TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya
kupambana na rushwa duniani ni kiashiria tosha kwamba tatizo la
rushwa ni kubwa sana na linataka juhudi za pamoja katika kukabiliana
nalo. (It’s a serious graft that needs concerted efforts).
Ametoa
kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Waziri wa Nchi wa
Uingereza anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Bibi Justine
Greening walipokutana kwenye mkutano huo uliofanyika Lancaster House,
jijini
London, Uingereza.
Waziri
Mkuu ambaye alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe
Magufuli, alimweleza Bibi Greening kwamba viongozi wa Serikali wa
awamu ya tano wameamua kwa dhati kupambana na kila ovu linalotokana
na janga la rushwa na pia wameamua kuwajibika na kuachana na tabia ya
kufanya kazi kwa mazoea.
“Sasa
hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua kufanya
kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka utamaduni
mpya wa kupiga vita rushwa ili kuleta uwajibikaji na uwazi miongozi
mwa watu wetu,” alisema.
Alipoulizwa
ni kitu kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa katika vita
hii, Waziri Mkuu alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo manne ambayo
ni kuzuia rushwa isitolewe ama kupokelewa (prevention), kampeni za
kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya sheria na kuwepo kwa utashi wa
kisiasa.
“Serikali
inachukua hatua za kiutawala na kisheria kama vile kuanzisha mahakama
maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai mwaka
huu,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa
upande wake, Bibi Greening alipongeza hatua zinazochukuliwa na
Serikali ya awamu ya tano katika kupambana na rushwa na kwamba ndiyo
maana Tanzania ilipewa mwaliko maalum wa kushiriki mkutano huo kwa
vile baadhi ya mataifa yanaziona juhudi zinazofanywa na Serikali.
Pia
alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya
awamu ya tano imeionyesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza
viwanda.
Pia
alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia
Tanzania kwenye mpango wake ilionao wa kupeleka umeme vijijini (Rural
Electrification Programe). “Tuko tayari kuwasiidia kutekeleza
mpango huu kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata
ufadhili kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza
(DFID),” alisema.
Wakati
huohuo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia
masuala ya kimataifa, Bibi Sarah Sewall ameipongeza Tanzania kwa
kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na kusisitiza kwamba
makampuni mengi ya Marekani yana nia ya kuja kuwekeza Tanzania.
“Ninaamini
uwekezahji huu utasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa
watu wetu. Tunampongeza Rais Dk. Magufuli kwa juhudi anazofanya na
nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani
utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,” alisema.
Waziri
Mkuu alimshukuru Bibi Sewall na kumsisitiza asiache kusaidia
kuwahimiza wamarekani wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi
waje kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali zikiwemo uanzishaji wa
viwanda, uongezaji thamani kwenye mazao yanayozalishwa nchini na
kuhakiksha kuwa Watanzania wanajifunza teknolojia mpya na za kisasa.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI,
MEI 14, 2016.

Hakuna maoni :
Chapisha Maoni