Binti huyu mdogo ambaye analelewa na familia iliyomuasili kwa malezi (hajaasiliwa kisheria) ni miongoni mwa watoto kadhaa nchini ambao wanafaidika na mpango mpya wa kusaidia watoto waliokumbwa na ukatili na unyanyasaji.
Pretty (ambaye si jina lake la ukweli-nimempa jina hilo kulinda haki yake) maisha yake mpaka sasa ni kama kitendawili kibaya ambacho ni Mungu tu alitaka kukifumbua.
Nasema ni Mungu tu kwa kuwa Pretty aliokolewa kutoka katika shimo la choo alilotumbukizwa akiwa ndani ya mfuko wa rambo uliofungwa vyema.
Sajini taji (Staff Sergeant) Pundensiana Baitu wa Dawati la jinsia wilaya ya Kipolisi Mbalizi, anasema kwamba Pretty wakati alipoopolewa katika choo cha mtu binafsi alikuwa na hali mbaya sana kiafya na juhudi kubwa sana ilifanywa na hospitali ya Meta kumrejeshea afya yake.
Akisimulia tukio hilo la kuhudhunisha alisema kwamba usiku wa Machi Mosi, mwaka jana alipokea simu iliyomtafadhalisha msaada ili kuokoa maisha ya mtoto aliyetupwa katika choo kinachotumika, katika eneo la Mlimareli huko Mbalizi.
Alisema wakati anajaribu kuwasiliana na askari kwenda kuona kama wanahitaji msaada wa Kikosi cha zimamoto, akapokea simu nyingine kwamba wananchi wamebomoa choo hicho na kumtoa mtoto huyo ambaye alikuwa amefungwa katika mfuko wa rambo na kwamba alishaanza kuliwa na wadudu wa chooni.
Aidha aliambiwa katika simu kwamba mtoto huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa wiki moja alikuwa bado anapumua hali iliyomfanya aelekeze polisi kuitengeneza PF 3 haraka na kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya Ifisu ambao nao kutokana na kukosa vifaa vya watoto wa aina yake katika hali ile, walimkimbiza hospitali ya Meta.
Anasema yeye alifika asubuhi kuona hali ya mtoto huyo akiambatana na Ofisa Ustawi wa Jamii na hakupendezwa na hali aliyomkuta nayo mtoto.
Anasema kwamba juhudi za upelelezi kujua mama wa mtoto huyo hazikufanikiwa kwani mtoto alitupwa katika choo binafsi karibu na klabu ya pombe. Hata hivyo anasema baada ya kushindwa waliwaambia wananchi wa eneo hilo kumtazama mtu ambaye wanamtilia shaka na kumfikisha kwao kwa mahojiano.
Mpaka wakati wa kuandika makala haya mtu huyo hajapatikana.
Anasema kutokana na mfumo mpya wa familia ya mfano baada ya wao kama polisi kukamilisha kazi ya usalama na kumkabidhi mtoto huyo kwa Ofisa Ustawi wa Jamii, ofisa huyo alimtafuta mtu ambaye yuko tayari kulea mtoto na kumkakabidhi kwao.
Sajini taji huyo anasema kuwa kuna ongezeko la vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto na kwamba jamii inatakiwa kubadilika na kukubali wajibu wake katika kuhakikisha usalama wa mtoto.
Anasema kabla ya kuanzishwa kwa wilaya mpya wakati bado iko Mbeya amekuwa akishuhudia vurugu nyingi kuhusu ukatili kwa watoto na kwamba dawati lake inachofanya ni kutoa ushauri hasa kwa wadada ambao wanatoa mimba na wengine kutupa watoto wanapopatikana.
Alisema ingawa kuna taratibu ndefu za sheria, mfumo mpya uliokubaliwa na serikali wa kupata familia ya mfano ni mfumo bora wenye kuhakikisha malezi mema na kizazi bora kijacho.
Pretty ambaye kwa sasa anaishi na familia ya mfano yenye watoto sita na yeye akiwa wa saba katika kijiji cha Muvwa kilichopo kata ya Mshewe wilayani Mbalizi ana uhakika na malezi kutokana na mfumo huo mpya.
Na Si ajabu akikua hakuna mtu hata yeye mwenyewe atakayejua kwamba aliokolewa kutoka kwenye shimo la choo alikotupwa na mama katili wiki moja baada ya kuzaliwa kwake na kusaidiwa malezi yake na mfumo wa familia ya mfano.
Dk Sipora Harison Kisanga ambaye anafanyakazi na UNICEF kanda ya Iringa anasema kwamba ulinzi na usalama wa mtoto ni eda ya wananchi wote kwa ujumla, lakini kutokana na dosari zilizopo ndio maana UNICEF na Tanzania zimetia saini makubaliano yanayowezesha maandalizi ya watu wa kuwapokea watoto waliotelekezwa na wale wenye mazingira magumu ili nao waweze kuwa sehemu ya familia zilizobora.
Anasema kuufanya mfumo huo uwe na utekelezaji uliobora waliendesha mafunzo na kutambua watu wanaoweza kukaa na mtoto, na baada ya kuwakagua wapo katika orodha wakisubiri mtoto yeyote atakayepatikana.
Anasema kutokana na maandalizi hayo ndio maana hata walipompata mtoto Pretty walijua kwamba watampelaka Muvwa kwa familia ambayo iko tayari kupokea mtoto wa aina yoyote na wa umri wowote.
Anasema ni lengo la UNICEF kuhakikisha kwamba haki za watoto zinatekelezwa ikiwamo ya ulinzi na usalama dhidi ya vitu na watu wabaya, huduma za afya, huduma za elimu, haki ya kucheza na haki ya kufundishwa yaliyo mema kutoka kwa wakubwa wao.
Anasema Ofisa huyo wa UNICEF kwamba Mradi wa familia ya mfano ulianzia Temeke na sasa upo Mbeya, Mbarali, na Mbalizi kwa lengo lile lile kuwawezesha watoto hawa kuwa na familia na kuwa salama kuliko kuwapeleka katika vituo vya kulelea yatima.
Mama anayemtunza mtoto huyo pamoja na mumewe, Mama Christer Eliston Mwashusa anasema amefurahi sana kupata mtoto huyo kwani alikuwa tayari kumsaidia kutokana na hofu ya Mungu aliyonayo.
Anasema yeye angelifurahi kama mtoto angemuasili kisheria kwani hali ya sasa ya ulezi pekee anaiona kama haimpi nafasi ya kufanyakazi yake vyema ya kumtunza. Anataka awe mali yake moja kwa moja.
Anasema amepata changamoto nyingi tangu alipomkuta mtoto Pretty hospitali ya Meta, changamoto ambazo zilimuumiza kwanza kama mzazi kwa kutambua kwamba mtoto yule hana wazazi na pia kwa kutambua kwamba ametelekezwa kikatili.
Pia changamoto ambayo alikumbana nayo ni kule kutambua kwamba mtoto yule kwa sababu ya kuwekwa chooni alikuwa na dhiki kubwa ya afya na hivyo kumfanya kuwa dhaifu.
Anasema hata wakati alipoanza kumtunza changamoto za afya yake zilikuwa kubwa na hasa alipoambiwa kwamba ana ugonjwa ambao ameurithi kwa mama yake, ugonjwa ambao ni upungufu wa kinga na kuanza kumlisha dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kuanzia alipokuwa na miezi miwili hadi minne.
Hata hivyo katika mahojiano na Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka hospitali ya kanda ya rufaa Mbeya (Meta) aliyempokea mtoto huyo Gerald Godfrey Mwambesi alisema kwamba Pretty hakuwa na virusi tangu awali walipompima na kusema kwamba hata vipimo vya hospitali nyingine vilivyosema kwamba ana virusi havikuwa sahihi.
Anasema Pretty alipoteza nguvu ya kinga ya mwili kutokana na kukaa chooni kwa muda na hivyo siku zilivyozidi ndivyo alivyokuwa akiongeza kinga.
Anasema baada ya siku tatu ya kukabiliana na vidonda vyake vilivyotokana na kutafunwa na wadudu chooni na baada ya wiki tatu alionekana kuwa nafuu sana na ingawa mlezi alipata changamoto kiukweli mtoto huyo hakuwa na virusi zaidi ya kupoteza kinga za kawaida ambazo zilitakiwa kurudishwa taratibu.
Anasema mtaalamu huyo kwamba waliongea na wataalamu wa watoto kuhusiana na shida hiyo ya hospitali Mbalizi kumuona mtoto na virusi wakati wao walimpima mara mbili bila kuviona na kusema kwamba hali hiyo inatokana na maambukizi yaliyosababishwa na kutupwa ndani ya choo ambayo yalihitaji tiba ya muda mrefu.
Mlezi anasema kwamba baada ya miezi miwili ya kukaa na mtoto huyo kwa uzuri aliona afya yake inadorora kiasi cha kuhitaji msaada wa tiba na kuanza kwenda hospitali kupata msaada.
Anasema hospitali aliyoenda ilisema mtoto ana maambukizi kutoka kwa mama na kushauri tiba hivyo alipelekwa katika kiliniki ya Beira ambako walimpima na kumwanzishia dozi waliyokuja kuikatisha baada ya kumpima tena kutokana na ufuatiliaji wa hospitali ya Meta na kugundua kwamba hana tatizo la maambukizi ya UKIMWI.
Mlezi wa mtoto huyo alishukuru sana watendaji wa taasisi ya Kihumbe ambao walimsaidia fedha za nauli kwenda katika hospitali kutetea afya ya Pretty na kwamba baada ya matumizi ya dawa na dawa lishe mtoto huyo mwezi uliopita (Juni 16,2016) aliambiwa kwamba mtoto wake hana maambukizi tena.
KIHUMBE, ni taasisi inayofundisha wawezeshaji namna ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hasa familia zao ili waweze kujimudu wenyewe na kuondokana na matatizo hayo.
Baba mlezi katika familia hiyo yenye watu saba akiwamo Pretty, Juma Mbuza amesifu juhudi za mke wake katika kuhakikisha kwamba Pretty anapata mapenzi yote ya kimama na kuendelea kustawi akiwa katika familia hiyo.
Anasema familia yake inawiwa.kulea mtoto huyo kwa kuwa ndiyo ilikuwa nia yao tangu awali na kwamba awali walitaka kuwachukua watoto waliotelekezwa katika kijiji jirani kwenye tarafa yao.
Mlezi huyo alifurahishwa sana na mpango wa familia ya mfano ambapo inawezesha watu kupata upendo wa kweli.
Kauli imeungwa mkono Ofisa Ustawi wa Jamii Gerald Mwaulesi ambaye alisema kwamba mahusiano ya moja kwa moja yasiyokuwa na unyanyapaa hupatikana zaidi katika familia na kwamba familia za mfano ndizo zinazoweza kulea watoto hao waliotelekezwa.
Anasema nyumba za kulea yatima mara nyingi haziwezeshi upendo na malezi ya karibu yenye staha na mara nyingi hutoa watoto wakorofi au wenye katabia kenye walakini katika jamii.
Mfumo wa familia ya mfano ambao kwa sasa upo katika majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja mkoani Mbeya umekabidhi watoto wanane kwa familia katika Jiji la Mbeya, Mbalizi na Mbozi.
Katika mfumo huu UNICEF inasaidia serikali ya Tanzania kuona namna bora ya kutunza watoto wa kwenye mazingira magumu, wanaonyanyaswa na wale ambao wanatelekezwa unawezeshwa kwa mujibu wa sheria.
Mfumo huu ambao ulianzia Wilaya ya Temeke na kisha kupelekwa Mbeya katika wilaya ya Mbalizi, Mbozi na Jiji la Mbeya unatarajiwa kufikishwa katika halmashauri zote ili kutoa nafasi ya malezi ya jamii kwa watoto waliokumbwa na maswahibu mbalimbali.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatoa nafasi kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kuwapeleka watoto katika uangalizi wa familia ya mfano kama njia ya kurekebisha na kuwapatia nafasi watoto ya kuishi kama watoto wengine.
Katika hili serikali kupitia taasisi zake hutambua familia za mfano baada ya kuzichunguza huwakabidhi watoto hao kwa malezi ya muda.
Familia za mfano zinatarajiwa kulea watoto ambao wanakosa malezi na maelekezo kutokana na mikanganyiko inayoendelea kutokea katika familia mbalimbali na hasa wazazi kutengana au migogoro mingine.
Lengo lake ni kumpa mtoto upendo ambao utamchagiza kutambua maana ya ustaarabu na maisha kwa mwanadamu katika familia iliyozungukwa na upendo na badala ya kuwekwa katika taasisi ambazo zinaweza kumharibu zaidi.
Watu wa UNICEF wanasema kwamba baada ya mafanikio katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa familia ya mfano katika wilaya ya Temeke mwaka 2014 halmashauri nyingine 14 zilifanyiwa majaribio ikiwamo Mbeya mwaka jana.
Kwa sasa nchini kuna watoto 80 ambao wamenufaika na familia ya mfano wakiwemo watoto 10 mkoani Mbeya.
Mfumo huu mpya ulianzishwa kutokana na utafiti uliofanywa na serikali mwaka 2009 wakisaidiwa na UNICEF.
Katika utafiti huo uliokuwa ukiangalia ukatili kwa watoto (wasichana kwa wavulana) matokeo yalionesha kwamba asilimia 70 ya watoto walikumbana na ukatili wa aina mbalimbali katika miili yao; asilimia 30 ya wasichana walielezea kunyanyaswa kimapenzi kabla ya miaka 18 na wasichana wa miaka 13 hadi 17 walikuwa wajawazito na wasichana 7 kati ya 49 walisema mimba zao zinatokana na kubakwa au kushawishi kilaghai.
Kuna mambo mengine mengi ambayo yanaweza kuzungumzwa katika hilo ikiwamo masuala ya ukeketaji na ndoa za utotoni.
Kukiwa na shida kwa sasa katika sheria za Tanzania kuhusiana na hakijinai uwapo wa mfumo wa aina hii ni neema sana kwa taifa na kwa malezi bora ya watoto.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni