.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 23 Agosti 2016

MAJALIWA AKAGUA JENZI WA DARAJA LA MTO KAVUU

Ujenzi wa daraja la mto Kavuu wilayani Mlele ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake Agosti 23, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa daraja la mto Kavuu wilayani Mlele Agosti 23, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa daraja la Kavuu linalojengwa na kampuni ya Nandra Engineering and Construction Ltd ya mkoani Morogoro na kumtaka mkandarasi huyo kulikamilisha haraka.

Ujenzi wa mradi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 85.34 ulianza Septemba 2013 na ulitarajiwa kukamilika Septemba 27, 2014. Mradi huo wenye thamani ya sh. Bilioni 2.718 unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

“Serikali imedhamiria kuimarisha barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja. Ujenzi wa daraja la Kavuu utakamilika katika kipindi cha mwaka huu wa fedha hivyo nawaomba muendelee kuiamini Serikali yenu,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele.

“Tumeamua kuwapa kazi wakandarasi wa ndani tunataka mfanye kazi daraja likamilike kwa viwango vyenye ubora ili kuthibitisha kama wasomi wetu mnafanya kazi na hatimaye tuwape kazi nyingine,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kujiepusha na matapeli wanaopita katika maeneo yao na kuwataka wachange fedha za kuanzisha vikundi ili wapewe sh. milioni 50 zilizoahidiwa na Serikali.

“Serikali bado hatujaanza kusambaza fedha hizo. Jihadharini na hao matapeli na wezi hivyo wakija kwenye maeno yenu wakamateni. Zoezi hilo likianza mtajulishwa kupitia halmashauri zenu,” amewasisitiza.

Awali mbunge wa jimbo la Kavuu, Dk. Pudensiana Kikwembe alimuomba Waziri Mkuu kutoa kipaumbele kwenye ujenzi wa daraja la Kavuu ili likamilike mapema na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Pia ameiomba Serikali kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais Dk. John Magufuli ya ujenzi wa barabara ya kutoka Majimoto hadi Inyonga yenye urefu wa kilomita 130 kwa kiwango cha lami aliyoitoa wakati wa kampeni. Waziri Mkuu amesema barabara hiyo itajengwa katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha.



Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Katavi, Mhandisi Abdon Maregesi akizungumzia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja la Kavuu amesema umekamilika kwa asilimia 50 na unategemea kukamilika Novemba 30 mwaka huu.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umekuwa na kasi ndogo kwa sababu ya uhaba wa fedha, ambapo tangu mwaka ulipoanza hakuna fedha zilizotolewa kwa miaka miwili mfululizo (2013/14 na 2014/15) licha ya kuwekwa kwenye bajeti.

“Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa kazi, uhaba wa fedha na mvua nyingi zinazonyesha mkoani Katavi mradi haukuweza kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Kwa sasa mradi unategemea kukamilika Novemba 30, 2016,” amesema.

Mhandisi huyo amesema hadi kufikia Agosti 22, 2016 tayari mkandarasi amekwishalipwa jumla ya sh. bilioni 1.284 ikijumuisha na malipo ya awali. Malipo hayo ni sawa na asilimia 47 ya mkataba.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMANNE, AGOSTI 23, 2016.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni