Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ALI Iddi akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Mohammed Ali Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akipokea salamu za pongezi kutoka kwa Viongozi wa Jumuiya ya Wastaafu wa SMT waliofika Ofisini kwake kumpongeza baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuendelea kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif akizungumza na kubadilishana mawazo na Viongozi wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa miongoni mwa wanachama wa Jumuiya hiyo tokea mwaka 2011.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba baadhi ya Watumishi wa Taasisi za Umma bado wana hofu ya kuogopa kustaafu utumishi wao wakihisi kunyemelewa na ukali wa maisha ya baadaye wakisahau kwamba maisha baada ya kustaafu yapo kama kawaida.
Alisema cha msingi kwa mtumishi anayehusika ni kujipanga mapema katika kujiandaa na harakati za kujiendesha kimaisha bila ya kutetereka mara amalizapo utumishi wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati alizungumza na Uongozi wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoishi Zanzibar walipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumpongeza baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kuendelea kushika wadhifa aliokuwa nao.
Alisema ipo miradi mbali mbali nchini inayoweza kufanywa na wastaafu wa Taasisi za Umma katika kukidhi mahitaji yao ya kila siku badala ya kutumia ustaafu wao kuendeleza tabia ya kuomba wakati baadhi ya watumishi hao wana uwezo kamili wa kiafya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wastaafu hao wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka mikakati imara itakayosaidia kupambana na changamoto zinazowakabili ndani ya Jumuiya yao ili wapate mafanikio yatakayostawisha maisha yao.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nd. Mohammed Ali alisema wana Jumuiya hiyo wako tayari kushirikiana na Viongozi na Wananchi katika kuelekeza nguvu zao kwenye miradi ya kuendeleza Nchi.
Nd. Mohammed alisema kazi za kampeni ya uchaguzi Mkuu kwa Zanzibar tayari zimeshamalizika hadi mwaka mwengine wa 2020, na kinachostahiki kufanywa kwa wakati huu ni kuona jamii inajikita zaidi katika harakati za zao za maendeleo badala ya kusikiliza kasumba za wanasiasa walioishiwa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanajumiya hao Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Jumuiya hiyo bibi Teleza Olban Ali alimpongeza Mwanachama mwenzao wa Jumuiya hiyo Balozi Seif kwa kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kushika nafasi ya Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Bibi Tereza alisema Balozi Seif anastahiki kuendelea kuwa Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali kutokana na usimamizi wake mzuri ulioleta maendeleo makubwa ndani ya kipindi cha miaka Mitano iliyopita.
Alisema Wanajumuiya hiyo ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hawana wasi wasi nae kutokana na utumishi wake uliotukuka wa kuhudumia Wananchi katika kupunguza kero zinazowakabili.
Balozi Seif Ali Iddi amejiunga na Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Tarehe 16 Machi Mwaka 2011 akiwa mwanachama nambari 481 wa Jumuiya hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
08/06/2016.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni