Felix Mwagara, MOHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameupongeza Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi ya UDA-RT wa jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi waendelee kuyatumia mabasi hayo wanaposafiri sehemu mbalimbali jijini humo.
Mhandisi Masauni ameyasema hayo jana mara baada ya kusafiri na mabasi hayo kutoka kituo cha mabasi hayo cha Ubungo mpaka katikati ya jiji kwa lengo la kujionea jinsi mabasi hayo ya mwendokasi yanavyohudumia abiria pamoja na kuwapa moyo wananchi kuwa usafiri huo unatumiwa na mwananchi wa aina yeyote.
Akizungumzia usafiri huo, Masauni alisema mradi huo umerahisisha sana usafiri kwani ametumia dakika chake akitokea Ubungo hadi Posta katikati ya jiji bila usumbufu wowote, hivyo mradi huo ameomba uendelee kulindwa pamoja na kutunzwa na UDA-RT na wananchi wenyewe kwa ujumla.
“Mimi kwa kweli nimeufurahia sana usafiri huu, Serikali imefanya jambo kubwa sana kwa wananchi wake, kwa kuwajali wananchi kwa kuuleta mradi huu ambao unarahisisha safari kwa uharaka zaidi na pia unapendezesha jiji kwa jinsi magari yalivyo nadhifu,” alisema Masauni ambaye pia alilipa nauli kwa kupanga foleni kama wananchi wengine wanavyofanya wanapotaka kusafiri na usafiri huo.
Masauni aliongeza kuwa; “Nimefarijika sana na lugha ya adabu na tulivu ambayo wanaitumia madereva wa mabasi hayo wanapowatangazia wananchi vituo mbalimbali vya kushuka na kuingia kwenye mabasi hayo, hii inasaidia kuwa na mawasiliano mazuri na abiria, pia inaonesha madereva hao wamefunzwa vizuri na wanaipenda kazi yao.”
Hata hivyo, Masauni alitoa ushauri kwa uongozi wa mabasi hayo, kuruhusu wananchi waingie ndani ya mabasi hayo kwa idadi ambayo haitaleta kero kwa abiria wengine ili kupunguza wingi wa abiria hao kwa lengo la kuepuka mbanano mkubwa wa abiria.
Pia aliwataka wananchi wa jiji hilo kuyatunza mabasi hayo, na pia kukubali maelekezo ya madereva wanapotoa matangazo wanapokuwa safarini kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji.
Naibu Waziri huyo alipanda mabasi hayo akitokea Ubungo mara baada ya kumaliza ziara yake ya kushtukiza kwa kutembelea Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo kwa lengo la kukagua mabasi mabovu pamoja na usalama wa abiria wanaosafiri na mabasi hayo. Masauni pia alifanya ziara hiyo ya ghafla kwa kutembelea Stendi ya Kibaha, mkoani Pwani.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni