.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 28 Oktoba 2016

BALOZI SEIF AFUNGUA MKUTANO WA KIKANDA WA KIMATAIFA WA SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA, ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa pili kutoka kulia akiwa pamoja na Viongozi waandamizi kabla ya kuufungua Mkutano wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Park Hyatt Mjini Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia wakimsikiliza Balozi Seif wakati akiufungua Mkutano huo.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia wakimsikiliza Balozi Seif wakati akiufungua Mkutano huo.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia.
 
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na Mataifa na Taasisi za Kimataifa kuunga mkono miradi ya Kiuchumi inayoanzishwa na Serikali, lakini bado nguvu za pamoja kwa Taasisi za ndani zinahitajika katika kushirikiana na Serikali kiuendeleza miradi hiyo.

Alisema zipo jitihada zinazofanywa na Serikali kuandaa Sera,mipango na Mikakati ya kujiandaa na miradi mipya kama Mafuta na Gesi asilia ambayo kufanikiwa kwake mbali ya kuinua pato la Taifa lakini pia inaweza kutoa ajira kubwa itakayopunguza wimbi la Vijana wasiokuwa na kazi za kujikidhi kimaisha.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiufungua Mkutano wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Park Hyatt Mjini Zanzibar.

Alisema ingawa usimamizi wa kuendesha miradi ya sekta ya Mafuta na gesi asilia hupangwa na kupewa dhamana wawekezaji kulingana na kiwango cha taaluma walichonacho, hata hivyo jukumu la kusimamia sera litabakia kuwa mikononi mwa wazalendo wenyewe ili kujilinda mapema na changamoto za kimazingira zisizoepukika katika kuendesha miradi hiyo.


Alieleza kwamba Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kipindi kifupi kijacho zinatarajia kuwa na muelekeo wa kuendesha miradi ya mafuta kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu zilizofanywa ndani ya maeneo ya ukanda huu jambo ambalo wasimamizi wa pande zote watalazimika kuwa makini katika kuendesha miradi hiyo itakayokomboa maisha ya Wananchi walio wengi.

Balozi Seif alifahamisha ni muhimu ikaeleweka wazi kwamba miradi hiyo ni fursa nzuri katika maendeleo ya Kiuchumi kwa kuimarika huduma za Kijamii sambamba na uwezekano wa kuirejesha Nchi kujijengea msingi wa mazingira mazuri katika muelekeo wa Uchumi wa wazi unaojitegemea.

Hata hivyo alitahadharisha wazi kwamba wananchi watapaswa kuwa makini katika uendelezaji wa miradi hiyo yenye kutoa mapato makubwa vyenginevyo vurugu mpya zinaweza kuibuka baina ya wawekezaji na wananchi au inawezekana ikawakumba pia wananchi wenyewe kwa wenyewe katika kumiliki utajiri huo mpya.

Alisema ipo mifano mingi na ya wazi iliyokwisha kutokea katika Mataifa yaliyoanza kuendesha miradi hiyo akiyatolea mfano yale yaliyomo ndani ya bara la Afrika ambayo kwa sasa yanaendelea kukumbwa na vurugu tokea kuanza kutekeleza miradi hiyo.

Balozi Seif alisema hakuna njia ya mkato katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo lliloibuka kwenye miradi ya mafuta na Gesi ndani ya Nchi zinazoendelea kuzalisha bidhaa hiyo isipokuwa cha msiongi ni kwa wataalamu waliobobea na kazi hiyo kuendelea kutoa taaluma kwa wazalishaji wapya ili kufaidika vyema na rasilmali hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza watendaji na Wataalamu wa Taasisi ya Uongozi, Wizara ya Ardhi, Makazi, Nishati na Mazingira Zanzibar kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kuendesha mkutano huo wa kikanda unaohusu sekta ya mafuta na Gesi Asilia.

Alisema hatua hiyo ni mwanzo mzuri kwa Mataifa ya Kanda ya Afrika kuanza kuingia kwenye Sekta hiyo katika misingi muwafaka itakayosaidia kuzingatia sheria, sera na mikakati ya kuendesha miradi husika kwa kutangulia amani na kuaminiana.

Mapema Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Uongozi Bwana Dennis Rweyemamu alisema lengo la Mkutano huo ni kuimarisha uwezo wa miundombinu itakayozalisha fursa za ajira miongoni mwa nchi wanachama wa Kikanda.

Bwana Dennis aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi iliyochukuwa ya kujenga mazingira yaliyowezesha kufanyika na hatimae kufanikiwa kwa Mkutano huo wa Kikanda.

Akitoa Taarifa katika Mkutano huo wa Kikanda Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Mazingira Ndugu Ali Khalil Mirza alisema mswada wa sheria ya kuazishwa kwa Taasisi itakayosimamia Masuala ya Mafuta na Gesi asilia umeshajadiliwa na kupitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Nd. Mirza alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa inaangalia zaidi mtazamo wa kushirikiana na Wataalamu wa Nchi na Taasisi za Kimataifa katika muelekeo wa kuanza vyema kwenye Sekta hiyo mpya ya Mafuta na Gesi Visiwani Zanzibar.

Mkutano huo wa Kikanda wa Kimataifa wa Siku Mbili unaohusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi umeshirikisha wajumbe kutoka Mataifa ya Sierra Leone, Afrika Kusini, Uingereza, Ghana, Uganda, Senagal, Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar.

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar



Hakuna maoni :

Chapisha Maoni