Kulia ya Balozi Seif ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Bibi Aziza Ramadhan Mapuri na Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani Nd. Abdulla Shunda.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati za Siasa za Wilaya za Dimani, Mfenesini na Mkoa wa Magharibi wakifuatilia hotuba ya Mjumbe wa Kamat Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama Balozi Seif.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa inayowakabili Viongozi na Wanachama wa CCM kwa wakati huu ni kuzifanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita ili kazi iwe rahisi wakati chama hicho kitapoingia kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Alisema mambo yote yanayopaswa kufanywa ili kujenga mazingira bora zaidi ya ushindi ni lazima yakatekelezwa ndani ya kipindi hichi cha miaka minne iliyoanza hivi sasa.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za Wilaya ya Dimani, Mfenesini pamoja na Mkoa wa Magharibi katika kikao cha kuwapongeza kufuatia ushindi wa kishindo uliopata Mkoa huo katika nafasi za Ubunge,Uwakilishi na Udiwani mkutano uliofanyika kwenye Tawi la CCM Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema wakati huu ni wa kurekebisha na kujenga nyumba ya ushindi wa mwaka 2020 na kusisitiza uzikwaji wa makundi yote yaliyojichomoza ndani ya chama na kupelekea wakati mgumu wa kujenga nguvu za ushindi kwenye Uchaguzi kwa baadhi ya Majimbo na Wadi.
Balozi Seif alieleza kwamba wapo baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi hasa Vijana waliodharau kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba na hata ule wa marejeo na kusababisha upunguzaji wa kura za chama hicho katika baadhi ya Majimbo na kusababisha ushindi hafifu kwenye Majimbo hayo.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwakumbusha Viongozi wa Kamati za Siasa akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama kuhakikisha wanawaelimisha Vijana wao umuhimu wa kujua thamani ya kura katika muelekeo wa kukijengea mazingira bora ya uwajibikaji Chama chao.
Hata hivyo Balozi Seif aliwashukuru na kuwapongeza Viongozi hao wa Kamati za Siasa za Mkoa wa Magharibi na Wilaya zake kwa kazi ngumu waliyoifanya katika kukipatia ushindi chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa marejeo uliofanyika Tarehe 20 Machi mwaka 2016.
Balozi Seif alisema katika uchaguzi huo wa marejeo Chama cha Mapinduzi kilifanya vyema baada ya kujirekebisha kutokana na kasoro na changamoto mbali mbali zilizowahi kujichomoza kwenye uchaguzi wa Mwezi Oktoba mwaka 2015 ambapo kasoro hizo zilipelekea Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi na matokeo yake yote.
“ Nimepata faraja kubwa kama mimi ni mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama kutokana na ushindi mliopata kwenye Majimbo na Wadi zenu licha ya kupoteza Jimbo moja kwa upande wa Ubunge ”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2015 ulikumbwa na changamoto nyingi lakini zilipata ufumbuzi kufuatia mshikamano mkubwa uliopo baina ya Viongozi na wanachama wao Matawini na Majimboni.
Aliwataka Viongozi na Wanachama wa Mkoa na Wilaya hizo kutokubali kubweteka au kulemaa kwa ushindi walioupata na badala yake wajipange vizuri zaidi ili kazi ya kukipatia fursa chama chao kuendelea kuongoza Dola iwe rahisi wakati utakapowadia.
Akizungumzia ahadi zilizotolewa na viongozi wa juu wakati wa kampeni za uchaguzi Balozi Seif aliwaomba Viongozi wa Wilaya na Mikoa kuziratibu ahadi zote ili kuwapa faraja Wananchi waondokane na mawazo ya kupewa ahadi hewa zisizotekelezeka.
Alisema Chama cha Mapinduzi kinakusudia kuingia kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kikiwa hakina dhima ya ahadi zilizobakia katika utekelezaji unaotarajiwa kufanyika ndani ya kipindi hichi cha miaka minne iliyobakia.
Balozi Seif aliwakumbusha Viongozi walioteuliwa Majimboni na Kwenye Wadi kutumia lugha ya kiungwana wakati wa kuwahudumia wananchi wao ili ile kiu ya matarajio yao waliyoionyesha kwa kumchaguwa kuwaongoza ipate kukamilika.
Alionya kwamba tayari wapo baadhi ya Viongozi waliochaguliwa na wananchi wameshaanza tabia ya kuzima au kutopokea simu kutoka kwa wananchi wao kwa visingizio vya kuweko kwenye vikao au Mikutano nyeti.
Alisema huo ni mwanzo mbaya unaokaribisha kuanza kwa tabia ya kupikiana majungu, vikundi na fitina ambapo mambo yote hayo kwa sasa wakati wake umekwishwa mara tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Bibi Aziza Ramadhan Mapuri alisema uchaguzi wa marejeo katika mkoa huo umefanyika kwa mafanikio makubwa yaliyotokana na mshikano uliowekwa kati ya Viongozi na Wanachama wao.
Bibi Aziza alisema Majimbo 13 kwa nafasi za Uwakilishi na wadi 26 kwa nafasi za Udiwani zimechukuliwa na wagombea wa Chama cha Mapinduzi ukitoa Jimbo la Mwanakwerekwe kwa upande wa Ubunge lililochukuliwa na chama cha Upinzani.
Wakichanga kwenye kikao hicho cha kupongezana baadhi ya wajumbe wa Kamati za Siasa za Mkoa wa Magharibi na Wilaya zake mbili waliuomba Uongozi wa juu wa chama pamoja na Serikali kutowaonea haya watu wenye sura mbili katika utekelezaji wa dhamana zao makazini.
Walisema jamii imekuwa ikishuhudia hujuma nyingi zinazofanywa na baadhi ya watendaji hasa Serikalini wakati wanapotekeleza majukumu yao bila ya hata kukemewa wala kuchukuliwa hatua za kisheria jambo ambalo linaondosha imani kwa wale walio chini yao.
Othman Khamis Ame
Ofisi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Ofisi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni