JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu:
255-22-2114512, 2116898
E-mail:
press@ikulu.go.tz
Tovuti :
www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
|
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 06 Septemba, 2016 amewatembelea Wakazi wa Magomeni Kota Jijini
Dar es Salaam ambao nyumba walizokuwa wakiishi katika eneo hilo
zilivunjwa mwaka 2012 kwa makubaliano ya kujengwa nyumba za kisasa na
kuwaahidi kuwa Serikali itaanza kujenga nyumba hizo katika kipindi
cha Miezi miwili kuanzia sasa.
Rais
Magufuli amesema ujenzi wa nyumba hizo utakamilika katika kipindi cha
mwaka mmoja na baada ya hapo Wakazi wote 644 walioondolewa kupisha
ujenzi wa nyumba za kisasa watapatiwa nyumba za kuishi na kwamba
wataishi katika nyumba hizo kwa muda wa miaka mitano bila kulipa
pango na baada ya muda huo kuisha wataandaliwa utaratibu wa kila
mmoja kuuziwa nyumba anayoishi.
"Nakwenda
kutoa pesa Mwezi huu, ili Mkandarasi atakayeteuliwa aanze kujenga
nyumba za wakazi wote 644, wakati wanapojenga hayo majengo ya wakazi
644, ujenzi utaendelea pia katika maeneo mengine, ili kusudi kama
yanajengwa maduka makubwa (Shopping Malls) au zinajengwa nyumba
zingine za wananchi wanaohangaika nao tuwalete hapa.
"Nataka
katika miji yetu ya Tanzania tuanze kupambana na makazi ya wananchi,
tuwe tunajenga nyumba ili hata hawa masikini wa Tanzania waweze
kufaidi kukaa kwenye ghorofa"
Amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na namna tatizo la wakazi
wa Magomeni Kota lilivyoshughulikiwa na amewaahidi kuwa Serikali yake
itahakikisha wananchi hao hawasumbuliwi tena.
Pamoja
na hatua alizochukua kwa wakazi wa Magomeni Kota ambao nyaraka
zimeonesha walikuwa wakiishi katika Nyumba za Shirika la Nyumba
(NHC), Rais Magufuli ameagiza maeneo yote katika mikoa 20 hapa nchini
yenye nyumba za kuishi za NHC kama lilivyo eneo hilo yatwaliwe na
Serikali na kwamba Serikali itatoa maelekezo ya namna yatakavyotumika
ama kuendelezwa.
Pamoja
na kumpongeza kwa kazi nzuri anazofanya, Rais Magufuli amemuagiza
Mtendaji Mkuu wa Shirika na Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Neemia Mchechu
Kyando kuwaondoa wapangaji ambao ni wadaiwa sugu wa pango zikiwemo
Taasisi za Serikali ambazo amezipa siku saba kuwa zimelipa madeni
yao.
"Wale
wapangaji wote lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo,
wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya Ujenzi, Wizara gani kule...
ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao wasipolipa
endelea kuwatoa nje.
"Endelea
hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote, awe amepangishwa ni wa
CCM mtoe nje, awe wa UKAWA mtoe nje, awe Serikali mtoe nje, awe
Waziri Mtoe nje, mpangaji huyo awe ni Rais mtoe nje, ni lazima upate
pesa zitakazowezesha kuendesha Shirika la Nyumba la Taifa"
Amesisistiza Rais Magufuli.
Wakati
huo huo,
Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa
kwa chuo hicho alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa
maktaba ya kisasa ya chuo hicho tarehe 02 Juni, 2016.
Jumla
ya majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja yanajengwa katika eneo hilo
la mashariki mwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yatakapokamilika
tarehe 31 Desemba, 2016 yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 3,840
kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya kuishi
mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.
Akizungumza
na wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Vijana
walioajiriwa katika kazi za ujenzi wa majengo hayo Rais Magufuli
amepongeza moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kufanya kazi usiku na
mchana na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga kuendelea
kuwatumia vijana hao katika miradi mingine ambayo Serikali
itaitekeleza kwa kutumia TBA.
TBA
ikitumia wataalamu na Vijana wa Kitanzania itatumia Shilingi Bilioni
10 kukamilisha ujenzi huo ikilinganishwa na endapo ingetumia
Wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya Shilingi Bilioni 50 na
Bilioni 100.
Rais
Magufuli ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuacha
kuingia mikataba mingine na wafanyabiashara wanaotumia maeneo ya chuo
hicho kujenga majengo ya kibiashara na badala yake amesema Serikali
itaendelea kutafuta namna ya kulimaliza tatizo la mabweni kwa
wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine hapa nchini.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
06
Septemba, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni