.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 7 Julai 2016

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU- (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU) MHE. JENISTA MHAGAMA (MB.) KWENYE HAFLA FUPI YA UZINDUZI WA BODI MPYA YA SHIRIKA LA TAIFA LA HIFADHI YA JAMII (NSSF) KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WAZIRI MKUU, TAREHE 5 JULAI, 2016

· Mhe. Anthony Mavunde (Mb.), NW –OWM (KVA)

· Mhe. Abdallah Possi (Mb.), NW –OWM (U)

· Bwana Eric Shitindi - Katibu Mkuu –OWM (KAVAU)

· Bibi Irene Isaka, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA;

· Prof. Samwel Mwita Wangwe, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF;

· Ndugu Nicholaus Mgaya – Katibu Mkuu, Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);

· Dkt. Aggrey Mulimuka – Mkurugenzi Mtendaji, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);

· Ndugu Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF;

· Prof. Godius Kahyarara, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF;

· Ndugu Kaali Nicodemus – Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii OWM –KVAU;

· Waandishi wa Habari;

· Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana.

Habari za mchana !!

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima, afya njema na kutuwezesha sote kukutana hapa mchana huu na kwa wale waliofunga nawatakia mfungo mwema na Ramadhan Kareem. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kushiriki nasi leo kwenye hafla hii fupi lakini muhimu ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mabibi na Mabwana,

Nianze kwa kukupongeza sana Profesa Samwel Mwita Wangwe kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Historian a utendaji wako wa kazi, mapenzi yako kwa nchi yetu na watu wake ni kielelezo tosha kuwa wewe ndio chaguo sahihi kwa wakati huu tulionao, kulilea na kuliongoza Shirika la NSSF kupitia Bodi yako ya Wadhamini ya Shirika la NSSF. Unastahili, tunajivunia na ninakupongeza sana.

Napenda vilevile kwa dhati ya moyo wangu, kuwapongeza wajumbe wote wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii kwa kuteuliwa kubeba jukumu hili muhimu la Bodi. Bodi ndiyo chombo cha juu cha maamuzi kuhusu Mfuko ambapo utekelezaji wa siku hata siku umekasimiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ambaye pia ni Katibu wa Bodi. Nawashukuru kwa kukubali uteuzi wangu. Ninayo Imani kubwa sana na Bodi hii kwa sababu ninaelewa uwezo, uzoefu na umahiri wenu kwa matarajio kwamba mtatuvusha hapa tulipo.

Mabibi na Mabwana,

Shirika la Taifa la Hifadhi YA Jamii ni moja kati ya mashirika makubwa na muhimu katika nchi yetu. Ninaamini kwa dhati kuwa uteuzi wenu umefanyika kwa kukidhi vigezo vya sifa na uzoefu wenu binafsi pamoja na kuzingatia kikamilifu matakwa ya Sheria ya NSSF ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA No. 5) ya mwaka 2012. Kwa msingi huu, ninaamini ninyi mnatosha kabisa kulipa Shirika letu la NSSF uongozi madhubuti utakaofanya kazi zake kwa viwango vinavyoendana na kauli mbiu ya “HAPA KAZI TU!”

Ndugu Mwenyekiti,

Vilevile, nitumie nafasi hii, kuipongeza sana Bodi ya Wadhamaini ya NSSF ambayo ilimaliza muda wake tangu Februari, 2016. Bodi hiyo imefanya mambo mengi mazuri na jambo kubwa moja wapo litakalokumbukwa na wengi ni ilivyowezesha kusimamia ujenzi wa daraja la Mwalimu Julius Nyerere au maarufu kama “Daraja la Kigamboni”

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Jukumu langu la msingi siku ya leo ni kuzindua Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hata hivyo, kabla sijatekeleza jukumu hilo naomba nitumie fursa hii kuzungumza machache kuhusu majukumu ya Bodi ya Wadhamini kama inavyoelekezwa na Sheria ya NSSF sehemu ya sita ya Sheria ya NSSF Na.28 ya mwaka 1997.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu yanayotajwa kwenye sehemu hii ya Sheria hamna budi kuliongoza Shirika kwa kuzingatia Misingi ya Utawala Bora, Ushirikiano, Nidhamu, Uadilifu na Weredi wa hali ya juu. Uongozi wenu ndiyo utakaowezesha NSSF kukidhi matarajio ya Wanachama wa Mfuko na Wadau kwa ujumla. Matarajio ya Wanachama na Sisi Wadau ni kuona Mfuko unakuwa imara, endelevu na unaotoa huduma bora za h mafao ya ifadhi ya jamii kwa Wanachama wake.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Pamoja na mafanikio mbalimbali yanayopatikana Nchini katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Changamoto kubwa zinazoikabili Sekta hii ni zifuatazo:-

(i) Namna ya kuongeza idadi kubwa ya Watanzania wengi katika Sekta Rasmi na isiyo rasmi kushiriki kwenye Mfumo wa Hifadhi ya Jamii.

(ii) Namna ya kuendelea kuboresha mafao ya Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili yaendane na hali ya uchumi; na

(iii) Namna ya kuwekeza michango ya Wanachama kwenye maeneo yenye tija zaidi na kwa ufanisi.

Hivyo, ni matarajio yangu kwamba katika uongozi wenu mtachukua hatua na kuweka mikakati bora itakayowezesha NSSF kuchangia katika kutatua changamoto hizo.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Pamoja na changamoto nilizoziainisha hapa juu, nipende kusema kwamba Sekta ya Hifadhi ya Jamii ni Sekta muhimu sana katika kuchangia ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato kwa watu hapa nchini. Sekta hii ina fursa kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu katika maeneo mbalimbali. Wote mnafahamu namna Sekta hii katika miaka ya karibuni ilivyowekeza katika Elimu, Afya, Kilimo na hata Majengo mbalimbali nchini. Hivyo, ni muhimu sana kuendelea kuitumia fursa hii katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.



Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Uteuzi wenu umefanyika wakati Serikali ya Awamu ya Tano imeaanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2021/22) ambao utekelezaji wake umelenga kuiwezesha nchi yetu kujenga Uchumi wa Viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo wamaka 2025. Dhamira ya kuifanya nchi yetu kuwa ni ya Uchumi wa Viwanda ni Sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo Mhe. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na amedhamiria kuitekeleza kwa vitendo katika kipindi chake cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Kuna masuala kadhaa yanayohitaji kufanyiwa kazi ikiwemo suala la ufuatiliaji wa Madeni sugu. Nina taarifa kwamba Shirika linadai zaidi ya Trilioni moja kwa Serikali ijapokuwa imefikiwa hatua nzuri kwamba Serikali imeamua kubadilisha deni kwenda kwenye hati fungani yaani Non Cash treasury bond yenye thamani ya Shilingi Bilioni 520. Naamini kwa pamoja tutasaidiana kkulisukuma jambo hili. Pamoja na madeni hayo, vilevile yapo madeni ya Wazabuni, Makampuni na Watu binafsi wanaoidai NSSF ambao hawajalipwa hadi sasa, hivyo dhahiri tunaona ni kwa kiasi gani kazi kubwa iliyopo mbele yetu.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Katika kuhakikisha kwamba hata Taasisi za Umma zinashiriki katika kujenga Uchumi wa Viwanda, hivi karibuni Mheshimiwa Rais alielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini itumie rasilimali zake katika kuiwezesha nchi kujenga Uchumi wa Viwanda kama kitega uchumi badala ya kuwekeza kwenye maeneo ambayo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikishindwa kurudisha fedha ilizowekeza hususan majengo.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Katika kuitikia maelekezo ya Mheshimiwa Rais ninafahamu kwamba chini ya Uratibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji NSSF pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi za Umma tayari zimekwisha shiriki katika kutambua maeneo yenye fursa ya kuwekeza viwanda kama Sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Napenda kuwataarifu kwamba tayari Menejimenti ya NSSF imekwisha chukua hatua ya kubainisha maeneo ambayo yana fursa nzuri kuwekeza viwanda na hivyo kuliwezesha Shirika la NSSF kupata faida na hata kuchangia katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya Taifa wa kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Eneo la kwanza lililobainishwa ni NSSF kuwekeza na kusaidia kufufua vinu vya NMC chini ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Vinu hivyo ni vile vilivyopo katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Dodoma, Arusha na Mwanza. Kiwanda cha Iringa kipo katika hatua ya juu ya utekelezaji. Bodi ya Mazao mchanganyiko tayari imewekeza takriban shilingi bilioni moja. Kinachovutia katika Mradi huu ni ukweli kuwa biashara hii ni ya kuchakata na kuuza unga wa dona unaotokana na mahindi yanayolimwa na Watanzania wenzetu katika Mikoa ya Kusini. Takriban tani 60 za unga wa dona zinauzwa kila siku sokoni ambapo mahitaji bado yapo na NMC hawajapata hasara yoyote katika biashara hiyo hadi sasa. Aidha, kiasi cha wakulima 300 wanashiriki katika kilimo hicho cha mahindi, wakulima ambao wako tayari kujiunga na NSSF kama wanachama wapya. Aidha, hatua hii itasaidia sana kukuza viwanda, na kilimo na inatarajiwa idadi ya wakulima wanaoshirki katika mradi huu itaongezeka kutoka wakulima 3,500 wa sasa hadi kufikia wakulima 10,000.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Katika kusaidia kuongeza vinu kwa NMC, shirika liitumie Benki ya Azania kutoa na kusimamia mikopo kwa NMC. NMC watafungua akaunti katika benki hiyo na hivyo kuzidi kuiimarisha benki hiyo na kuleta manufaa kwa uwekezaji wa Shirika katika Benki hiyo ya Azania. Itakumbukwa kuwa NSSF ni mmoja wa wanahisa wakubwa katika Benki ya Azania na hivyo hatua hii itaiwezesha Benki ya Azania kuimarika Zaidi.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Eneo jingine la uwekezaji linahusu NSSF kusaidia kutengeneza kinu cha alizeti cha NMC kilichopo Dodoma ili kiweze kuzalisha mafuta ya alizeti. Tafiti zinaonesha kuwa zao la alizeti linalimwa sehemu nyingi za nchi yetu. Hivyo, kwa kushirikisha viwanda vya kuchakata mafuta ya alizeti, zipo faida nyingi zitakazopatikana kwa Shirika na Taifa kwa ujumla. Viwanda hivi vitazalisha mafuta ya alizeti yenye ubora, yasiyochangaywa na kemikali hatarishi kwa afya za binaadamu, lakini pia vitakuza kilimo cha zao hili na kuchangia kuondoa umasikini. Kama ilivyo kwa zao la mahindi kule Iringa, kilimo cha alizeti pia kitakuza wigo wa wanachama wa NSSF na hivyo kuongeza makusanyo ya michango ya wanachama wa Shirika.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Uwekezaji mwingine unaotarajiwa kufanywa na Shirika ni uwezekaji katika kiwanda cha kuzalisha sukari. Shirika la NSSF pamoja na mfuko wa hifadhi wa NSSF tayari wamepewa maelekezo ya kuwekeza kwenye kiwanda cha Sukari huko Bonde la Mkurazi lililopo Mikoa ya pwani na Morogoro. Mradi huu ni mmoja wa miradi ya kimkakati katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka mitano. 


Wataalamu wanasema kuwa kiwango cha utumiaji wa sukari kina uhusiano wa moja kwa moja na hatua ya ukuaji wa uchumi wa nchi husika. Hivyo, wakati Tanzania inapoazimia kukuza uchumi wake kuwa uchumi wa kiwango cha kati, hatuna budi kama Taifa kuongeza uzalishaji wa sukari. Nimetaarifiwa kwamba, zipo Benki nyingi nchini ambazo zimeonyesha utayari wakushirikiana na NSSF katika uwekezaji husika. Mradi huu unatarajiwa kutoa fursa kwa wakulima na yapo mazao mengine mengi yenye soko yanayoweza kuzalishwa katika Bonde hilo pamoja na uzalishajiwa nishati.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Napenda nitumie nafasi hii kukuelekeza wewe Mwenyekiti pamoja na Bodi wa Wadhamini ya NSSF kuhakikisha mnasimamia kwa mafanikio utekelezaji wa maeneo niliyoyataja ya fursa za uwekezaji ambazo tayari zimebainishwa. Aidha, muendelee kubainisha maeneo mengine ambayo yanafaa kuwekeza na hivyo kuchangia katika azma ya Serikali ya kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa viwanda na kupanua wigo wa wanachama katika Mfuko.

Pia ni muhimu tuwekeze katika viwanda ambavyo vinavyotumia malighafi za ndani na vinavyozalisha fursa nyingi za ajira (Labour intensive). Mtakapotekeleza hayo, kama Mfuko mtakuwa mmetengeneza vyanzo vipya vya kupata wanachama wapya ambao watachangia katika makusanyo ya michango. Kwa utaratibu huu, watanzania wengi watapata ajira pamoja na mafao ya hifadhi ya jamii na hivyo kuharakisha maendeleo ya Taifa.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Mbali na masuala ya Viwanda, mnapoanza majukumu yenu yapo mambo mengi muhimu ya Shirika yanayosubiri maamuzi ya Bodi ya Wadhamini kwa faida na ustawi wa Shirika la NSSF, maslahi ya wanachama na umma kwa ujumla. Zipo Taarifa za Ukaguzi, zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Benki Kuu na Mkaguzi wa Hesabu za Ndani ambazo

mapendekezo yake yanasubiri uamuzi wa Bodi. Taarifa hizi zimebainisha mambo mengi mabaya ya ukiukwaji wa Sheria mbali mbali za nchi ambao umefanywa ndani ya NSSF na kupendekeza hatua za kuchukua. Ukiukwaji huo wa Sheria za nchi ulipelekea hata Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa maelekezo ya kufanyiwa kazi kutokana pia na taarifa ya ukaguzi ya CAG.

Hivyo kwa mujibu wa Mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 60 cha Sheria ya Taifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii namba 28 ya mwaka 1997, kikisomwa pamoja na Sheria ya marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii kama yalivyofanyika mwaka 2012. Napenda kuielekeza Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuchukua hatua stahiki mapema iwezekanavyo. Sitarajii Bodi ya Wadhamini itapoteza muda kwa kuanzisha michakato ya uchunguzi isipokuwa kuchukua hatua na hata kuwachukulia hatua wale wote waliobainika kushiriki katika ukiukwaji wa Sheria mbalimbali za nchi. Maelekezo ya Ofisi yangu nitakupatia Mwenyeketi kwa ajili ya utekelezaji wa Bodi ya wadhamini.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi,

Pamoja na yote hayo, suala la uwekezaji na utekelezaji wa mipango yote niliyoieleza hapo awali haiwezi kukamilika endapo Shirika halitaweka mkazo na msimamo katika makusanyo ya michango kutoka kwa wanachama. Nina taarifa kwamba kuna baadhi ya Makampuni ya Kimataifa yanadanganya na kukwepa kulipa michango stahiki ya wanachama kwa kutoa hati za malipo kwa aina mbili yaani kwa shilingi na dola, lakini kile kinachokatwa na kuwasilishwa kwenye Mfuko ni kile kinachotokana na malipo ya shilingi ambacho ni kidogo kuliko kile kiwango cha dola. Hatuna budi kuchukua hatua ili kulipatia tiba suala hili mapema iwezekanavyo. Bodi hakikisheni mnaisukuma Menejimenti ikusanye michango kutoka kwa waajiri na wanachama. Uhai wa mfuko ni michango ya wananchama.

Pamoja na hilo, hakikisheni Shirika linatumia Rasilimali zake ipasavyo. Ninafahamu kwamba kuna baadhi ya Majengo binafsi yamekodiwa na kupangishwa kwa Shirika, ni vema tukatumia majengo ya Shirika na pale inapobidi basi tutumie majengo ya umma ambayo gharama zake ni nafuu tofauti nay ale ya binafsi.

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi

Nihitimishe hotuba yangu kwa kuwatakia kazi njema katika majukumu yenu mapya. Napenda kuwahakikishia ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwangu, Ofisi yangu na Serikali kwa ujumla ili kuwawezesha kutimiza wajibu wenu kwa ufanisi wa hali ya juu.

Baada ya kusema hayo, napenda kwa heshima na taadhima nitamke kuwa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imezinduliwa rasmi!

Asanteni sana!

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni