.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 9 Juni 2016

BALOZI SEIF AKUTANA NA VIONGOZI WA ZAPSWU, ATAKA USHIRIKIANO WA KARIBU KATI YA VYAMA VYA WAFANYAKAZI NA TAASISI ZA UMMA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akibadilishana mawazo na Uongozi Mpya wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma { ZAPSWU } uliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } Bibi Mwatum Othman akimuelezea Balozi Seif hatua za kuunganishwa vyama vingi vya wafanyakazi na kupata kimoja chenye nguvu zaidi ya uwajibikaji.

Balozi Seif akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Zapswu uliojumuisha wajumbe wa Baraza Kuu pamoja na Kamati Tendaji ya Chama hicho. Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Nd.Ameir Mwadini Nahoda.

                                                                                                      Picha na – OMPR – ZNZ.

Ushirikiano wa karibu wa mara kwa mara baina ya Vyama vya Wafanyakazi na Viongozi wa Taasisi za Umma katika kutatua changamoto zinazowakabili Wafanyakazi hasa maslahi yao ndio njia pekee inayosaidia kuwafanya watekeleze kazi zao kwa juhudi, maarifa na nidhamu.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akibadilishana mawazo na Uongozi Mpya wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za huduma za Umma { ZAPSWU } uliofika kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo migogoro kadhaa inayowasumbuwa Wafanyakazi katika sekta tofauti Nchini na kuitanzua kwake ni kutafuta suluhu inayotoa fursa kwa kuwakutanisha wadau wote ili kupata njia ya kukabiliana na migogoro hiyo kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Akifafanua mgogoro wa muda mrefu uliowakumba wafanyakazi wa shamba la Mipira Kichwele dhidi ya mwekezji wa shamba hilo { Agro Tec } waliotaka kujua Viongozi hao wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Balozi Seif alisema Wizara ya Fedha na Uchumi ndio iliyopewa jukumu na Serikali Kuu kuangalia hatma ya suala hilo.

Balozi Seif alisema Wizara ya Fedha kwa sasa inaendelea kutafakari namna ya kuukwamua mradi huo kwa kutafuta mbinu nyengine za uwekezaji baada ya kampuni iliyokodishwa kuendesha mradi huo kushindwa kuliendeleza na kuwaacha wafanyakazi wake njia panda.

Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Zanzibar { ZAPSWU } Bibi Mwatum Othman alisema Chama hicho kipya ni mjumuisho wa vyama vya Wafanyakazi vitatu vya Raaw, Zadgu na Zipau.

Bibi Mwatumi alisema Viongozi na wanachama wa vyama hivyo wamefikia muwafaka wa kuwa na nguvu za pamoja za kuunganisha vyama hivyo ili kupunguza utitiri wa vyama uliokosa uwakilishi madhubuti.

Katibu Mkuu huyo wa Zapswu aliiomba Serikali kuu kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuangalia kwa kina Sheria ya utumishi wa Umma inayoelekeza Muajiri kumpatia Mkataba Mfanyakazi wakati anapoajiriwa kazi.


Bibi Mwatum alisema utaratibu unaotumika hivi sasa ni kwa muajiriwa kupewa Barua ya Ardhi-lhali kuthibitisha ajira yake inayotoa fursa pana kwa Muajiri kuchukuwa hatua dhidi ya mfanyakazi wake wakati inapotokea hitilafu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi huo wa Zapswu uliojumuisha Viongozi wa Baraza Kuu na Kamati Tendaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta za Huduma za Umma Nd.Ameir Mwadini Nahoda aliomba Uongozi wake kuendelea kupatiwa fursa kama hizo kwa lengo la kupunguza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wanaowasimamia.

Nd. Ameir alisema Mkutano huo umewapa faraja kubwa kiasi kwamba utafungua pazia jipya litakalotoa mwanga wa kufikia malengo na kupata ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuitumikia jamii.

Kampuni ya Agro Tec iliyopewa shamba la Mipira Kichwele hadi inaingia kwenye mgogoro wa ugemaji wa utomvu kwa ajili ya mipira ilikuwa ikikabiliwa na madeni ya zaidi ya shilingi Milioni 284,839,982/- ikiwa ni pamoja na Mishahara ya wafanyakazi wa mashamba ya Mipira Unguja na Pemba, fedha za Likizo pamoja na deni la ZSSF kwa wafanyakazi wake katika kipindi kati ya miezi Mitatu hadi Minane.

Utafiti wa Kitaalamu unaonyesha kwamba umri wa ugemaji wa Utomvu kwenye Mipira iliyooteshwa tokea mwaka 1977 umekwisha na kupindukia uzalishaji kiuchumi.

Bei ya bidhaa hiyo ya mipira katika soko la kimataifa pia imeshuka chini kiasi kwamba haiwezi kuongezeka tena sambamba na kukumbwa na ukosefu wa ushindani kwenye soko hilo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
09/06/2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni