Na Mathias Canal, Dodoma
Kushindwa kusimamia miundombinu ya maji na kupelekea kuwa na ugumu wa upatikanaji maji kwa kiwango kinachotakiwa ni miongoni mwa kadhia zilizopingwa wakati wa kampeni na Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ambaye ndiye Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kuahidi kuchagua wasaidizi watakaosimamia na kulimaliza jambo hilo mara baada ya kuingia madarakani.
Kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wakitupa
lawama kwa baadhi ya watendaji wa serikali ambao wamesababisha kudorora kwa uchumi na kuchagiza ugumu wa maisha kutokana na umbali wanaotumia kutafuta maji, huduma za afya sambamba na umbali wa shule za Sekondari na Msingi.
Kutokana na kadhia ya upatikanaji hafifu wa maji safi na salama Wilayani Kongwa imepelekea kukalia kuti kavu kwa Meneja wa Mamlaka ya Maji safi na Salama Wilayani humo Ndg Kisha Bonga kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwemo kusababisha wafanyakazi wa Mamlaka ya maji kufikia maamuzi ya kuandamana.
Maandamano ya Wafanyakazi hao yalifanyika siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita yaliyoanzia Ofisi za Mamlaka ya Maji safi hadi ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa wakiwa wamegoma kufanya kazi kutokana na kuchelewa kulipwa mishahara yao.
Katika malalamiko ya wafanyakazi hao yaliyopelekea kugoma kufanya kazi yanachagizwa na kudai mishahara ya zaidi ya miezi nane sasa (8) ikiwa ni muda wenye ishara ya kutolipwa mishahara yao tangu mwaka 2016 ulipochomoza mwanzoni mwa Januari mwaka huu.
Katika malalamiko yao pia wamemlalamikia Meneja huyo wa Mamlaka ya maji Ndg Kisha Bonga kwa kutumia lugha zisizo na staha kwa kuwataka waache kazi wale wote wanaoshindwa kuishi pasina kulipwa mshahara jambo ambalo linawafedhehesha watumishi hao.
Hata hivyo Dc Ndejembi akizungumza na wafanyakazi hao aliwataka kwa umoja wao kurejea Ofisini kwao na kuendelea na kazi huku akiahidi kulivalia njuga jambo hilo kwa kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ili wajue tatizo limeanzia wapi na kwa namna gani linaweza kutatuliwa.
Katika kutaka kutatua mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deogratius Ndejembi alizuru katika ofisi ya Meneja wa Mamlaka ya maji kama alivyotoa taarifa kuwa angefika kukutana nae kwa pamoja washirikiane namna ya kutatua kadhia hiyo lakini Meneja huyo aliondoka na hakurejea tena tena jambo lililomlazimu kufanya kikao na wafanya kazi hao kwa kuanza kuomba kusomewa Mapato na matumizi ili kupata ahueni ya mahali pa kuanzia.
Mamlaka ya maji safi na salama Wilayani Kongwa inakusanya jumla ya shilingi milioni kumi na moja (11,000,000) kwa mwezi fedha ambazo zingeweza kabisa kuwalipa wafanyakazi wote ambao kwa kila mwezi malipo ya mishahara yao haizidi milioni tano 5,000,000 hivyo kushindwa kufanya malipo hayo Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa huo ni uvivu na uzembe katika utendaji.
Fundi Mkuu wa Bomba Wilayani humo pamoja na Mkurugenzi huyo hawajawahi kupitisha hata mwezi mmoja bila kupata malipo ya mshahara wao jambo ambalo limemshangaza Mkuu wa
Wilaya hiyo na hatimaye kufikia maamuzi ya kumsimamisha kazi Meneja wa Mamlaka ya maji Ndg Kisha Bonga kwa kupungua ufanisi wake katika utendaji.
Kutokana na maamuzi hayo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kongwa kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhandisi Ngusa Izengo wamemteua Mhandisi Hamisi Ally kuwa kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji ili kusukuma gurudumu la utendaji kazi
kusonga mbele.
Mara baada ya kukaimu nafasi hiyo Mhandisi Ally aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deogratius Ndejembi kutatua kero ya muda mrefu katika kata ya Chamkoroma kwa hujuma za
wafanyabiashara wa maji kukata bomba na kuliunganisha ili wapate maji wao peke yao na hatimaye kuwauzia wananchi kwa shilingi mia nne kwa kila dumu la lita ishirini.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni