Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika, Issa Hayatou ameteua Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kuwa miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati
maalumu ya mageuzi ya muundo wa CAF itakayokuwa na jukumu la kufanya
mabadiliko mapya ya shirikisho, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, katika
Kamati hiyo ikayoongozwa na Rais Issa Hayatou mwenyewe, Malinzi
ameteuliwa katika Kamati hiyo iliyotangazwa leo Oktoba 30, 2016
kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Kamati hiyo imeundwa ikiwa ni
sehemu ya maazimio ya mkutano uliopita wa kawaida wa CAF uliofanyika
Septemba 29, mwaka huu ambako Rais Hayatou amezingatia mjadala
uliolenga kufanya mabadiliko CAF kwa kufanyia kazi mara moja.
Hayatou si tu kwamba amejali mjadala
wa mkutano ule, pia ameheshimu mawazo ya vyama wanachama vya nchi
pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wataalamu mbalimbali ili
kupata mustakabali wa muundo wa uongozi wa shirikisho hilo ili
kukabiliana na changamoto dhidi ya mpira wa miguu barani Afrika.
Akizungumzia uteuzi huo, Malinzi
kwanza alimshukuru Hayatou kwa uteuzi huo ambao umeonyesha moja kwa
moja kuwa na imani naye katika kuleta maendeleo ya mpira wa miguu
katika muundo mpya.
“Lakini sifa hii ya kuteuliwa ni
yangu pekee kwani ni heshima kubwa ambayo imepewa nchi yetu pendwa ya
Tanzania, kadhalika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati,” alisema
Malinzi alipozungumza namtandao wa TFF ambao ni www.tff.or.tz.
Kamati hiyo itawajibika kwa Kamati
ya Utendaji ya CAF ili kupata mwongozo ingawa haibanwi zaidi na
Katiba ya shirikisho.
Kamati inaundwa na:
1. Issa Hayatou (Cameroon), ambaye
ni Rais CAF atakayekuwa Mwenyekiti.
2. Amadou Diakite (Mali), Makamu
Rais wa CAF na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho.
3. Mohammed Raouraoua (Algeria),
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji CAF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Masuala
ya Sheria. Pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Algeria
(FAF).
4. Lydia Nsekera (Burundi) Mjumbe wa
Baraza la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
5. Raymond Hack (Afrika Kusini),
Mwenyekiti wa Bodi ya Nidhamu ya CAF.
6. Me. Prosper Abega (Cameroon),
Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya CAF.
7. Jamal Malinzi (Tanzania), Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
8. Me. Augustin Senghor (Senegal),
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal (FSF)
9. Victor Adolfo Osorio (Cap Verde),
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Cap Verde (FCF)
10. Maclean Letshwti (Botswana),
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Botswana (BFA)
11. Hicham El Amrani (Morocco)
ambaye ni Katibu Mkuu wa CAF.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni