Baada ya kuwatoa Shelisheli kwa
jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa , timu ya
soka ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’,
imebakiza mitihani miwili kabla ya kuandika historia ya kufuzu
kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, imefahamika.
Mtihani wa kwanza ni mchezo dhidi ya
Afrika Kusini unaotarajiwa kufanyika ama Agosti 5, 6 au 7, 2016
ambako mechi ya kwanza itapigwa ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar
es Salaam, Tanzania wiki moja baada ya mchezo huo. Hivyo mchezo wa
marudiano utafanyika Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamzi Agosti 14,
2016 saa 9.00 alasiri.
Mshindi wa jumla katika michezo
hiyo, itacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.
Wakati Afrika Kusini imepitishwa moja kwa moja Namibia imepenya kwa
kuiondoa Botswana licha ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wake
uliofanyika jana Julai 2, 2016 huko Botswana.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika
Namibia, Juni 24, mwaka huu wenyeji (Namibia) walishinda 1-0. Kwa
msingi huo, Namibia imepenya kwa bao la ugenini ililolivuna katika
mchezo wa jana. Bao la ugenini imefanya kuwa na mabao 3-2.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari
Nyundo Shime, ameangalia ratiba ya mlolongo huo na kusema “Ushindani
utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga kushinda michezo yote iliyo
mbele yangu. Si kwamba napigania kufuzu kwenda Madagascar tu kwenye
fainali za Afrika, la hasha, nataka timu hii niipeleke Kombe la
Dunia.”
Fainali za Kombe la Dunia, mwakani
zitapigwa India ambako kama Serengeti Boys itafuzu kucheza fainali za
Afrika na ikaingia nusu fainali kwa maana timu nne bora zote
zitashiriki fainali hizo ambazo tayari Tanzania imejiwekea mazingira
mazuri ya kufuzu.
“Timu hii nimeanza nayo zaidi ya
mwaka mmoja. Sioni kama itakuwa kikwazo kuifanikisha kufika fainali
za Kombe la Dunia. Namuomba Mungu atunyooshee mkono wake, nawaombea
viongozi wa TFF wazidi kuihudumia timu hii, lakini pia wadau wengine
waisapoti timu hii bila kuangalia au kuchagua mtu anayeongoza TFF.
Hii ni timu ya Watanzania wote,” amesema Shime maarufu kama Mchawi
Mweusi.
Shime alishukuru mipango na ahadi ya
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
kugharamia kambi ya wiki mbili itakayofanyika Madagascar kuanzia
Julai 24, mwaka huu akisema: “Hii itakuwa ni kambi bora. Kwa sasa
kikosi change kinahitaji utulivu hivyo kwa maoni na mipango yangu
naona inafaa.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira
wa Miguu kwa Vijana anayeongoza timu hiyo, Ayoub Nyenzi kadhalika
aliomba sapoti ya Watanzania ili kuendeleza timu hiyo, amesema:
“Hakika nikipata watu wakatusapoti, naamini ndoto zangu zitatimia
.”
Nyenzi amethibitisha kwamba timu
hiyo itaondoka hapa jijini Victoria kesho Jumatatu Julai 4, 2016 saa
11.00 jioni Kisiwa cha Mahe miongoni mwa visiwa 115 vya nchi hii ya
Shelisheli na inatarajiwa kufika Tanzania saa 7.45 usiku wa kuamkia
Jumanne Julai 5, mwaka huu.
“Wachezaji watakuwa na mapumziko
mafupi kabla ya kuanza kambi ya maandalizi kwenda Madagascar kwenye
kambi ya kuiandaa timu kucheza na Afrika Kusini,” amesema Nyenzi
ambaye pia alijibu kuwa watawapumisha nyota hao kwa ushauri wa
makocha na daktari: “Mapumziko mafupi. Msihofu”
Timu hiyo yenye wachezaji 20 na
viongozi wanane, itasafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia
hadi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa, Ethiopia
kabla ya kubadili ndege ya kuunganisha kwenda Dar es Salaam,
Tanzania. Ikiwa Shelisheli ilifikia hoteli ya Berjaya Beau Vallon
Resort, iliyoko jijini Victoria. Hoteli ipo umbali wa Kilometa 25
kutoka uwanja wa ndege.
Nyota waliosafiri ni pamoja na
makipa, Ramadhani Awm Kabwili na Samwel Edward Brazio wakati mabeki
wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick
Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba.
Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally
Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa,
Ibrahim Abdallah Ali, Yassin Muhidini Mohamed, Shaban Zuberi Ada huku
washambuliaji wakiwa ni Rashid Mohammed Chambo, Mohammed Abdallah
Rashid, Yohana Oscar Mkomola, Muhsin Malima Makame Vitalis.
Hivi karibuni Serengeti Boys
ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya
Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth
Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu
katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya
tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.
KAMATI YA MAADILI TFF
Kikao cha Kamati ya Maadili ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kiliketi jana Julai 2,
2016 na kupitia malalamiko ya TFF dhidi ya
Nassib Mabrouk - Katibu wa MZFA na
Msimamizi msaidizi wa kituo cha Mwanza
Mbasha Matutu - Mjumbe wa mkutano
mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga).
Jerry Muro, Ofisa Habari wa Young
Africans S.C
Shauri dhidi ya Mabrouk
lilisikilizwa. Lakini mashauri dhidi ya Jerry Murro na Mbasha Matutu,
yaliahirishwa hadi wiki ijayo ili walalamikiwa wapate muda wa kupitia
mashtaka na pia TFF kupata fursa ya kuleta mashahidi wake.
TFF inatoa tahadhari kwa
walalamikiwa kuacha kutumia mitandao ya kijamii kupotosha umma wakati
huu mashauri yao yakiendelea kusikilizwa.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA
TANZANIA-TFF
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni