Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda
Balozi Seif akizungumza na wana CCM na Wananchi wa Matawi ya
Mangapwani na Mangapwani Bondeni katika Mkutano wa kutoa shukrani
baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu.
Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh.
Bahati Ali Abeid akisisitiza Jambo wakati wa Mkutano wa kushukuru
wapiga kura wake baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu hapo Tawi la
CCM Mangapwani.
Baadhi ya Viongozi wa Kamati za
Siasa na wana CCM wa Matawi ya Mangapwani na Mangapwani Bondeni
wakifuatilia hotuba ya Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo la Mahonda
hawapo Pichani Balozi Seif na Mh. Bahati waliofika kutoa shukrani
baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu. Picha na OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Viongozi na Wanachama wa Chama cha
Mapinduzi {CCM } ngazi ya Matawi Nchini wameagizwa kujipanga vyema
ili kuhakikisha Viongozi watakaowachagua wakati utakapowadia wa
uchaguzi ndani ya chama hicho hapo mwakani wana sifa sahihi
zitakazokidhi mahitaji yote ya kuwatumikia wanachama hao katika
kipindi cha miaka Mitano ijayo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati
akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za Matawi ya Mangapwani na
Mangapwani Bondeni katika mkutano wa kuwashukuru wanachama hao baada
ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu uliopita.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda akiambatana pamoja na Mbunge wa Jimbo
hilo Mh. Bahati Ali Abeid na Madiwani wa Wadi zilizomo ndani ya Jimbo
hilo alisema CCM ikiendelea kujipanga vyema kwenye chaguzi hizo
itakuwa na uhakika wa kuendelea kuongoza Dola ya Watanzania katika
miaka mingi ijayo.
Alisema wapo baadhi ya wapinzani
walijipenyeza kwenye chaguzi za Chama hicho mwaka 2012 na kuomba
Uongozi wakitumia hila na ujanja wa fedha na hatimae kuwayumbisha
Viongozi na Wanachama wakati wa kupanga safu ya utekelezaji wa Ilani
na Sera za CCM.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM
Taifa aliwapongeza Wana CCM na Wananchi wa Mangapwani kwa uamuzi wao
walioufanya mwezi Oktoba mwaka 2015 na Machi 2016 wa kuipa dhamana
CCM iendelee kuongoza Dola ya Tanzania katika chaguzi zote mbili ile
ya Zanzibar na ya Tanzania.
Balozi Seif alisema kazi
inayowakabili Wananchi kwa hivi sasa ni kuelekeza nguvu zao katika
kuimarisha miradi ya Kiuchumi na Maendeleo na kwa upande wa Uongozi
wa Jimbo hilo tayari umeshajipanga kuhakikisha changamoto
zinazowakabili Wananchi wa Maeneo hayo zinapatiwa ufumbuzi muwafaka.
Alisema yeye pamoja na Mbunge wake
Mh. Bahati watashirikiana na viongozi wa Jimbo hilo ngazi ya Jimbo na
Matawi katika ujenzi wa Jengo Jipya la Ofisi ya CCM Tawi la
Mangapwani Bondeni litakalolingana na hadhi ya Chama chenyewe.
Balozi Seif aliwahakikishia Viongozi
na Wanachama wa CCM wa Tawi la Mangapwani Bondeni kwamba yeye binafsi
pamoja na Viongozi wenzake atasimamia maandalizi ya kuanza kwa msingi
wa ujenzi wa Jengo hilo ili kuondoa kiu ya muda mrefu waliyokuwa nayo
Wanachama hao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh.
Bahati Ali Abeid aliwathibitishia Wanachama na Viongozi wa Matawi
hayo kwamba juhudi za awali zimeanza kuchukuliwa katika mwanzo wa
kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo
hayo.
Mh. Bahati alisema katika
utekelezaji wa ahadi, Ilani na Sera za Chama cha Mapinduzi za
kusimamia upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa wananchi
wa Matawi hayo Uongozi wa Jimbo hilo umeanza harakati za kuliondosha
tatizo hilo sugu linalowakabili Wananchi hao.
Alisema ulazaji wa mabomba ya maji
katika mradi maalum ulioanzishwa unatekelezwa katika Vijiji vya
Kiomba Mvua, Fujoni na Mangapwani na kilichobakia kwa wakati huu ni
Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kukamilisha uwekaji wa Mashine ya
kusukumia Maji katika kisima kilichochimbwa kwenye eneo hilo.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mahonda
alifafanua zaidi kwamba juhudi hizo za uimarishaji wa miundombinu
katika Sekta ya Maji zimechukuliwa kwa makusudi na Uongozi wa Jimbo
hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar baada ya kubaini
kwamba Kisima kilichokuwa kikisambaza huduma ya maji katika kijiji
hicho kiliopo Mfenesini kuzidiwa mara dufu.
Akigusia uhai wa Chama cha Mapinduzi
Mh. Bahati aliwakumbusha Wanachama wa Matawi hayo kuhakikisha
wanalipa ada zao kama kawaida bila ya kusibiri kusukumwa kufanya
hivyo ili kukipa nguvu chama chao kiweze kutekeleza majukumu yake
kama kawaida.
Mapema Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la
Mahonda ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa la Wilaya ya Kaskazini
“B” Mama Asha Suleiman Iddi waliwanasihi Wazee wa Vijiji hivyo
Kuanzisha Kamati ya maadili itakayosaidia kutoa elimu kwa vijana
waliojitumbukiza katika matumizi ya Dawa za kulevya.
Mama Asha alisema inasikitisha kuona
jitihada kubwa zilizochukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo kwa kutumia
fedha nyingi katika kuwapatia ushauri nasaha vijana hao kwenye nyumba
za kurekebisha tabia { Sober House } hatimae ziligonga mwamba.
Alisema Kamati itakayoundwa katika
Kijiji hicho cha Mangapwani itapaswa kwenda kujifunza kwa Kamati kama
hiyo iliyoanzishwa katika Kijiji cha Fujoni ambayo imeleta mafanikio
makubwa katika kukabiliana na wimbi la vijana waliojitumbukiza katika
wimbi la matumizi ya dawa za kulevya.
Mama Asha alieleza kwamba Vijana wa
Fujoni walioamua kuacha dawa hizo tayari hivi sasa wamekuwa na
mafanikio makubwa katika muendelezo wa mradi wao wa Uvuvi unaokidhi
mahitaji yao ya kimaisha baada ya kupatiwa msaada wa Boti pamoja na
Mashine yake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
08/10/2016.



Hakuna maoni :
Chapisha Maoni