Imeandaliwa na BMG
Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na idara ya Ustawi wa Jamii, metakiwa kuwaondoa watoto waliozagaa mitaani ambao wamekuwa wakiomba misaada kwa wasamaria wema barabarani.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza yamefanyika shule ya msingi Mabatini, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, amesema wengi wa watoto hao wameacha shule kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufiwa na wazazi ama wazazi kutokuwa na uwezo wa kuwaendeleza kimasomo, hivyo Halamshauri hiyo ina wajibu wa kuwasaidia.
Amesema hatua ya kuwaondoa watoto hao inaweza kuonekana ni ngumu kutekelezeka, lakini inawezekana ikiwa kila mdau ikiwemo jamii itatoa ushirikiano ambapo amewasihi madiwani katika baraza la halmashauri ya Jijini la Mwanza kupeleka hoja kwenye baraza lao ili jambo hilo liwekwe kwenye vipaumbele vya Halmashauri hiyo.
"Mkurugenzi, Meya na Madiwani wa halmashauri ya jiji la Mwanza, chukueni hatua kuwaondoa watoto waliozagaa mitaani ikiwemo mtaa wa Nkuruma kwani hawako pale kwa kupenda. Mkifanya hivyo itakuwa sifa kwenu na kwa baraza la madiwani la mwaka 205/20". Amesema Konisaga.
Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka June,16 ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya mamia ya watoto waliouawa na polisi wa kikaburu mwaka 1976 katika Kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini wakati walipokua wakiandamana kupinga kubaguliwa kielimu kwa kufundishwa katika lugha wasiyoifahamu ya Afrikana.
Katika risala yao, watoto wameiomba serikali pamoja na jamii kuwalinda na vitendo viovu ikiwemo ubakaji na ukatili unaowakumba ikiwemo kukosa elimu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni