidha Rais na Mkurugenzi Mkuu huyo wa MeTL Group aliyataka mashirika binafsi mengine kuungana kwa pamoja na kusaidia kumaliza changamoto zilizopo nchini kwani anaamini kuwa wana nafasi kubwa kukabiliana na matatizo hayo na kuweza kuyamaliza.
Nae mwanzilishi wa Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation), Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa alimshukuru Mohammed Dewji kwa msaada ambao amewapatia na anaamini ni mmoja wa watu wa kuigwa nchini kutokana na misaada ambayo amekuwa akiitoa nchini kwa kupitia taasisi yake ya Mohammed Dewji (Mo Dewji Foundation).
“Mohammed Dewji ni mfano wa kuigwa nchini na ameweza kuboresha biashara ya Tanzania kimataifa, ninaamini utadumu kwa kipindi kirefu zaidi na kuwa balozi mzuri wa Tanzania,” alisema Mkapa.
Katika sherehe hizo za kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, kulifanyika harambee ambapo jumla ya Bilioni moja na Milioni mia moja na sabini zilichangishwa.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni