Ligi ya Taifa ya Wanawake
inatarajiwa kuanza kesho Jumanne Novemba 1, 2016 kwa viwanja sita
kuchezwa mechi za ufunguzi ingawa hafla ya uzinduzi wa ligi hiyo
utafanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo ambao Baobao
ya hapo itakapocheza na Victoria Queens ya Kagera.
Ligi hiyo ya kwanza kufanyika nchini
Tanzania, lakini pia kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati imetokea
kuvutia wadau kadhaa wakiwamo Azam Tv ambao wamedhamini kwa kuonyesha
mubashara (live), michezo hiyo 30 itakayofanyika viwanja mbalimbali
hapa nchini.
Viongozi mbalimbali wa Serikali
wakiwamo mawaziri na wabunge ambao kwa sasa wako kwenye vikao mjini
Dodoma kwa pamoja wanatarajiwa kuwa katika hafla hiyo ambayo
pilikapilika zake zinatarajiwa kuanza saa 8.00 mchana kabla ya mchezo
kuanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
TFF imepeleka uzinduzi huo Dodoma
ikiwa na lengo la kuhamasisha soka mikoani tofauti na Dar es Salaam
ambako ilizoeleka zaidi miaka ya nyuma kabla ya kuwa na mpango wa
mashindano ya aina hiyo yanayoshirikisha timu 12 kutoka kona
mbalimbali za nchi.
Kadhalika, kwa siku ya Novemba mosi
ya uzinduzi huo vingozi wengi wa Serikali wakiwamo wabunge wanatajiwa
kuwa Dodoma ambako watapata fursa pekee ya kushuhudia burudani ya
mpira wa miguu wa ushindani itakayosukuma hamasa ya kutoa michango
yao mbalimbali kwa ajili ya soka la wanawake.
Mbali ya mchezo huo wa kundi B kati
ya Baobao na Victoria, michezo mingine itakuwa ni kati ya Sisterz na
Panama utakaofanyika Uwanja wa Tanganyika huko Kigoma wakati Marsh
Academy ya Mwanza itacheza na Majengo Women ya Singida kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kundi A kutakuwa na michezo mitatu
ambako Viva Queens ya Mtwara itacheza na Mburahati Queens ya Dar es
Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Fair Play ya Tanga
itapambana na Evergreen ya Dar Salaam katika mchezo utakaofanyika
Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku JKT Queens ikiwa ni wenyeji wa
Mlandizi Queens ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni